Ticker

6/recent/ticker-posts

ZAECA YAPEWA WIKI MOJA KUKAMILISHA UCHUNGUZI PAMPU SABA ZA KUSUKUMIA MAJI.


 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla ametoa muda wa wiki moja kwa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar {ZAECA} kukamilisha uchunguzi juu ya Pampu Saba za kusukumia Maji zilizonunuliwa na Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} hivi karibuni.

Alitoa kauli hio alipofanya ziara ya ghafla Makao Makuu ya Mamlaka ya Maji iliyopo Kinazini jirani na  Msikiti Mabuluu Mjini Zanzibar Mheshimiwa Hemed alisema amefikia uamuzi wa kutoa agizo hilo ili Serikali Kuu ipate kujiridhisha kama hakuna dalili yoyote ya harufu ya rushwa kwenye manunuzi hayo.

Mh. Hemed alisema Serikali kamwe haitovumilia kuona  Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} ambayo ni Taasisi muhimu inayogusa moja kwa moja maisha ya viumbe inazunguukwa na uzembe unaoweza kuleta athari pamoja na kupungua kwa Mapato ya Serikali.

Aliutaka Uongozi wa Mamlaka ya Maji kujisafisha kwa kuondoa hitilafu za migogoro ya Uongozi ndani ya kipindi cha Mwezi Mmoja vyenginevyo Serikali italazimika  kusafisha safu hiyo ya Uongozi kwa maslahi ya Umma.

Mheshimiwa Hemed alisema Wahandisi wa Taasisi hiyo wanapaswa kurekebisha miundombinu sambamba na kuweka utaratibu utakaoharakisha Watendaji wa Mamlaka hiyo kuwajibika ipasavyo ili kuwapa fursa Wananchi kupata huduma za maji safi na salama muda wote.

Alisema wazi kwamba hali ya uwajibikaji kwa Watendaji wa Mamlaka ya Maji haiko vizuri kutokana na tabia ya muhali inayochukuwa nafasi kubwa na matokeo yake hata makusanyo ya Mapato yatokanayo na Huduma za Maji hayafikii lengo halisi lililokusudiwa.

Alieleza kuwa  suala hilo ni vyema likaenda sambamba kwa Watendaji hao kuhakikisha kwamba Wananchi na Taasisi zote zinazotumia huduma hiyo zinawajibika kulipa huduma hiyo ili Taasisi hiyo iweze kujiendesha badala ya kuendelea kupeleka maombi ya kupatiwa fedha Serikali Kuu.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} Nd. Mussa Ramadhan Haji alisema hali ya upatikanaji wa huduma za maji safi na salama ndani ya Visiwa vya Unguja na Pemba  kwa sasa imefikia asilimia 80% hadi 85% kutegemea matumizi yaliyopo.

Nd. Mussa alisema wakati mwengine hali hiyo hushuka hadi asilimia 75% kutokana na baadhi ya Visima kukumbwa na hitilafu za Umeme lakini pia baadhi ya mashine za kusukumia Maji huharibika  kutokana na kutumika kwa muda mrefu hasa katika baadhi ya maeneo yasiyo na Matangi ya kuhifadhia Maji.

Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu huyo wa Mamlaka ya Maji Zanzibar alibainisha kwamba katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na huduma za usambazaji Maji Wataalamu wake wameanza kufanya Utafiti wakianzia eneo la Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja ili kubaini kasoro zinazochangia uwepo wa changamoto hizo.

Nao kwa upande wao Wakurugenzi wa vitengo mbali mbali vya Mamlaka hiyo walimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba muitiko wa Wananchi kuendelea kulipa huduma za Maji ni mdogo wakitoa sababu za kutokupata huduma hiyo kwa uhakika.

Walisema hivi sasa wapo katika utaratibu wa kujiandaa kufunga Mita kwa watumiaji wote wa Huduma hiyo mpango ambao utatoa uhalisia wa upatikanaji wa maji kwa wateja licha ya kwamba wapo baadhi yao hulalamikia ukosefu wa huduma hiyo wakati majumbani mwao yamejaa.

 

 

Post a Comment

0 Comments