Ticker

6/recent/ticker-posts

Wanawake Wachangamkiee Fursa Za Uongozi


Na Amrat Kombo, Zanzibar:


VIONGOZI watatu waandamizi serikalini akiwemo Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, wametoa maoni kutaka mfumo maalum wa kusaidia wanawake kupata nafasi zaidi za uongozi.

Kila mmoja kwa wakati wake, viongozi hao walipozungumza katika mahojiano binafsi, wamesema ni muhimu watu kubadilika na kufikiria namna bora ya kuwapatia wanawake fursa ya kuwa viongozi kama ilivyo kwa wenzao wanaume.

Wakati Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mgeni Hassan Juma anahimiza wanawake kuchangamkia nafasi za uongozi ili kutetea haki na maslahi yao na watoto, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Siti Abbas Ali anasikitika kuendelea kwa utamaduni wa jamii kuona uongozi ni fursa inayomfaa tu mwanamme na kusahau kuwa hata mwanamke ametokana na Adam Na Hawa, kama historia inavoelekeza.

Naibu Spika Mgeni aliyehojiwa akiwa nyumbani kwake Tunguu, nje kidogo ya jiji la Zanzibar, amesema matatizo mbalimbali yanayomkabili mwanamke na watoto yanaelekea kumhitaji sana kiongozi mwanamke ambaye haraka hupata hisia kali anapoyaona na hubakiwa na mzigo wa athari yakishatokea.

Bi Mgeni anasema mwanamke akipata uongozi imani hujengeka kwamba huwa mstari wa mbele kupigania maslahi ya mwanamke na mtoto katika nchi akitoa mfano wa tatizo linalokua la udhalilishaji.

Hata hivyo, analalamika kuwepo mazingira yanayokwaza wanawake kupata nafasi za uongozi hivyo wachache mno kufanikiwa kupenya. 

"Muamko wa wanawake kushiriki kutafuta uongozi ni mdogo  kutokana na hofu, vitisho na dhana potofu.

"Tunakutana na changamoto nyingi zinazotukwamisha kuingia kwenye uongozi. Mtu unashindwa kugombea jimbo kutokana na ugumu wa kupambana na mwanamme. Hili jambo si rahisi kwetu wanawake," anasema.

Anasema kwa upande mwengine ni haki ya kikatiba mwanamke kuwa kiongozi na kwamba akiingia humsaidia kunufaika kiuchumi na kuendeleza familia yake.

Naibu Spika Mgeni akatoa nasaha kwa taasisi za serikali na za kiraia kujitahidi kubuni mifumo itakayosaidia kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi za uongozi.

"Tunahitaji mabadiliko. Angalia hapa petu Zanzibar kwa sababu ya mfumo mbaya, katika majimbo 50 ya uchaguzi, tunao wawakilishi wanane tu waliochaguliwa majimboni. Utadhani hakuna wanawake majimboni au labda hawataki. Hapana. Wanahofia mapambano na wanaume," alisema.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Bi Siti anasema,

"Kwenye shehia zetu kunaanzishwa kamati tofauti kuhusu afya, mazingira, elimu masuala yanayohusu kila mtu lakini utakuta wajumbe wengi ni wanaume kama vile Shehia haina wanawake wenye uwezo.

"Baadhi ya changamoto zinazokwamisha wanawake kugombea jimboni ni mtu kuona atashindwa tu maana atapambana na mwanamme na mitazamo ya wananchi ni kuamini zaidi wanaume katika uongozi kuliko wanawake.

"Wanawake wengi ndio wapiga kura, tukisimama kwa pamoja katika kumnyanyua mwanamke itasaidia wengi kushika nafasi lakini mfumo waliotujengea wazee wetu kuona mwanamme ndo anapaswa kuwa kiongozi tunakwama."

Kwa kuliona hilo, Wizara yetu hujenga njia ya kuhamasisha wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo kutambua na kuzidai haki zao, katika ajira, elimu ya uongozi."

Mkurugenzi wa Uchaguzi Zanzibar ( ZEC), Thabit Idarous Faina amesema hali halisi ya viongozi wanawake Zanzibar kupitia nafasi ya uwakilishi kwenye majimbo 50 ya Zanzibar ni idadi ya mawaziri sita katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, sawa na asilimia 33, makatibu wakuu ni saba ambayo ni sawa na asilimia 39.

Kuhusu wakuu wa mikoa, alisema yupo mwanamke mmoja tu, ikiwa ni sawa na asilimia 20; wakuu wa wilaya wapo wanane ambayo ni sawa na asilimia 36 na Masheha 389 waliopo nchi nzima, 68 tu ndio wanawake ambayo ni asilimia 17.

Ametaja vikwazo vinavyozuia mwanamke kuingia kusaka uongozi ni pamoja na woga wa mwanamke na zile hatua ngumu za kupita mpaka kufikia kuwa kiongozi wa wananchi.

Post a Comment

0 Comments