Nafda Hindi, Zanzibar:
Vifaa vya kupimia maambukizi ya virusi vya ukimwi (HIV KITS) vyarejea Zanzibar baada ya kukosekana kwa takriban miezi mitatu katika Vituo vya Afya vya Serikali.
Hayo
yamebainika baada ya Chama cha Waandishi wa habari Wanawake TAMWA ZNZ kufanya ziara ya kutembelea
Vituo vya Afya vilivyopo Wilaya ya Kati na Magharibi “B” Unguja na kugundua
tatizo hilo kwa sasa limeshatatuliwa.
TAMWA ZNZ pamoja na waandishi wahabari walifika
katika kituo cha Afya Mwera na kujionea hali halisi ya uwepo wa vifaa hivyo
jambo linalotowa hamasa kwa vijana kurudi katika vituo hivyo na kupima Afya zao bila ya usumbufu wowote.
Akizungumza
na waandishi wahabari Afisa Ustawi wa jamii na mtoa huduma rafiki kwa vijana
Kituo cha Afya Mwera Fatma Yussuf amesema baada ya kurudi kwa vifaa vifaa hivyo
vijana wamehamasika kujitokeza kwa wingi kwa lengo la kupima Afya zao.
Amesema
katika kituo hicho kwa siku wanapokea vijana wanane ambao wanafika kupima Afya
zao hali ambayo inatowa matumaini kwa vijana kuishi kwa Amani kutokana na uwepo
wa maradhi ya kuambukiza ambayo
husababisha kupoteza nguvu kazi ya Taifa hususan vijana.
“Vifaa
tulivyoletewa vinaweza kutusogeza miezi mitatu, ila tunaomba tupatiwe vyengine
kabla ya kumalizika vilivyopo ili tatizo hilo lisijitokeze tena,” Fatma Yussuf,
alisema.
Nae
Muelimishaji rika kwa vijana Kituo cha Afya Mwera Mwajuma Khatib amesema kurejea kwa vifaa hivyo kunachangia
ongezeko la vijana kujitokeza kwa wingi katika kituo hicho wakiamini ni mahali
sahihi na kufurahishwa na utunzaji siri wa kituo kwa vijana ambao wamefika.
“Vijana
wameelimika toka tupokee hizi kits wanaambiana kwamba mambo yetu tayari na
wanajitokeza kwa wingi kwa sababu wanasema wana Amani na siri pia wako huru kwa
lolote wanalouliza ukilinganisha na vituo vyengine vya binafsi,” Mwajuma Khatib
alisema.
Nao vijana
waliofika katika kituo hicho wamesema wanafurahia kurudi kwa huduma hiyo na
watatumia fursa ya kupima Afya zao ili kujikinga na maradhi mbali mbali.
“ Mimi nina
miaka 21, bado ni kijana nataka kuoa ndio maana napima Afya yangu mara kwa mara
kuhakikisha niko salama , mimi situmii kinga kwa sababu ukitumia kinga haina
ladha mwenzangu yeye hataki kutumia kinga ,” alisema Mohammed mkaazi wa Mwera.
Afisa Mradi
wa Afya ya Uzazi kwa wasichana na wanawake Zaina Abdalla Mzee amesema wamefarajika kuona
vifaa vya kupimia virusi vya ukimwi kurejea katika vituo vya Afya vya Serikali baada
ya ziara iliofanywa na TAMWA ZNZ na kugundua kuadimika kwa vifaa hivyo na
waandishi wahabari kutekeleza jukumu lao la
kuandika habari juu ya suala
hilo.
“Kama
tunavyojuwa kuwepo kwa vifaa hivyo ni muhimu kwa vijana na wananchi kwa jumla,
hivyo tunaiomba Serikali kuwa na utaratibu maalum na wa uhakika kwa vifaa hivyo
kwa sababu kukosekana kwake kunawasababisha vijana kukosa nafasi muhimu ya kupima afya zao.
Mradi wa kuendeleza
utetezi wa haki ya elimu ya Afya ya uzazi kwa vyombo vya habari kwa wasichana
na wanawake unaotekelezwa na TAMWA ZNZ ulitowa mafunzo kwa waandishi wa
habari 71 na wahariri 23 kwa Unguja na Pemba ambapo ulioanza Octobet 2022 na
kumalizika October 2023 ulitekelezwa kwa Wilaya ya Magharibi "B" na
Kati kwa Unguja na Wilaya ya Chake Chake kwa Pemba.
0 Comments