Na Ahmed Abdulla
DEMOKRASIA ni neno lenye uwanja mapana, lakini
ikitekelezwa katika jamii ama katika nchi huwa kuna faida kubwa hasa
ikizingatiwa kuwa hoja za wengi ndizo zinazofuatwa na kutekelezwa.
Hata hivyo, kwenye jamii yenye kuzingatia demokrasia ya
kweli wachache kwa uchache wao nao husikilizwa hoja zaa na sio kupuuzwa na
inapotokea hoja za wachache zina mantiki sio dhambi kutekelezwa.
Wataalamu wengi wanakubaliana kuwa uwepo wa vyombo vya
habari vya aina mbalimbali una mchango mkubwa kwenye ujenzi wa demokrasia na
pia suala la kupata habari linahesabiwa kama miongoni mwa haki muhimu za
binaadamu.
Ili vyombo vya habari vitekeleze vyema jukumu la kujenga
demokrasia katika nchi, lazima viwe huru katika kutekeleza majukumu yake
pasiwepo na taasisi ama mtu ambaye kwa nguvu zake ama utashi wake atakuwa
anaamrisha habari ipi itoke na ipi isitoke, pengine tu kwa maslahi yake sio
maslahi ya jamii.
Uhuru huo wa vyombo vya habari katika nchi, lazima
uambatane na uwepo wa sera, sheria na kanuni rafiki za habari zinazowawezesha
wanahabari kutekeleza majukumu yao na sio kuwabana na lakini pasi na waandishi
hao kuvunja sheria nyengine.
Kwa muda mrefu Zanzibar imekuwa na kilio cha kuwa na
sheria mbovu za habari, ambapo msingi wa ubovu wa sheria hizo unatokana na kuwa
ni za muda mrefu, kwa maana ya kwamba zimezeeka, zimechoka na kuchakaa.
Tunaposema sheria hizi zimekongweka maana yetu ni kwamba
zimeshindwa kabisa kwenda na wakati, hasa kutokana na mabadiliko yanayotokea
mara kwa mara kwenye tasnia ya habari yanayotokana na kukua kwa teknolojia.
Sheria nyingi za habari zilizopo Zanzibar ikiwemo ya
magazeti na zinawapa nguvu viongozi ambazo hawastahiki kuwa nazo katika
ulimwengu wa sasa wa demokrasia.
Kwa mfano sheria ya magazeti ya mwaka 1988, kifungu cha
30 (i) kinasema; “Endapo waziri anaona kuwa ni kwa manufaa ya umma au kwa
maslahi ya amani na utulivu, anaweza kuamuru kufungiwa kwa gazeti... na gazeti
hilo litakoma kuchapishwa kuanzia tarehe iliyotajwa.
Kwanini pasiwepo na bodi huru itakayoundwa na wataalamu
kutoka serikalini, taasisi na mashirika binafsi ya habari yakachambua kuwa gazeti
hilo limefanya kosa kadhaa na dhabu yake kadhaa.
Msingi wa kusema hivyo ni kwamba uwaziri ni wadhifa wa
kisiasa kwa maana ya kwamba wakati mwengine anaweza asiwe mtaalamu wa habari
lakini kapewa nafasi hii atakuwa na uwezo kiasi gani kitaalamu kubaini kosa la
gazeti?
Mfano mwengine kifungu cha 48 cha sheria ya magazeti,
kinaeleza makosa ikiwa ni pamoja na uchochezi na kashfa kwa mtu yeyote ambaye
anachapisha, kuchapisha, kuuza, kusambaza au kutoa chapisho lolote la uchochezi
na baada ya kukutwa na hatia mtu huyo faini au kifungo au vyote viwili faini na
kifungo vitatolewa na uchapishaji huo utatolewa.
Hichi ni miongoni mwa kifungu ambacho sio tu kinapunguza
uhuru wa vyombo vya habari, lakini pia kinahatarisha uhuru wa kujieleza kwa
jumla, vifungu kama hivi vipo kwenye katiba na baadhi ya sheria za habari.
Serikali ya awamu ya nane imejipambanua kwenye ukuzaji
demokrasia ndio maana iko tayari kuzirekebisha sheria zote zenye utata, hivyo
sheria za bahari nazo umefika wakati kupitiwa tena upya.
Wadau wa habari wameshajadili sana na mapendezo yapo,
serikali ione umuhimu wa kurekebisha sheria ili vyombo vyetu vya habari vikuze
demokrasia nchini
0 Comments