Na Berema Nassor, Zanzibar
Katika miezi sita ya mwanzo ya maisha ya mtoto, hakuna chakula chenye thamani kubwa kama maziwa ya mama.
Wataalamu wa afya duniani, ikiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) na UNICEF, wanapendekeza mtoto anyonyeshwe maziwa ya mama pekee kwa kipindi hicho bila kupewa maji, juisi, uji, au chakula kingine chochote isipokuwa dawa au vitamini kwa maelekezo ya kitaalamu.
Mwongozo huu umepewa msisitizo maalum kupitia Sera ya Afya ya Zanzibar (2011) na Kanuni za Kitaifa za Unyonyeshaji Bora wa Mtoto, ambazo zinasisitiza umuhimu wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee katika kipindi hiki muhimu kwa ukuaji na kinga ya mtoto.
Maziwa ya mama yanatosheleza mahitaji yote ya mtoto kimwili, kiakili, na kimfumo wa kinga. Yana virutubisho kamili vinavyosaidia ukuaji wa ubongo, kuimarisha kinga mwilini, na kuzuia magonjwa ya mara kwa mara kama kuhara, homa ya mapafu, na maambukizi.
Zaidi ya hilo, unyonyeshaji wa maziwa ya mama huimarisha uhusiano wa kihisia kati ya mama na mtoto.
Sera ya Afya ya Uzazi na Mtoto Zanzibar inatambua kuwa watoto wengi hupoteza maisha kwa magonjwa yanayoweza kuzuilika endapo wangepata maziwa ya mama kwa ukamilifu katika miezi sita ya mwanzo.
“Sera hii inasisitiza kuwa kila mama anapaswa kupewa elimu kuhusu faida za unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kuanzia kliniki ya kwanza ya ujauzito,” inaeleza sehemu ya sera hiyo.
Hata hivyo, changamoto bado zipo ikiwa ni pamoja na imani potofu kwamba mtoto anapaswa kupewa maji kutokana na joto la mazingira, au ushawishi wa familia kuhusu vyakula vya ziada, zimeendelea kudhoofisha utekelezaji wa mwongozo huu muhimu.
Kwa upande wake, Mratibu wa Masuala ya Lishe Zanzibar, Fatma Ali Said, kutoka Kitengo cha Lishe cha Wizara ya Afya Zanzibar, alisema miongoni mwa jitihada zinazochukuliwa ni kutoa elimu endelevu kwa akina mama kuhusu umuhimu wa kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama kwa miezi sita ya awali.
“Mara nyingi akina mama hawafuati kanuni na taratibu za unyonyeshaji, jambo linalosababisha watoto kuathirika na magonjwa kama utapiamlo. Ni muhimu kufuata ushauri wa wataalamu na kuacha mila na desturi zinazoathiri afya za watoto,” alisema Fatma.
Aidha, Asha Suleiman, mama wa mtoto wa miezi mitano kutoka Kijiji cha Kiboje, Wilaya ya Kati Unguja, alisema uzoefu wake wa kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama pekee umemsaidia kutambua faida kubwa ya unyonyeshaji.
“Mtoto wangu amekuwa mwenye afya njema na hajawahi kuugua mara kwa mara. Mwanzoni nilidhani anatakiwa apewe maji, lakini baada ya kupata elimu kutoka kituo cha afya, nilielewa kuwa maziwa ya mama yanatosha kabisa,” alisema Asha.
Si mama pekee ndiye anayehusika bali na baba pia wanapaswa kushirikiana kikamilifu juu ya kuhakikisha kuwa mtoto anapata maziwa ya mama pekee kwenye kipindi hicho.
Mohamed Khamis, baba kutoka Mkokotoni, Unguja, alisema: “Nilijifunza kutoka kliniki kuwa maziwa ya mama yanatosha kwa miezi sita. Niliamua kumpa mke wangu ushirikiano kamili hakupokei kitu kingine chochote. Mtoto wetu amekuwa na afya njema, hakupata homa wala kuharisha. Ushirikiano wa baba ni muhimu, kwani malezi ni jukumu la wote.”
Mohamed aliongeza kuwa wengi wa wanaume bado hawashiriki kikamilifu kutokana na mitazamo ya kijamii, lakini ushirikiano wa baba unaongeza asilimia 40 ya uwezekano wa mafanikio ya unyonyeshaji wa miezi sita ya mwanzo, kulingana na takwimu za Wizara ya Afya Zanzibar.
Kanuni za Unyonyeshaji Zanzibar (2020) zinakataza matangazo ya vinywaji mbadala vya maziwa ya mama kwa watoto chini ya miezi sita na zinahimiza mafunzo kwa wakunga, wahudumu wa afya ngazi ya jamii, na familia kwa ujumla.
Hii inalenga kuhakikisha elimu sahihi inawafikia akina mama wote na kushirikisha wanaume katika malezi.
Kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo si jambo la hiari, bali ni haki ya mtoto kupata afya bora na maisha salama.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa unyonyeshaji huu kama njia ya kupunguza vifo vya watoto wachanga na kuboresha ustawi wa familia.
Ni wajibu wa familia, waajiri, na jamii kwa ujumla kumuunga mkono mama na mtoto kwa ajili ya kizazi chenye afya bora, kinga imara, na mustakabali salama wa taifa.


0 Comments