Na Mwandishi Wetu:
Jioni wa tarehe 26 Oktoba 2015,
hewani kupitia redio ya kijamii Swahiba
FM ya Zanzibar, kulisikika sauti ya Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama
cha Wananchi (CUF), akizungumza moja kwa moja na waandishi wa habari.
Katika mkutano huo uliopeperushwa
moja kwa moja, Maalim Seif alitangaza kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa
na mawakala wa chama chake kutoka vituo vya kupigia kura, alikuwa ameshinda
urais wa Zanzibar kwa asilimia 52.87,
dhidi ya Rais aliyekuwa madarakani kwa tiketi ya CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, aliyepata asilimia 47.13, katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, 2015.
Swahiba FM, ikiwa ni chombo cha
habari kilicho karibu na wananchi, ilikusudia kuwapatia taarifa mapema juu ya
kinachoendelea, kama sehemu ya wajibu wake wa kuhudumia umma.
Lakini ndani ya saa chache, hali
ilibadilika. Tume ya Utangazaji
Zanzibar (ZBC) iliamuru redio hiyo ifungwe mara moja, kwa madai ya "kurusha taarifa zisizothibitishwa
rasmi na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC)." Redio hiyo ilishtumiwa kwa
"kujitangazia matokeo," jambo lililoonekana kuwa kinyume cha sheria
za uchaguzi za wakati huo.
Tukio hili lilisababisha mjadala
mkubwa kitaifa na kimataifa kuhusu uhuru wa habari wakati wa chaguzi, mipaka ya
vyombo vya habari, na mazingira ya kisheria yanayowakabili wanahabari Zanzibar.
Mashirika ya haki za binadamu na
watetezi wa uhuru wa vyombo vya habari walihoji:
"Je,
ni sahihi kwa chombo cha habari kufungiwa kwa kurusha matamko ya mgombea? Je,
sheria zetu zinawalinda waandishi au zinawatisha?"
Kwa waandishi wa habari na
wachambuzi wengi, kufungiwa kwa Swahiba FM kilikuwa kielelezo cha wazi cha
udhaifu wa mfumo wa kisheria katika sekta ya habari.
Tukio hilo lilionyesha bayana hitaji
la dharura la sheria mpya ya habari sheria itakayolinda uhuru wa kujieleza,
kuimarisha uwajibikaji, na kulinda tasnia ya habari dhidi ya ukandamizaji wa
kisiasa.
Kutokana na mkasa huo na mengine
mingi kwa wanahabari na vyombo vya habari kuwa na hofu juu ya uhuru wao kwenye
tasnia hiyo zaidi ya miaka ishirini, wadau wa sekta ya habari visiwani Zanzibar
wamekuwa wakihimiza kupitishwa kwa sheria mpya ya habari.
Licha ya mazungumzo, semina, na
ahadi kutoka kwa viongozi wa serikali, bado hakuna utekelezaji wa dhati
uliofanyika. Ukosefu huu wa sheria umeendelea kuathiri kwa kiasi kikubwa
utendaji wa vyombo vya habari na namna taasisi za serikali zinavyowajibika kwa
umma.
Hofu ya kufanya kazi kwa waandishi wa habari inaweza
kusababibsha kutokuwepo kwa utawala bora kwama anavyoeleza Warda Khatibu Khamis, Katibu wa Jumuiya ya Kijana Amka Wajibika, "Kukosekana
kwa sheria bora ya habari kunachangia kwa kiasi kikubwa ukosefu wa uwajibikaji
kwa taasisi za serikali na vyombo vya habari vyenyewe."
Mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi wa
Habari Wanawaeke Tanzania upande wa Zanzibar Dklt. Mzuri Issa anasema Sheria
zilizopo hivi sasa zinatoa mamlaka makubwa kwa viongozi wa serikali kuingilia
uhuru wa vyombo vya habari.
"Kifungu
cha 30 cha Sheria ya Wakala wa Habari, Magazeti na Vijarida Na. 5 ya 1988
kinampa Waziri mamlaka ya kufungia gazeti kwa kigezo cha 'maslahi ya taifa'.
Mamlaka haya yanaweza kutumiwa vibaya kisiasa."
Jabir
Idrissa, mwandishi wa muda mrefu na mdau wa
habari, yeye anasema kuwa "Mpaka
leo Zanzibar hakuna gazeti binafsi. Kabla ya Mapinduzi kulikuwa na magazeti
mengi, lakini historia ya uandishi wa habari Zanzibar imekufa kutokana na
sheria zisizo rafiki."
Said
Suleiman Ali, mchambuzi wa sheria, anaangazia
Sheria ya Tume ya Utangazaji Na. 7 ya 1997, ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka
2010. Ananukuu:
“Kifungu
cha 27(2) kinasema: 'Waziri anaweza kusitisha au kuzuia utangazaji wa redio au
televisheni yoyote kwa sababu anazoziona kuwa ni kwa maslahi ya umma.”
Anaonya kuwa kifungu hicho kinampa
waziri mamlaka ya juu kupita kiasi, hali inayodhoofisha uhuru wa vyombo vya
habari.
Berema
Suleiman Nassor, Mwandishi wa habari kutoka Zenj Fm
Radio, anasema kuwa vyombo vya habari vingi haviandiki habari za kukosoa hasa za kiuchunguzi kwa hofu ya
kufungiwa.
"Hadhira
inahitaji habari zenye kusisimua lakini tuna hofu ya kuandika habari hizo kwani
ukiandika zinazogusa maslahi ya watu wenye mamlaka, biashara ya habari inakufa
hapo hapo." Anasema
Katiba ya
Zanzibar ya 1984, Kifungu cha 18 kinaeleza bayana
kuwa uhuru wa kutoa maoni, kutafuta, kupokea
na kusambaza habari ni haki ya kola mtu.
"Kila
mtu anayo haki na uhuru wa kutoa maoni, kutafuta, kupokea na kusambaza habari
na mawazo yake kupitia chombo chochote cha habari bila ya kujali mipaka ya
nchi." Kinafafanua kifungu hicho
Azimio la Kimataifa
la Haki za Binadamu (UDHR), Ibara ya
19: inaeleza "Kila mtu ana haki ya
kuwa na maoni na uhuru wa kujieleza; haki hii inajumuisha uhuru wa kushikilia
maoni bila kuingiliwa, kutafuta, kupokea na kusambaza habari na mawazo kwa njia
yoyote ile bila kujali mipaka."
Kwa upande
wa Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (ACHPR), Ibara ya 9 nao unafafanua vyema kwa kusema "Kila mtu ana haki ya kupokea taarifa.
Kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake ndani ya sheria."
0 Comments