Wanawake wawili pamoja na watoto
wakiwa migongoni mwao wa Kijiji cha Tululu, Kata ya Kaoze, Bonde la Ziwa Rukwa
Wilayani Sumbawanga wanasadikiwa kuzama katika mto momba na kufariki baada ya
mtumbwi waliokuwa wamepanda kushindwa kuhimili kasi ya maji ya mto huo na kusababisha
kupinduka kwa mtumbwi huo.
Kinamama hao ambao walikuwa wakitoka
ng’ambo ya mto huo unaotenganisha Mikoa ya Rukwa na Songwe kufuata huduma
mbalimbali zikiwemo za afya walipatwa na kadhia hiyo wakiwa Pamoja na wananchi
wengine watatu ambao walipona baada ya kupata msaada wa kuokolewa baada ya
Mwenyekiti wa Kijiji kufika eneo la tukio hilo.
Akielezea kwa kwa ufupi mkasa huo
uliotokea tarehe 24.2.2021 Mwenyekiti wa Kijiji hicho cha Tululu Frank Simon
alisema kuwa walipata taarifa ya kadhia hiyo wakati wakijiandaa kwa mkutano wa
Kijiji ndipo walifika kwenye eneo hilo na kukutana na mtoto wa umri wa miaka
mitano aliyekuwa akilia akiwa katika maji karibu na ukingo wa mto huku akiwa
ameshika kichwa cha mtumbwi uliokuwa umezama.
“Kama mimi Mwenyekiti kwa uchungu
uliokuwepo sikupata muda wa kufikiria, nilitumbukia kwenye maji, nikaogelea
hadi kumwokoa mtoto yule, na kuanza kumhoji na kujua idadi ya watu waliotumbukia
kwenye mto kuwa ni watu sita na dereva wa Saba, tukarudi tena kuhangaika na
kumpata kijana mwenye umri wa miaka 19, tukamuokoa, tumejitahidi kuitafuta
miili hiyo lakini mpaka hivi sasa haijapatikana, lakini tulitoa taarifa, ofisi
ya kata, kituo cha polisi, ofisi ya tarafa Pamoja na Kijiji cha jirani, Kijiji
cha Mkulwe, kata ya Mkulwe, Tarafa ya Kamsamba, Wilaya ya Momba, Mkani Songwe,”
Alisema.
Aidha alimuomba Mkuu wa Mkoa wa
Rukwa Mh. Joachim Wangabo kuwatafutia ufumbuzi wananchi wa Kijiji hicho kwa
kuwapatia daraja la dharura ili wananchi hao waepukane na majanga hayo na
kuwasadidia kumalizia zahanati yao ambayo imefikia usawa wa linta kwa nguvu za
wananchi wa kaya 276 za Kijiji hicho.
Naye Diwani wa Kata ya Kaoze Gidion
Fungameza alisema kuwa changamoto kubwa ya wananchi wa Kijiji hicho ni kutokuwa
na zahanati hali inayowafanya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya kwa
kuzingatia kuwa barabara kutokuwa nzuri hasa katika kipindi hiki wakati mvua
zikiendelea kunyesha.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Apolinary Macheta alisema kuwa miongoni mwa
miradi walioipitisha katika vikao vya bajeti ya halmashauri hiyo ni Pamoja na
ujenzi wa kituo cha afya cha kata ya Kaoze.
“Kwa kutumia mapato ya ndani
tumeamua tuhakikishe tunakamilisha kituo cha afya kimoja, na moja ya kituo
ambacho tumekipitisha kwenye baraza, ni kituo cha afya cha kata ya Kaoze,
kwahiyo jambo hili la kufuata huduma mbali kwaajili ya kituo cha afya,
tutakapokuwa tumekamilisha kama bunge litapitisha bajetihii kama tulivyokuwa
tumeomba, ndio kituo cha afya cha Kaoze kitatusaidia kusogeza huduma za afya
kwa watu wa kapenta na kipeta,” Alisema.
Pamoja na hayo Mkuu wa Wilaya ya
Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule aliushukuru uongozi wa Kijiji hicho kwa
ushirikiano walioutoa kwa serikali katika kusaidiana kuwatafuta watu hao
waliozama ambapo alisema kuwa baada tu ya kupata taarifa hiyo alihakikisha
jeshi la Zimamoto na uokoaji wanafika katika eneo hilo na kutoa msaada.
“Pamoja na hilo, niwashukuru sana
hasa wale waliojitolea kutumbukia mule kwenye mto kuwatafuta, nimeambiwa sasa
hivi mmehamia pale kirando (Kijiji cha jirani), tunawaomba vijana wote pale
mtakapohitajika na uongozi wa Kijiji au wa kata, basi mjitolee ili tuweze
kuwatafuta hawa wenzetu mpaka tuwapate,” Alisema.
Dkt. Khalfan Aliongeza kuwa huduma
muhimu zinapatikana katika Kijiji cha Kipeta ambacho hakifikiki kutoka kijijini
hapo kutokana na kukosekana kwa barabara yenye km 14 inayounganisha Kijiji
hicho cha Kipeta na Kijiji cha Tululu.
Wakati akitoa salamu zake za
rambirambi kwa wanakijiji wa Tululu Mh. Wangabo alimuagiza Mkurugezi wa halmashauri
hiyo kuhakikisha kuwa zahanati iliyoanza kujengwa na wananchi wa Kijiji hicho
inamalizika ndani ya mwaka huu wa 2021 na aidha alimuagiza Mratibu wa Wakala wa
Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kuhakikisha wanafanya matengenezo ya
dharura katika barabara ambazo zipo kwenye hatari ya kuwakosesha wananchi
mawasiliano na maeneo muhimu wanayofuata huduma za kijamii.
“Fedha zilizotengwa kwa mwaka
2021/2022 ni lazima iwekwe kwenye dharura, maeneo haya yanashida nyingi,
barabara huku haipitiki, wakienda kuvuka mto wanaliwa na mamba, wanatumbukia,
mitumbwi inabinuka na watu wanakufa, sasa hawa watu wakimbilie wapi? huko
hewani? Ni lazima tutatue matatizo hapa ardhini kwenye barabara yetu lakini pia
kwenye zahanati na tatu kwenye mto, hay ani maeneo makuu matatu ambayo ndio
msingi wa matatizo makubwa ya Kijiji hiki na vingine na kata hizi mbili,”
Alisema.
0 Comments