Ticker

6/recent/ticker-posts

Wagombea Nafasi Za Uongozi Wapewa Somo

 Na Ahmed Abdulla, Zanzibar:

Wanawake wametakiwa kujiamini na kuwa na misimamo imara yenye lengo la kuleta mabadiliko katika nchi.

Hayo yamesemwa na Dk Mzuri Issa Ali wakati akizungumza na wanawake wenye kutia nia kugombea nafasi za Uongozi kutoka vyama mbali mbali vya siasa katika hafla iliofanyika huko Tunguu Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.

Dk Mzuri amesema wanawake wasirudi nyuma na kubabaisha na maneno ya baadhi ya watu wasiopenda maendeleo ya wanawake kwa kuwakatisha tama na kuwaekea vikwazo mbali mbali ili wasiweze kutimiza adhma yao hiyo.

Amesema utafiti uliofanywa kisayansi wanawake wana uwezo wa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja ukilinganisha na wanawake hivyo wanawake waitumie fursa hiyo ili kufikia malengo yao.

“Mwanamke anaweza kuwa mke,mama,kiongozi na wakati huo huo pirika za nyumbani zinamsubiri kama vile kulea watoto huku akiwa anafuwa nguo,anachota maji,anapika na kazi zote hizo anazifanya kwa wakati mmoja tofauti na mwanamme yeye akiwa anasoma gazeti hata kumsemesha hakujibu kwake inakuwa ni shida,” Dk Mzuri.

Naye Mwakilishi mstaafu wa Jimbo la Magomeni Bi Hafsa Said amesema katika kupigania nafasi ya Uongozi alikutana na vikwazo mbali mbali lakini si jambo ambalo lilimkatisha tama bali alipambana na hatimae kushika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka kumi.

Bi Hafsa amesema jambo ambalo lilimfanya kudumu katika nafasi hiyo kwa kipindi chote hicho ni kujiuamini ,kujiheshimu pamoja na mashirikiano na wananchi bila kujali rangi, dini, kabila wala kujali itikadi zao za kisiasa bali alihudumia watu wa aina zote.

“Mimi sikujali watu wa chama changu tu kwa sababu hata wananchi wa chama cha upinzani walinipigia kura kwa hiyo wote ni wananchi wangu na maendeleo niliyaleta kwa wote, na nikauunda kamati ya sheha nikashirikisha watu wa chama changu cha CCM na chama cha Upinzani tukafanya kazi” Bi Hapsa.

Nae Kiongozi wa Dini ya Kiislam Ukhti Amina Salum Khalfan amesema dini ya kiislam haijakataza mwanamke kuwa kiongozi bali baadhi ya watu hutumia kipengele cha dini kwa lengo la kuwakandamiza wanawake kwa malengo yao binafsi.

“Aya ya mwanzo katika kitabu kitukufu cha (Qur  an) ilimfikia Bibi Khadija ambae alikuwa mke wa bwana Mtume Muhammad (S.A.W) kama vile Suratul Mujadila na Nnisai ni mfano dhahir uliotumika kuonesha mwanamke ni kiongozi , hata masahaba waliambiwa wachukuwe Elimu(kusoma) kwa bibi Aysha (R.A.), Siasa isiwe sababu ya kunyoosheana vidole “, Ukhti Amina.

Mapema  mratibu wa mradi wa kuinuwa wanawake katika harakati za Uongozi  kutoka TAMWA,ZANZIBAR Maryama Ame Choum amesema wametowa mafunzo kwa wanawake wapatao themanini kwa Unguja na Pemba kutoka katika vyama vya siasa na wanafunzi kutoka vyuo vikuu , ambapo kupitia mafunzo hayo  wanatarajia wanawake wengi Zanzibar watajitokeza kugombea nafasi za Uongozi katika Uchaguzi mkuu wa October 2025.

Nao baadhi ya wanawake  watia nia ya kugombea nafasi za Uongozi  wamesema watasimama imara kuondosha hofu na kuhakikisha wanagombea nafasi za Uongozi kuanzia jimbo hadi Taifa kwa lengo la kuleta mabadiliko katika Taifa hili.

                                          

Post a Comment

0 Comments