Ticker

6/recent/ticker-posts

Utekelezaji mradi wa Viungo Z’bar unasaidia kwa kiasi kikubwa adhma ya Serikali kuongeza idadi ya ajira kwa wananchi wake-Waziri Shamata


Meneja mkuu utekelezaji mradi wa Viungo Amina Ussi Khamis akitoa maelezo mafupi juu ya utekelezaji mradi huo.

Baadhi wa viongozi wa vikundi vya kuweka na kukopa wakimskiliza kwa umakini  waziri wa kilimo,uvuvi mifugo na mali asili Shamata Shaame Khamis (hayupo pichani)



Waziri wa kilimo mali asili,umwagiliaji na mifugo Shamata Shaame Khamis akisisitiza jambo wakati alipokua akizungumza na viongozi wa vikundi vya kuweka na kukopa.
Waziri wa kilimo mali asili, umwagiliaji na mifugo Shamata Shaame Khamis (katikati) akiwaongoza wanufaika wa baiskeli hizo kuzijaribu mara baada ya kukabidhiwa kwao.

Waziri wa kilimo mali asili,umwagiliaji na mifugo Shamata Shaame Khamis akimkabidhi Baiskeli mmoja miongoni mwa viongozi wa kuweka na kukopa Halima Makame kutoka shehia ya kidoti mkoa wa kaskazini Unguja.




Na Muhammed Khamis 

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema uwepo wautekelezaji mradi wa viungo unaoendelea visiwani hapa unasaidia kwa kiasi kikubwa adhma ya Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi wake Unguja na Pemba.

Kauli hiyo imetolewa Waziri wa kilimo,umwagiliaji  mali asili na mifugo Shamata Shaame Khamis  wakati alipokua akikabidhi Baiskeli 30 mpya (brand new) aina ya sehewa zenye thamani ya shilingi milioni saba na laki tano, pamoja na visanduku maalumu vya kuweka na kukopa 80 vyenye thamani ya shilingi milioni nane katika hafla iliofanyika viwanja vya wizara hiyo Maruhubi mjini Unguja.

Alisema  moja ya adhma ya Serikali kwa wananchi wake ni kutoa ajira laki tano hivyo kupitia utekelezaji mradi huo umesaidia kupunguza kundi kubwa la vijana ambao wanaendelea kusaidiwa na hatimae kujiajiri wenyewe kupitia sekta ya kilimo.

Akitolea mfano miongoni mwa nafasi za ajira zilizotengenezwa na mradi huo ni pamoja na ujenzi wa soko jipya la Viungo (spice)  linaloweza pia kuhifadhi mboga mboga bila kuharibika lililopo Darajani mjini Unguja kuwa ni kielelezo tosha kuwa mradi huo umekwenda kuwakomboa wengi na kuisaidia Serikali katika kuleta maendeleo.

Sambamba na hayo Waziri Shamata aliwataka wasimamizi wa vikundi vya kuweka na kukopa waliopatiwa mafunzo maalumu katika utekelezaji mradi  kuhakikisha wanazitumia vyema baiskeli hizo vijijini mwao na hatimae waweze kuongeza chachu ya maendeleo na kuwa sababu ya kuleta mabadiliko.

Awali akitolea ufafanuzi  utekelezaji mradi huo Meneja mkuu Amina Ussi Khamis alisema mradi huo unatekelezwa na Jumuia isiyo ya kiserikeli Peoples Development Forum (PDF)wenye lengo la kuboresha uzalishaji wa kilimo cha mbogamboga, matunda na viungo chini ya udhamini wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (European Union).

Mradi huo unaojulikana kwa jina la VIUNGO kwa jina halisi ni “Value web horticulture and income growth project” ni mradi wa miaka minne kuanzia mwaka June 2020 Hadi Juni 2024 unaotekelezwa katika visiwa vya Unguja na Pemba na Jumuiya ya PDF wakishirikiana na Chama cha waandishi wa habari wanawake Zanzibar (TAMWA-ZNZ) na Community Forest Pemba (CFP).

Alisema mradi umepanga kufikia walengwa 57974 na unatekelezwa katika Wilaya 9 ambazo 5 Unguja (Kaskazini A, Kaskazini B, Wilaya ya Kati, Magharib A na Kusini) na 4 Pemba (Wete, Micheweni, Chakechake na Mkoani) katkika Wilaya hizo hadi sasa mradi umeweza kufikia Shehia 60 ambazo 30 kutoka Unguja na 30 kutoka Pemba.

Alisema lengo kuu la mradi ni kufungua fursa katika mnyororo wa thamani wa bidhaa za matunda, mboga na viungo ili kuweza kuongeza uhakika wa chakula na kipato cha wakulima wadogo wadogo wanaojishughulisha na kilimo cha mboga mboga, matunda na viungo, uzalishaji wa bidhaa zenye viwango bora na utanuzi wa masoko, pamoja na kukuza uchumi wa kilimo ndani ya visiwa vya Zanzibar kiujumla.

Alieleza katika kufanikisha malengo yake, mradi pia uliweka mikakati ya kuwajengea  uwezo na kuvisaidia vikundi 200 Unguja na Pemba ambavyo vinajihusisha na ujasiriamali mbalimbali vinavyojulikana kama (Village Savings and Loans Associations) yaani vikundi vya kuweka na kukopa katika jamii, mradi umekuwa ukisaidiana na wasimamizi wa vikundi hivi vya uwekezaji katika ngazi ya Wilaya (Community Representative Person- CRP) katika kazi zao.

Alisema awali  mradi ulifanya upembuzi yakinifu kufahamu kazi zinazofanywa na vikundi hivyo, maendeleo wanayoyapata, changamoto zinazokabili vikundi hivyo, sambamba na misaada ya kifedha au taaluma ambayo wanapata kutoka katika taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali.

Utafiti ulionyesha kwamba kati ya vikundi 200 vilivopitiwa asilimia 75 ya vikundi hivyo ni wanawake, na wenye umri kati ya miaka 25-36, hii inaonyesha dhahiri kuwa wanawake hao pia ni vijana na wenye nguvu katika kuleta maendeleo katika Taifa letu.

Aidha meneja huyo alisema  asilimia 60 ya kazi za vikundi hivyo ni kazi za kilimo, zikifuatiwa na ufugaji pamoja na kazi za ushoni,hii inaonyesha kwamba vikundi hivyo vinauwezo mkubwa wa kuongeza mikakati ya kilimo pindi vikiwezeshwa.

Akizungumzia kuhusu chamngamoto zilizoonekana kuvikabili vikundi hivyo ni ukosefu wa elimu juu ya taaluma za uongozi, ukosefu wa taaluma za kifedha na mipango endelevu ya biashara, pamoja na ukosefu wa misaada ya rasilimali fedha kwa kuendesha vikundi hivyo.

Akiendelea kufafanua zaidi alisema kupitia utekelezaji mradi huo wamefanya jitihada mbali mbali na hadi sasa na wamejaribu kusaidia katika kutatua changamoto hizo ikiwemo kuvifikia vikundi 114 Unguja na Pemba, na kupatiwa elimu  elimu na taaluma za usimamishaji wa vikundi hivyo, ikiwemo na mafunzo ya uongozi bora,usimamizi bora wa biashara na kifedha, pamoja na mbinu za ujasiriamali katika dhana ya kilimo.

Alisema vikundi 32 vimeshaunganishwa na taasisi za kifedha ikiwemo NMB Bank pamoja na Boresha Maisha Saccoss,vikundi 61 tayari wamepatiwa visanduku vya hisa kwa ajili ya kuhifadhia fedha zao.

Sambamba na hayo alisema mradi huo unampango wa kusaidia vikundi hivi vya kuweka na kukopa kwa kuwapatia ruzuku za kuwasaidia kujiekeza katika miradi endelevu na yenye manufaa katika jamii zao na Nchi kiujumla. Mkakati huu bado upo katika maandalizi na utawekwa wazi katika vyombo vya habari pindi taratibu zake zitakapokamilika.  

Post a Comment

0 Comments