Ticker

6/recent/ticker-posts

Wanawake na Uongozi: Ni Wakati wa Kuvunja Ukimya na Kuchukua Nafasi

 


Na Ahmed Abdulla, Zanzibar:


Wanawake Zanzibar si wachache, na si dhaifu Kwa mujibu wa Sensa ya 2022, wanawake ni zaidi ya nusu ya wananchi, lakini bado uwakilishi wao katika uongozi wa kisiasa uko chini ya matarajio. 


Swali kubwa ni moja: kwa nini sauti za wanawake bado hazisikiki sawasawa katika maamuzi ya taifa?


Kwa miaka mingi, wanawake wameongoza majumbani wakilea, wakisimamia rasilimali na kujenga maadili ya jamii. 


Leo, uongozi huo unahitaji kuvuka mipaka ya nyumba na kufika kwenye mabaraza ya maamuzi. 


Uongozi wa mwanamke si neema, ni haki ya msingi inayotambuliwa na mikataba ya kimataifa kama CEDAW, ambayo Tanzania ni mwanachama wake.


Licha ya kuwepo kwa fursa, takwimu za uchaguzi wa 2025 zinaonesha kuwa wanawake wachache sana walifanikiwa kushinda kwa kura za moja kwa moja, katika nafasi za katika baraza la wawakikishi  ikiwa ni wanawake wanne 4 tu walioshinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo ukilinganisha na uchaguzi wa mwaka 2020 uwakilishi wa wanawake nane 8 huku wengi wakitegemea viti maalum.


Katika harakati za kuimarisha ushiriki wa wanawake katika uongozi wa kisiasa Zanzibar, vyama vya siasa vina nafasi kubwa ya kufungua au kufunga milango ya mabadiliko.


 Ingawa wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha jamii, bado uwakilishi wao katika nafasi za maamuzi zinasuasua kutoana na  idadi yao halisi ya kupata nafasi hizo.



Zanlight blog ilizungumza na mwakilishi wa jimbo la konde kupitia chama cha Mapinduzi CCM Zawad Amour ambae anaongoza kwa kipindi cha awamu ya pili sasa tokea mwaka 2020 hadi sasa alisema jambo la muhimu kwa wanawake ni kujiamini na kuwa na ujasiri katika harakati za kugombea nafasi hizo licha ya kuwa kuna vikwazo ambavyo wanawake hukutana navyo wakati wa kugombea.


Alisema   kuwa uongozi wa mwanamke ni nyenzo muhimu katika kuleta uwiano na maamuzi jumuishi katika jamii na taifa kwa ujumla.


Pamoja na hayo alisema jamii inatakiwa  kuwaunga mkono wanawake wanaojitokeza kugombea nafasi za uongozi  badala ya kuwakatisha tamaa kwa misingi ya kijinsia.


"Kwangu haikuwa rahisi kuingia tena kwa awamu pili mengi nilipambana nayo ikiwemo mtazamo wa kijinsia katika jamii kukubwa ambacho kilinipa nafasi ya kuongoza tena ni namna ambavuo niliweza kuleta mabadiliko ya maendeleo katika jimbo langu alieleza Zawadi".



“Wanawake wasiwe na hofu. Uongozi ni uwezo na dhamira, si jinsia,” alisisitiza Zawad.



Halima Ibrahim ni msemaji wa sekta ya maendeleo ya wanawake watoto na makundi maaalum kutoka chama cha a ACT-Wazalendo, alisema bado mifumo ya kisiasa na kijamii imekuwa kikwazo kwa wanawake wengi, hasa katika kushinda kwa kura za moja kwa moja katika majimboni hivyo jitihada zinahitajika zaidi licha ya wanawake hujitokeza kwa wingi kugombea nafasi hizo.


 Alieleza kuwa chama cha Act Wazalendo  kinaamini katika uongozi unaozingatia usawa na haki kwa wote. 


Alisema wanawake wameanza kuchukua hatua za makusudi kujitoa kwenye kivuli cha viti maalum na kuwania nafasi za ushindani hasa majimboni ili kukuza usawa wa kijinsia katika nafasi za uongozi lakini bado changamoto za kuingia katika nafasi hizo majimboni ni kizungumkuti.


“Tumekataa kubaki watazamaji  wanawake kwa sasa  tumeamua kushindana na kushinda,” alisema kwa msisitizo bihalima."


Kwa upande wake Nadhira Ali Haji aliyekuwa mgombea wa ubunge jimbo la Malindi kupitia chama cha Adc alisema  changamoto kubwa kwa wanawake ni  mitazamo hasi ya jamii kuhusu uwezo wa mwanamke kuongoza.


 Aliseleza kuwa mapambano makubwa yapo katika kubadili fikra za kijamii zilizo zoeleka kwa muda mrefu licha ya jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na taasisi binafsi ikiwemo TAMWA Zanzibar katika kuhakikisha wanamuwezesha mwanamke na kumjengea uwezo katika masuala ya uongozi lakni bado hazijafikiwa asilimia Mia.


Alisema kuwa  elimu ya uraia na uhamasishaji vina nafasi kubwa katika kufanikisha mabadiliko hayo.


“Jamii ikiamini mwanamke anaweza, basi uongozi wa mwanamke hauwezi kuwa tatizo,” aliasema Binadhira.



Pamoja na hayo Rahima Sharif kutoka chama cha CHAUMA na Zuhura Mussa Karata kutoka chama cha wananchi CUF walisema vyama viidogo navyo vina wajibu wa kuhakikisha wanawake hawabaki nyuma katika siasa. 


Walisema fursa za uongozi zinapaswa kutolewa kwa haki na kwa vitendo, si kwa kauli pekee.


Walieleza kuwa wanawake wengi wana uwezo mkubwa wa kuongoza lakini hukosa fursa kutokana na rasilimali  fedha pamoja na kukatishwa tamaa na baadhi ya wanajamii.


“Wanawake wana uwezo mkubwa wa kuongoza  kinachohitajika ni kuaminiwa na kupewa nafasi sawa ya kushindana,” walisema.


Hata hivyo makala hii ilizungumza na Mratibu wa masuala ya uhamasishaji wa wanawake katika uongozi kutoka chama cha Wandishi wa Habari wanawake Tamwa kwa upande wa Zanzibar (TAMWA ZNZ) Sabrina Yussuf Mwintanga alisema miongoni mwa mikakati ya chama hicho ni kumuhamasisha na kuwawezesha  kmwanamke katika masuala ya uongozi ili kuweza kufikia asilimia 50 kwa 50 katika nafasi mbalimbali za uongozi.


Alisema mwanamke akipewa nafasi ya kuongoza mara nyingi hisimamia imara na mwenye maono makubwa katika kuyafikia mafanikio makubwa katika jamii yake iliyomzunguka.


Uongozi wa wanawake haupaswi kuwa mjadala wa ahadi bali wa utekelezaji hivyo wanawake wako tayari kwa kujitolea kwa hali na mali na kuwa na  ujasiri katika utekelezaji wa majukumu yao sambamba na  maono ya kuongoza. 


Kilichobaki sasa ni jamii, vyama na mifumo ya uchaguzi kuhakikisha haki hiyo inatekelezwa kwa vitendo.

Post a Comment

0 Comments