Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Raymond
Mndolwa amewataka wakulima wa Skimu ya Mahenge Wilayani Korogwe kulinda vifaa
vya ujenzi vitakavyotumika wakati wa Ujenzi na ukarabati wa Skimu hiyo ili
kupata mradi wenye ubora na viwango stahiki.
Akizungumza wakati wa hafla ya kumkabidhi eneo la
mradi mkandarasi Gilco Construction Company ltd, Bw. Mndolwa amefafanua juu ya
madhara yanayoweza kujitokeza na kuathiri mradi endapo hatua za pamoja za
kidhibiti ulinzi wa malighafi hazitazingatiwa.
" Mkiiba simenti mkandarasi hatanunua simenti
nyingine badala yake atapunguza kiwango Cha simenti wakati wa Ujenzi na matokeo
yake mradi hautakuwa na ubora wa kiwango kilichokisudiwa na mvua ya masika
ikija itausomba mradi wote." Alisema
Aidha Mndolwa amewaasa wanaanchi wa Korogwe kuwa
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeanza zoezi la Usanifu katika Bonde la mkomazi
Kwa gharama ya Tsh. Bilioni 22, Kwa Lengo la kujenga Bwawa na skimu za
Umwagiliaji na kwamba zoezi la ujenzi wa Skimu litakapomalizika wenye mashamba
makubwa watapunguziwa ili wananchi wengine wasio na mashamba wapewe.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Korogwe mjini,
Jokate Mwegelo amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kuchangamkia fursa ya Kilimo
cha Umwagiliaji ili kuinua maisha na pato la mtu mmojammoja na taifa kwa
ujumla, huku akiwasisitiza waache tabia ya kuuza ama kukodisha mashamba yao.
Hata hivyo mkurugenzi wa halmashauri ya Korogwe mji
Bw. Tito Mganwa amewaagiza wataalam wa Ofisi yake kushirikiana Kwa karibu na
wataalam wa Tume wakati wa ujenzi na ukarabati wa Skimu hiyo ili kupata matokeo
chanya Kwa manufaa ya wananchi wa Korogwe na Mkoa wa Tanga Kwa ujumla. Baadhi
ya wakulima wa skimu ya Mahenge wameishukuru serikali kupitia Tume ya Taifa ya
Umwagiliaji NIRC kwa kutenga zaidi bilioni 1.85 kwa ajili ya ukarabati
miundombinu ya umwagiliaji katika skimu hiyo.
0 Comments