Ticker

6/recent/ticker-posts

NCA Yazindua "Tumbe Bodaboda Peace Club" Vijana Waanza Safari ya Mshikamano

 


Shirika la Norwegian Church Aid - NCA limezindua rasmi Klabu ya Amani ya Bodaboda -Tumbe Bodaboda Peace Club, inayowaleta pamoja vijana waendesha bodaboda wa kijiji cha Tumbe, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, kwa lengo la kuwa mabalozi wa amani, mshikamano na majadiliano ya kujenga jamii salama. Klabu hiyo ina wanachama 25, wote wakiwa vijana wa bodaboda ambao ni sehemu muhimu ya jamii ya Tumbe na wanaochangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za kijamii na kiuchumi.

Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa soko la wajasiriamali uliopo Tumbe Mabatini n ani sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Swahili Coast, unaofadhiliwa na Royal Norwegian Embassy na kutekelezwa na NCA, ukilenga kuhamasisha ushirikiano wa kiimani, uwezeshaji wa vijana na wanawake, pamoja na kuzuia misimamo mikali katika ukanda wa pwani ya Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi, Doreen Bwogi, Mratibu wa Mradi wa Swahili Coast kutoka shirika la NCA Pemba, alieleza kuwa, kuanzishwa kwa klabu hii ni hatua muhimu katika kuwakabidhi vijana nafasi ya kuwa walinzi wa amani ya jamii yao. “Waendesha bodaboda mara nyingi wamekuwa wakionekana kama chanzo cha migogoro, lakini kwa mtazamo wetu wao ni sehemu ya suluhisho. Klabu hii imeanzishwa kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuwa viongozi wa mabadiliko chanya,” alisema Doreen

Doreen alieleza kuwa NCA itaendelea kushirikiana na vijana hao katika kuhakikisha wanakuwa na uelewa wa kutosha juu ya masuala ya amani, uraia, usalama wa jamii na mapambano dhidi ya misimamo mikali. “Tumbe Bodaboda Peace Club siyo tu klabu, ni harakati ya kuimarisha ustawi wa kijamii kwa kutumia vijana kama daraja la mabadiliko,” aliongeza.

Katika hatua nyingine ya tukio hilo, Khelef Nassor,  Afisa Utekelezaji Mradi Msaidizi kutoka NCA, alitoa mafunzo kwa wanachama wote wa klabu, na kuwapa mwongozo wa namna ya kuendesha klabu hiyo kwa ufanisi. Alisisitiza umuhimu wa kuwa na vikao vya mara kwa mara, kuwa na uongozi shirikishi, na kushirikiana na taasisi za serikali, dini na usalama katika kulinda amani ya kijiji.

“Klabu hii inapaswa kuwa mfano wa namna ambavyo vijana wanaweza kuwa mstari wa mbele katika kusimamia masuala ya amani. Mnapaswa kuwa macho ya jamii yenu, mtambue viashiria vya migogoro mapema, mkatae kuingizwa kwenye ajenda za vurugu, na kuwa sehemu ya usuluhishi,” alisema Khelef wakati akizungumza na wanachama wa klabu.  


Afisa Utekelezaji Miradi Msaidizi wa NCA ndugu Khelef Nassor akitoa mafunzo na muongozo wa "Tumbe Bodaboda Peace Club" kwa wanachama

Mafunzo hayo yalihusisha pia mijadala ya wazi kuhusu uongozi chanya, wajibu wa raia, usalama wa kijamii, na namna ya kushughulikia changamoto za vijana wa bodaboda kwa njia ya mazungumzo na siyo kwa mabavu.

Wanachama wa klabu walipata nafasi ya kutoa maoni yao na kuelezea namna wanavyoiona klabu hiyo kama fursa ya mabadiliko.  Ali Matar, mmoja wa wanachama wa klabu, alisema: “Tulizoea kuitwa wahuni, tukatengwa kwenye vikao vya kijamii. Leo tuna klabu yetu, tunapewa nafasi ya kushiriki kwenye maamuzi na kuelimika kuhusu amani. Hii ni hatua kubwa kwetu.”

Ai Matar Mwanachama wa "Tumbe Bodaboda Peace Club" akitoa shukrani zake kwa NCA

Kwa upande wake, Mohammed Kombo, dereva wa bodaboda, alisema kuwa klabu hiyo imekuja wakati muafaka ambapo vijana wengi wanahitaji miongozo ya kuacha vishawishi vya vurugu na kujielekeza katika maendeleo. “Klabu hii imenipa nguvu. Sasa najua siyo lazima kuwa mkali au mkimya ili usikike, unaweza kusikilizwa kwa sababu ya mchango wako kwa jamii,” alisema.

Wanachama walitumia fursa hiyo kutoa shukrani kwa shirika la Norwegian Church Aid - NCA na wafadhili wa mradi kwa kutambua nafasi ya vijana wa bodaboda katika kuleta amani. Waliahidi kushirikiana kwa karibu na uongozi wa kijiji, shehia, na viongozi wa dini katika kuimarisha usalama na mshikamano.

Akitoa salamu za uongozi wa shehia, Naibu Sheh awa shehia ya Tumbe Mashariki Bwana Makame Hassan Makame, alitoa pongezi kwa NCA na vijana wa bodaboda kwa kuanzisha klabu hiyo ya kipekee. Alieleza kuwa ni mara ya kwanza katika shehia yake kuona kundi la vijana wa bodaboda wakikusanyika si kwa ajili ya kazi pekee, bali kwa ajili ya kuijenga jamii yao. “Vijana hawa wameamua kusimama upande wa amani. Kama uongozi wa shehia, tutaendelea kushirikiana nao bega kwa bega kuhakikisha klabu hii inakuwa dira kwa vijana wengine. Naamini kupitia klabu hii, Tumbe itakuwa mfano wa kuigwa katika Pemba nzima,” alisema Makame.

Uzinduzi huo wa klabu ya amani ya Bodaboda umefungua ukurasa mpya kwa vijana wa Tumbe, ambapo sasa wana jukwaa rasmi la kushiriki katika maamuzi ya kijamii, kushiriki mafunzo ya uongozi, na kuandaa kampeni mbalimbali zenye kuhamasisha mshikamano, usalama barabarani na maendeleo.

Kwa maneno ya wanachama wenyewe, “Tumbe Bodaboda Peace Club” ni zaidi ya klabu, ni harakati ya kizazi kipya cha vijana waliojitoa kulinda amani, kuunganisha jamii, na kusimamia mabadiliko ya kweli.

Wanachama wa "Tumbe Bodaboda Peace Club" wakifatilia mafunzo kwa umakini



Post a Comment

0 Comments