Na Amrat Kombo, Zanzibar
Tanzania imeridhia mikataba mbalimbli ya kimataifa inayozisisitiza nchi wanachama kuchukua hatua ya kukuza uongozi shirikishi kwa wanawake na wanaume.
Miongoni mwa mikataba hiyo ni Kutokomeza aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake (The convention on the Elimintation of all Forms of Discrimination against Women -CEDAW) uliopitishwa New York, ,Marekani kwa Azimio la Baraza kuu la Umoja wa Mataifa namba 34\180 la tarehe 18 Disemba 1979.
Kwa kuridhia mkataba huu, nchi wanachama zinakubali wajibu wao wa kuweka usawa kati ya wanaume na wanawake katika mfumo wake wa kisheria na kitaasisi.
Katika kudhihirisha kuridhia kwake ni kwa vitendo na sio mdomo mtupu, hili limewekwa wazi katika katiba ya Zanzibar.
Hatua hiyo pia imo katika kifungu cha 21 cha Sharia ya Vyama Vingi ya Siasa ya mwaka 1992 inayosema kila Mzanzibar anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi.
Kwa bahati mbaya, licha ya hayo yote bado wanawake wamekuwa wakikumbana na changamoto ambazo zinawarudisha nyuma katika kufikia malengo yao ya kushika nafasi za uongozi.
Miongoni mwa changamoto kubwa ni vikwazo vya malezi ya familia ambavyo humjenga mtoto wa kike aone na kuamini kuwa hawezi kuwa kiongozi kutokana na jukumu alilonalo la kulea familia.
Athari ya mtazamo huu tunaiona katika familia zetu na jamii kwa jumla na hili linathibitisha ule msemo maarufu wa Waswahili wa mtoto umleavu ndio akuavyo.
Hata hivyo, juhudi za mwanamke za kuipata hai ya uongozi ambayo wameporwa kwa visingizio mbali mbali zimenedelea kuonekana kukua kwa kasi kidogo katika miaka ya karibuni.
Miongoni mwa vielelezo hivyo ni kwa baadhi yao kusonga mbele na kugombania nafasi mbalimbali za uongozi.
Wengi wao wamedhihirisha kumudu harakati za uongozi bila ya kuathiri malezi ya familia kutokana na kujua majukumu yake.
Fatma Fereji, ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu wa Chama Cha ACT Wazalendo, alisema kutokana na majukumu yake ya uongozi hakuwahi kuitenga familia yake wala kuikwepa kutokana na majukumu ya uongozi.
Mwana mama huyu ambaye pia aliwahi kuwa waziri katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar alisema anaamini kiongozi mzuri mwanamke hawezi kutekeleza familia yake kutokana na majukumu yake ya uwongozi.
Alisema kinachotakiwa ni kutenga muda na ikiwezekana kupata msaidizi wa kushughulikia familia.
Fatma alikumbusha kwamba familia huwa ni kitovu cha maendeleo,furaha na ustawi wa maisha na ni katika familia ndio hujifunza umoja,upendo na uongozi .
“Kila mzazi anawajibu wa kuhakikisha familia yake ipo salama’’, aliongeza
Aliwaasa viongozi wanawake wasijaribu kutenga familia zao kwani huko ndipo kwenye chanzo cha kupata faraja na nguvu za kuweza kufanya kazi vizuri.
Diwani wa Kiongoni, Zawadi Hamdu Vuai,alisema kiongozi mwanamke anaweza kuishughulikia familia yake bila ya kuwepo vikwazo vyovyote na kuwepo maelewano.
Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma, alisema uongozi wake haumfanyi atenge familia yake licha ya kuwa na majukumu mengi,Kwake yeye wajibu wake kwa familia unakuja kwanza.
“Nikiwa nyumbani napendelea kupika,kujadiliana mambo mbalimbali na mume wangu na wazazi. Vilevile huwapa nasaha za maisha watoto wangu,kwahiyo uongozi wangu haunifanyi kuwa mbali na familia yangu.” Aliongeza.
Mwakilishi wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja, Panya Ali Abdallah, alisema Uwongozi ni cheo ambacho unapewa katika familia hadi kufikia kwa wananchi na hii inatokana na kukubali majukumu uliopewa.
Hata hivyo, kushika nafasi ya uongozi haimaanishi kuyatupa majukumu yako katika familia.
Alisema utunzaji wa familia husaidia kupata watoto wenye madili,imani na wenye kujiamini na huenda wakainukia kuwa viongozi bora wa badaye.
“Sisi ni viongozi, lakini pia ni wazazi ambao tunategemewa na familia zetu. Kwahiyo ni lazima tutekeleze majukumu ya malezi ili tuweze kupata baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.” Alisisitiza.
Maryam Ame Chum ambae ni Mratibu wa Mradi wa kuwawezesha Wanawake katika Uongozi Kutoka Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake -Zanzibar (TAMWA) alisema mwanamke anaweza kuongoza na huku akilea familia yake bila ya vikwanzo vyovyote.
‘’Suala la malezi sio la mama peke yake,bali na baba anajukumu lake kama mwanafamilia. Wapo wanaoona mwanamke akiwa kiongozi atakuwa hana mda wa kumlea mtoto wake, jambo ambalo halina ukweli,” Aalisisitiza.
Alisema anawajua viongozi kadha wanawake ambao wanafanya kazi zao za nyumbani kama kawaida na baaadhi ya watu hushangaa wanapowaona wanapika, wanafua na kufanya kazi nyengine za nyumbani.
Utafiti wa awali umeonyesha kiongozi anaeshindwa kukuza na kuongoza familia yake ipasavyo hatoweza kuongoza jamii katika ngazi ya juu.
Aisha Haji, mkaazi wa mwanakwerekwe anaona moja ya vigezo muhimu kwa mtu anataka kuwa kiongozi basi huo uwezo kwanza uonaekana ndani ya familia yake kwani huko ndio chanzo cha kujenga mtu kuweza kuongoza.
Khamis Ali mkaazi wa kikwajuni alisema ni vizuri kuwaunga mkono wanawake kwasababu wao ndio wenye uzoefu mkubwa wa uongozi.
Hii huanzia kwa kuendesha familia na kupitia mambo mengi katika safari yao ya kulea . Kwahiyo wanapotamani kujiunga katika nafasi tofauti ambayo inapelekea kuleta maendeleo ni vyema kuwapatia fursa.
0 Comments