Na Ahmed Abdulla Othman
Wazazi na walezi visiwani Zanzibar wametakiwa kutokata
tamaa na kupambana iwapo watoto wao watakutwa na kadhia ya kudhalilsihwa
ikiwemo kubakwa au kulawitiwa.
Wito huo umetolewa na miongoni mwa mzazi ambae jina lake
nilanhifadhiwa kufuatia kadhia ya mtoto wake kubakwa na kukashifiwa na mtu
aliedai alikua karibu nao.
Alisema kwa kuwa mtu aliembaka mtoto wake alikua mtu wa
karibu walimrubuni mume wake na alikua
tayari kufuta kesi hio baada ya kupewa shilingi milioni nne.
Alisema watu hao bila ya hofu walimshawishi mume wake na
kumpa fedha ili kesi hio waiondoe kituo cha polisi lakini yeye binafsi alikataa
kufanya hivyo na kuendelea kupambana.
Alieleza kuwa
watu hao walimpa mume wake shilingi milioni nne lakini yeye alikataa kuchukua
pesa hio na kupelekea kutofautiana na mume wake lakini hakujali kwani aliamini
anapambania utu wa mtoto wake na si jembo jengine lolote lile.
Akiendelea kusimulia zaidi mama huyo huku machozi
yakimtoka alisema ni jitihada zake binafsi na ushauri aliokua akipata kutoka
kwa maafisa wa TAMWA-ZNZ kila wakati ndio faraja pekee iliomfanya kutokata
tamaa.
Sambamba na hayo alieleza kutokana na kufuatilia kesi
hio bila kuchoka hatimae Mahakama ilimtia hatiani aliemfanyia unyama huo mtoto
wake na kumuadhibu kwenda chuo cha mafunzo kwa miaka 30.
Mama huyo anaamini kuwa hayo yote yametokana na jitihada
binafsi ambazo wazazi wengine wanapaswa kuwa nazo na sio kukata tamaa wakiamini
kuwa hakuna hukumu itakayotolewa.
0 Comments