Ticker

6/recent/ticker-posts

Ujumuishwaji Wa Watu Wenye Ulemavu Ndio Chachu Ya Kuwakomboa KiuchumiNa Asha Ahmed, Unguja.


Licha ya jitihada nyingi za serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kusimamia na kuyasaidia makundi maalum ikiwemo watoto, wanawake na watu wenye ulemavu, kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi, bado jamii imekua na uelewa mdogo kuhusiana na uwezo wa watu wenye ulemavu kujishughulisha na shughuli mbali mbali za kijamii kiuchumi na hata kisiasa.

Jamii kubwa ya kizanzibari inaamini kuwa watu wenye ulemavu ni watu wanaohitaji usaidizi tu, na hawana uwezo wa kufanya chochote, lakini ukweli ni kuwa watu hao wakiwezeshwa na kuwekewa miundombinu sawa wanaweza kujitegemea na kuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo endelevu ya taifa.

Katika kuwawezesha kuwainua kiuchumi watu wenye ulemavu, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA-ZNZ) kwa kushirikiana na Shirikisho la Jumuiya za Watu wenye Ulemavu (SHIJUWAZA) kwa mashirikiano makubwa na Shirika la Watu wenye Ulemavu la Norway (NAD) wanatekeleza mradi maalum unaojulikana kama KIJALUBA Isave Zanzibar.

Mradi wa KIJALUBA ni mradi jumuishi wa unaolenga kuwasaidia watu wenye ulemavu kujikomboa kiuchumi na kuweza kujitegemea wenyewe pamoja na kuendesha familia zao.

Kwa sasa mradi huo una jumla ya vikundi 43 ambapo vikundi 20 vipo  wilaya ya Kusini Unguja na wilaya ya chakechake Pemba kuna jumla ya vikundi 23.

Na tayari wanachama wa vikundi hivyo wameshapatiwa mafunzo tofauti yakiwemo ya uendeshaji vikundi, uchukuaji wa mikopo, uchaguzi wa biashara amabapo mafunzo yote hayo yanalenga kuwasaidia kutumia fedha wanazojiwekea katika vikundi ili kujikuza kiuchumi.

“Tumeshatoa mafunzo mbalimbali kwa Unguja na Pemba, na sasa tuko katika mafunzo ya uchaguzi wa biashara ambayo yatawaelekeza jinsi ya kuchagua biashara ambazo zitakuwa na faida na hivyo waanze kuchukua biashara na kuanza kufanya biashara”, Nairat Abdulla, afisa mkuu mradi wa Kijaluba.

Nairat alisema kuwa kundi la watu wenye ulemavu mara nyingi huwa linawachwa nyuma na kusabbaisha kukosa fursa mbalimbali za maendeleo, hivyo mradi huu utawawezesha kujikwamua lakini pia kuwaongezea hadhi yao katika jamii.

Mohammed Ali ni mmoja wa walimu wa vikundi ndani ya jamii alisema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia wanavikundi hao kukuza ujuzi wa masuala ya biashara na hivyo kuweza kujiajiri kupitia biashara watakazozichagua na kuzianzisha.

“Elimu hii wataenda kuwafundisha wenzao, ili  kuona wanachama wote wanapata taaluma hiyo ambayo itawasaidia kufanya biashara zao kwa ufanisi”, alisema.

Nae mmoja wa wanachama wa vikundi vya Kijaluba Othman Simba amesema kuwa awali hawakuwa na uelewa kuhusu uchaguzi wala mipango ya biashara, hivyo kupitia mafunzo hayo wamejifunza mbinu bora na ujuzi wa kuanzisha biashara mbalimbali ili kujiongezea kipato chao.

“Awali tulikua tunafanya biashara ndogondogo lakini hatukua khasa na ujuzi wa uendeshaji wa biashara zetu, hali ambayo imesababisha kukosa faida nzuri katika biashara zetu”, alisema.

Mkufunzi wa mafunzo hayo ambae ndie afisa msimamizi wa wilaya Muhidini Ramadhan aliwasisitiza wanachama hao suala la kujiwekea malengo ya biashara ikiwemo kujua mitaji, faida na hasara zinazoweza kujitokeza katika uendeshaji wa biashara zao.

Aliongeza kuwa biashara nyingi zinakufa na zinashindwa kuendelea kwa kukosa mipango madhubuti ya kuendesha biashara zao.

Utafiti uliofanyika kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi wa Kijaluba ulionesha kuwa watru wenye ulemavu wanaishi katika mazingira magumu na hawana ajira rasmi wala biashara za kuwasaidia kuendesha maisha yao.

Mradi huu mbali ya kuwainua kiuchumi watu wenye ulemavu, una lengo pia la kuweka ujumuishi kwa kuwachanganya watu wenye ulemavu na wasio na ulemavu ili waweze kufanya shughuli zao kwa pamoja ili kuondokana na kuwatenga watu wenye na kukodoesha masuala ya watu wenye ulemavu katika kila Nyanja mbalimbali. 


Post a Comment

0 Comments