NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, JInsia Wazee na Watoto Anna Athanas amesema mashindano ya klabu bingwa Tanzania ‘ligi ya Muungano’ yana umuhimu mkubwa katika kujenga umoja wa kihistoria baina ya nchi mbili za muungano.
Akizungumza katika ufungaji wa ligi kuu ya muungano ya mchezo wa netiboli uliowakutanisha KVZ na Jeshi Star, mwishoni mwa wiki iliyopita, katika uwanja, wa Jimkana Unguja, Athanas alisema, kupitia mashindano hayo wanapata nafasi ya kubuni mikakati mbali mbali ya kudumisha muungano wao na kuongeza upendo na mshikamano mwa wanamichezo wa pande hizo.
Aidha alisema mashindano hayo pia timu zao zinapata nafasi ya kujipima uwezo wa kiwango cha uchezaji wa timu zao na baada ya mashindano timu hizo hukaa na kutathmini na hatimae kupanga mikakati mbali mbali ili ziweze kufanya vizuri zaidi katika mashindano yanayofuta.
“Mashindano haya yanaweza kupima uwezo wa makocha, wachezaji na waamuzi tulionao, hivyo pamoja na changamoto na ukata tulionao nashauri ni vyema yakaendelezwa ili kupata faida nilizoziainisha”, alisema Naibu Waziri.
Sambamba na hayo alisema kuwa serikali inaelewa kuwa sekta ya michezo hasa netiboli inakabiliwa na changamoto ya udhamini pamoja na viwanja, hasa michezo ya ndani, lakini viongozi ambao mmepewa dhamana ya kusimamia msichoke kuisaidia serikali katika kuhakikisha kuwa vyama vya michezo havifi.
Aidha alisema serikali itajitahidi kujenga viwanjwa vya kisasa pamoja na viwanja vyenye viwango vya kimataifa , ili kuwapa hamasa wadhamini kuja kushirikiana na serikali katika kuinua michezo .
Hata hivyo alisema kuwa serikali itahakikisha inazifanyia kazi changamoto zilizopo ili kuweza kuwa na ushiriki mzuri wa michezo kuanzia ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa.
Mapema Katibu Mkuu wa Chama cha Netiboli Zanzibar CHANEZA Said Ali Mansab na Naibu Katibu Mkuu wa mchezo huo Tanzania CHANETA Hilda Aunsi waliiomba serikali kuwasaidia kuwapatia wadhamini ili kuweza kufanikisha vyema katika mashindano yao wanayoayaandaa.
Katika mashindano hayo timu ya TAMISEMI ilitwaa ubingwa na kuwa mara ya pili mfululizo huku timu ya KVZ ikichukuwa nafasi ya pili.
0 Comments