Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi amehimiza
ushirikiano wa kiutendaji baina ya taasisi za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano
wa Tanzania (SMT) na za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ili kuendeleza
mageuzi ya uchumi na uwekezaji.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo
Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na
Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo na ujumbe wake wa watu 20 waliofika
kujitambulisha.
Alisema, SMZ na SMT wana
ushirikiano mkubwa kwenye utendaji wa taasisi zao na kueleza, mara kadhaa
taasisi ya hazina ya Zanzibar imekua ikipata ushirikiano mzuri na ya Jamuhuri
ya Muungano wa Tanzania pia Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar, ZIPA na TIC pamoja
na taasisi nyengine za pande mbili hizo za Muungano hushirikiana katika
kuboresha maendeleo kwa ustawi wa uchumi wa taifa la Tanzania na watu wake.
Rais Dk. Mwinyi pia alitumia
fursa hiyo, kuwapongeza na kuushukuru ujumbe huo kwa utayari wao kwa kuendelea
kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mawazo ya mageuzi
yanayolenga kujenga uchumi wa wananchi wa pande zote mbili za Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania kupitia ushirikiano uliopo baina ya tasisi za serikali
mbili hizo, zikiwemo Mamlaka ya Bandari, Ofisi ya Msajili Hazina, Mamlaka za
Uwekezaji pamoja na Tume ya Mipango ya Taifa.
“Niwapongeze
kwa mawazo haya ya mageuzi, ni vizuri mara zote tuwe kunafikiria kujenga uchumi
wetu kupitia taasisi zetu” alipongeza Rais Dk. Mwinyi.
Akiizungumzia bandari Jumuishi
ya Mangapwaji Rais Dk. Mwinyi, alimueleza Waziri huyo kwamba SMZ imepania
kuleta mageuzi makubwa ya uchumi kupitia bandari hiyo, ambayo kutokana na
maumbile ya kisiwa cha Zanzibar kilivyo, inakusudiwa kujumuisha shughuli zote
za badari mbali na kupakia na kushushia abiria na mizigo lakini kuruhusu meli
mbalimbali za kimataifa zitakazoleta mageuzi makubwa ya biashara, uwekezaji na
kuimarisha uchumi wa buluu.
Naye, Waziri Mkumbo alimuahidi
Rais Dk. Mwinyi ushirikiano wa hali ya juu katika kuujenga uchumi wa nchi hasa
kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya
Zanzibar wamejipanga kuleta mabadiliko makubwa ya uchumi.
Alisema, mbali na mambo
mengine lakini kupitia mradi wa Bagamoyo, ujio wa Zanzibar umewaletea tija na
ufanisi mkubwa kwenye utendaji wao hasa kwa taasisi wanazoshirikiana nazo
kiutendaji kwani watajifunza mengi kupitia bandari jumishi ya Mangapwani pamoja
na taasisi nyengine wanazoshirikiana nazo kiutendaji.
Ujumbe ulioongozana na Waziri
Prof. Kitila umemjumuisha Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji
Dk. Tausi Kida, Msajili wa Hazina Bara, Nehemia Mchechu, Katibu wa Tume ya
Mipango Lawrence Mafuru, Mkurugenzi Mkuu EPZA Charles Itembe, Mkurugenzi Mkuu
TIC Gilead Teri na Mkurugenzi wa Miundombinu TPA Dk. Hussein
Lufunyo.
IDARA
YA MAWASILIANO IKULU, ZANZIBAR
0 Comments