Ticker

6/recent/ticker-posts

Sheria Kandamizi Kwenye Tasnia Ya Habari Bado Kigugumizi

 


Na Berema Nassor:

Takriban zaidi ya miaka 10 sasa wadau wa habari na waandishi wa habari Zanzibar wanalilia mabadiliko ya sheria za habari ambazo ndani yake kuna vifungu vinavyokwaza na kuminya uhuru wa habari nchini.

Wadau hao wakiwemo Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania Zanzibar (TAMWA-ZNZ), MCT, WAHAMAZA, ZPC hawajakata tamaa katika kufanya uchechemuzi kwa lengo la kupata kile ambacho wanahisi kitakuwa mkombozi katika tasnia yao.

Hamasa ya  kuripoti na kuandika taarifa zinazohusu umuhimu wa  uhuru wa habari,  uhuru wa kupata taarifa na uhuru wa kujieleza kwa waaandishi na vyombo vya habari ndio kipaombele kikubwa  ambapo kwa sasa umuhimu huo unaonekana kwa asilimia ndogo katika visiwa vya Zanzibar.

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Dkt. Mzuri Issa, amehimiza vyombo vya habari kuripoti kwa kina mapungufu ya sheria za habari za Zanzibar ili zifanyiwe marekebisho na kutoa fursa kwa wananchi kupata habari bila vikwazo.

"Waandishi wa habari tutumie nafasi kupaza sauti zetu juu ya mapungufu ya kisheria yaliyopo ili zifanyiwe marekebisho, hii itawapa watu furaha na kujisikia kuwa ni sehemu ya nchi kwa kutoa maoni yao bila hofu,” alieleza Dkt. Mzuri.

Alibainisha kuwa waandishi wa habari wakiwa na uwezo wa kutoa maoni yao bila hofu itarahisisha upatikanaji wa taarifa na kuongeza uwajibikaji katika nyanja mbalimbali.

"Kukiwa na uhuru wa habari itasaidia kupunguza madhaifu yaliyopo kwenye sekta ya habari kwa kudhibiti waandishi holela wanaotoa taarifa feki na kuifanya sekta ya habari kuwa imara na kutoa taarifa ambazo zinakidhi misingi ya uandishi." Alieleza.

Kwa upande wake mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar Said Suleiman Ali ambae pia ni mchambuzi wa sheria mbali mbali za habari wa habari alisema uchambuzi wa sheria hizo umebaini kuwepo baadhi ya vifungu vinavyokwaza uhuru wa habari.

Aliongeza kuwa ripoti hiyo imepitia jumla ya sheria nane (8) ambazo ni Sheria ya usajili wa wakala wa habari, magazeti na vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria no.8 ya 1997, Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar namba 7 ya mwaka 1997 iliyorekebishwa na sheria namba 1 ya mwaka 2010.

Nyengine ni sheria ya Adhabu ya Mwaka 2004 (Sheria Na. 6) iliyorekebishwa mwaka 2018, Sheria ya kufuta Sheria ya Uchaguzi Na. 11 ya mwaka 1984 na kutungwa kwa Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2017 na mambo mengine yanayohusiana na hayo pamoja na Sheria ya Baraza la Wawakilishi Na 4 ya mwaka 2007 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.

Alieleza kuwa Sheria ya Tume ya Utangazaji Na. 7 ya 1997 kama ilivyofanyiwa marekebisho na sheria Na. 1, 2010 inahitaji kufanyiwa marekebisho kifungu cha 27 (2) kutokana na kutoa mamlaka zaidi kwa viongozi.

"Sheria ya Tume ya Utangazaji No. 7 ya 1997 kama ilivyofanyiwa marekebisho na sheria No. 1, 2010 viongozi wamepewa mamlaka makubwa sana mfano kifungu cha 27 (2). Waziri amepewa mamlaka makubwa sana ya kuchukua maamuzi yoyote," alieleza mkufunzi huyo.

Alipendekeza sheria na sera kuwekewa vifungu vinavyoweka mazingira ya usalama wa waandishi wa habari ili kuwalinda dhidi ya uvunjifu wa uhuru wa kujieleza.

Alisema, "Sera na sheria lazima zihusishe vifungu vinavyohakikisha usalama wa waandishi wa habari, wanaharakati na wasomaji ili kuwaweka katika mazingira salama."                                    

Mratibu wa program ya kuendeleza mapitio ya uhuru wa Sheria za habari (ARFEL), Zaina Mzee, alisema ipo haja ya kufanyiwa marekebisho kwa sharia hizo hususan mama za habari ili kupata sheria rafiki na zenye muktadha mwema wa tasnia ya habari.

“Ipo sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar nambari 7 ya mwaka 1997, 1997 iliyorekebishwa na sheria namba 1 ya mwaka 2010, pamoja na sheria nambari 5 ya Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria no.8 ya 1997.

Alisema sheria hizo, zimekuwa na vifungu ambavyo sio rafiki kwa kuimarisha uhuru wa habari pamoja na uhuru wa kujieleza katika jamii.

Sambamba na hilo mratibu huyo aliongezea kuwa pamoja na ukongwe wake sheria hizo mbili kuu zinazosimamia vyombo vya habari, lakini kubwa zaidi zimekuwa zikiwabana waandishi katika kutekeleza haki yao ya  kikatiba.

‘’Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kwenye kifungu chake cha 18 kimeweka wazi suala la kupata, kusambaaza habari habari tena bila ya kujali mipaka ya nchi,’’anasema ilivyoeleza sehemu ya katiba.

Jabir Idrissa, ambaye ni mdau wa habari alisema, uwepo wa sheria zinazokwaza uhuru wa habari imepelekea Zanzibar kukosekana kwa vyombo vya habari binafsi kwa upande wa magazeti kutokana na urasimu katika utekelezaji wa sheria hizo.

"Mpaka leo Zanzibar hakuna Gazeti binafsi, ambapo kabla ya Mapinduzi kulikuwa na magazeti mengi Zanzibar, historia ya uandishi wa habari Zanzibar ni ya muda mrefu lakini imekufa kutokana na uwepo wa sheria zisizo rafiki," alieleza mdau huyo.

Nae Mratibu wa MCT-Zanzibar Shifaa Said amesema wakati umefika sasa kwa waandishi wahabari kutumia vyema kalamu zao kuikumbusha Serikali  namna gani sheria zilizopo zinavyoathiri uhuru wa kutoa na kupata habari nchini .

“Ni wakati sasa waandishi wa habari kutumia kalamu zenu kuonesha kwa namna ambavyo sheria zilizopo zinavyoathiri tasnia ya habari na zinahitaji kufanyiwa marekebisho kwa maslahi ya umma”, alisema Shifaa Said.

Mwandishi mwandamizi kutoka Zanzibar Salim Said Salim amesema ni Utamaduni wa watu wa Zanzibar ulianzia enzi za kale kupenda kupokea habari kupitia njia tofauti hivyo ni vyema kuendelezwa bila ya vikwazo kupitia sheria za habari.

“Wazanzibar walipenda kupata habari kama njia moja ya mawasiliano kupitia njia tofauti, tukiwa kwenye usafiri wa baharini (meli) kulikuwa na  vipaza sauti (mabomba) ambayo yanatowa taarifa za habari na abiria wakipata kujua kila kilichokuwa kinaendelea/ kinatokea kwa wakati huo,” Salim Said.

Mradi wa kuimarisha masuala ya uhuru wa habari ni wa miaka miwili wenye lengo la kuendeleza mapitio ya uhuru wa Sheria za habari (ARFEL), ambao unatekelezwa na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na Commonwealth Foundation.

Post a Comment

0 Comments