Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ Dkt,Mzuri Issa akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Chama hicho Tunguu Wilaya ya kati Unguja kuhusu baadhi ya sheria zinazokinza uhuru wa habari Zanzibar. |
Waandishi wa habari wa vyombo tofauti kutoka Unguja na Pemba wakipasha viungo kabla ya kuendelea na mkutano huo kwa awamu ya pili. |
Mwandishi wa habari mwandamizi Salim Said akitoa ufafanuzi kuhusu changamoto za sheria ya habari Zanzibar zinavyowapa wakati mgumu wanahabari katika utendaji kazi wao. |
Chama cha waandishi wa habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) kimesema kuna haja ya taasisi husika za mabadiliko ya sheria kuweka kipaumbele kufanyiwa marekebisho yanayoendana na matakwa ya wadau katika sheria za habari Zanzibar ili zitoe mazingira ya uwepo wa uhuru wa vyombo vya habari katika kutekeleza majukumu yao.
Alisema uhuru wa habari ni nguzo muhimu inayoweza kusaidia kwa kiasi kikubwa ukuzaji wa maendeleo kwenye Nchi hivyo inapotokea sheria ya tasnia hiyo kubana ni sawa na kuchelewesha maendeleo ambayo yanahitajika na kila mtu.
Alieleza, “lazima
tufahamu kwamba uhuru wa habari kwenye Nchi yoyote ni nguzo muhimu inayoweza
kusaidia maendeleo na ndio maana enzi za
uhai wake Nelson Mandela alipigania uhuru wa habari katika muda wake wote
hususani vyombo binafsi (Private media).’’
“Tuna kila sababu ya kuona kwamba Sheria zetu, Sera na matendo yaendane na mikataba ya kimataifa kuhusu uhuru wa habari ili iweze kuleta maslahi kwa makundi yote,” alieleza Dkt. Mzuri Issa.
Aliongeza “tumepitia sheria kumi za habari na katika kufanya mapitio hayo tunasukumwa zaidi na mambo matatu. kama Zanzibar na Tanzania tunapaswa kwendana na mikataba ya kimataifa.”
Sambamba na hayo Mkurugenzi huyo akifafanua zaidi alionesha kusikitishwa kwake na mamlaka mengine ya sheria ambayo inampa uwezo waziri wa habari kufungia chombo chochote cha habari iwapo ataona inakwenda kinyume na matakwa yake.
Alieleza kuwa hatua ya kufungia chombo ni jambo kubwa amabalo lisingepaswa kufanywa na waziri badala yake lilipaswa kufanywa na mamlaka nyingine ikiwemo Mahkama.
Mapema akiwasilisha ripoti ya mapitio ya sharia za habari, Shifaa Said alisema licha ya juhudi kubwa kuchukuliwa na wadau wa habari kutoa mapendekezo ya mabadiliko ya sheria mbalimbali lakini bado utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua.
“Sisi kama wadau tumeshatoa mapendekezo yetu ya kuhitaji mabadiliko ya sheria mbalimbali za habari ikiwemo Sheria ya tume ya utangazaji ya Zanzibar namba 7 ya mwaka 1997 na tunaendelea kufanya ushawishi ili tuweze kupata sharia bora zitakazotoa nafasi kwa wandishi na vyombo vya habari kutekeleza majukumu yake kwa uhuru,” ’Shifaa Said Hassan, mdau wa habari.
Hivyo aliwataka
wandishi wa habari kuendelea kufanya ushawishi wa mabadiliko ya sharia kwa
kuandika mapungufu yaliyopo katika sharia hizo ili ziweze kufanyiwa marekebisho
kwa haraka.
Alieleza, “sisi wandishi wa habari tuipigie chapuo sheria za habari zilizofanyiwa mapitio ambazo zinakinza uhuru wa vyombo vya habari na waandishi wa habari kwa kufanya ushawishi kupitia vyombo vya habari ili hizi sheria ambazo tunahisi zinatatiza uhuru wa habaroi ziweze kufanyiwa marekebisho.”
Akichangia ripoti hiyo mwandishi wa habari mwandamizi Zanzibar, Jabiri Idrissa alisema waandishi wa habari Zanzibar wanakabiliwa na mazingira magumu ya kufanya kazi iwapo siku sheria zilizopo zitafanyiwa kazi ipasavyo.
Akitolea mfano kupitia Sheria ya Kinga na Madaraka ya Baraza la Wawakilishi no. 4 ya 2017, Spika anaweza kumuita raia yoyote wa Zanzibar kuhojiwa kwenye kamati za Baraza hilo iwapo ataona amefanya kosa ambalo limekinzana na sheria za Baraza, huku sheria hiyo ikimzuia alieitwa kwenda na wakili wake wakati wa kuhojiwa. Tunaona kuwa kufanya hivyo ni kumyima haki muhimu ya mtu kujitetea pamoja na kuwa jambo la kuitwa na kuhojiwa lilipaswa kufanywa na Mahkama na sio taasisi nyengine yoyote ile.
Nae Khadija Rashid kutoka Redio Jamii Mkoani Pemba alisema kuna haja ya kuongezwa uhamaishaji zaidi kwa wanahabri juu ya ushawishi wa mabadiliko ya sharia hizo ili kuweka mazingira salama kwa tasnia hiyo.
Alisema, “kinachosikitisha zaidi ni kuona idadi kubwa ya wananchi hawajui sheria zinazowahusu wao wenyewe na kuongezea kuna haja kazi kubwa zaidi kuendelea kufanyika.
Nae Rerema Sleiman Nassor alisema wakati wa uchaguzi wanahabari wengi hukutana na mazingira mgumu licha ya kufanya kazi zao kwa misingi yote ya sheria za tume.
Alisema, “mazingira niliokutana nayo sitaweza kusahau maisha yangu yote nilitolewa kituo cha kupigia kura kama sikua na kazi maalumu ya kukusanya habari kwa maslahi ya umma’’alisema.
Mkutano huu wa
kuwasilisha ripoti ya sheria za habari Zanzibar unakuja kufuatia kufanyika kwa
mapitio ya sheria mbalimbali za habari ambayo yamefanywa na TAMWA ZNZ kwa
kushirikiana na Shirika la INTERNEWS Tanzania pamoja na wadau wengine wa habari
Tanzania.
0 Comments