Ticker

6/recent/ticker-posts

Vijana Zanzibar Kunufaika Na Huduma Rafiki Za Afya Ya Uzazi


Na Berema Nassor, Zanzibar

Katika jamii nyingi, vijana wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali za afya ya uzazi kutokana na ukosefu wa elimu sahihi na upatikanaji mdogo wa huduma stahiki.

Hali hii imechangia ongezeko la mimba za utotoni, magonjwa ya zinaa, na matumizi yasiyo sahihi ya njia za uzazi wa mpango.

Hata hivyo, hatua zinazochukuliwa sasa Zanzibar kupitia huduma rafiki kwa vijana zinaonekana kuwa suluhisho la kudumu katika kupunguza changamoto hizi.

Huduma rafiki kwa vijana (Youth Friendly Services) ni mfumo wa huduma za afya unaolenga kuwafikia vijana katika mazingira yanayowapa faragha, ushauri wa kitaalamu, na taarifa sahihi kuhusu afya ya uzazi.

Huduma hizi zinalenga kuwasaidia vijana kufanya maamuzi sahihi kuhusu miili yao, mahusiano, na mustakabali wa afya zao.

Mratibu wa mradi wa Haki ya Afya ya Uzazi kwa Wanawake na Wasichana kutoka Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ), Zaina Abdalla Mzee, alisema elimu ya afya ya uzazi ni silaha muhimu kwa vijana na wanawake ili kuepuka matatizo yanayotokana na ukosefu wa maarifa.

“Tumeona vijana wengi hawana uelewa kuhusu afya zao, hasa kwenye masuala ya uzazi kama saratani ya shingo ya kizazi na matumizi salama ya uzazi wa mpango. Elimu inawasaidia kujitambua na kujikinga na athari zinazoweza kuepukika,” alisema Zaina.

Kwa upande wa, Warda Khatib Khamis, mhudumu wa afya ngazi ya jamii, alisisitiza umuhimu wa elimu bora ya afya ya uzazi kuanzia katika ngazi ya familia.

“Ni muhimu vijana kupatiwa elimu ya afya ya uzazi mapema, ndani ya familia. Hii itawasaidia kuelewa namna ya kujiepusha na mambo hatarishi yanayoweza kuathiri mustakabali wao,” alisema Warda.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imekuwa ikiendelea na jitihada zake za kuhakikisha inatoa huduma bora za afya kwa wananchi wake ikiwa ni pamoja na utoaji elimu sahihi ya afya ya uzazi

Kwa kushirikiana na UNFPA na UNICEF, ilizindua kituo cha huduma rafiki kwa vijana (Youth Friendly Services Clinic) huko Bumbwisudi, Mkoa wa Mjini Magharibi, mnamo Februari 2023 ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha vijana wanapata huduma za uzazi zenye ubora na taarifa sahihi.

Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Mazrui, alisema kuwa Vijana wengi wamekuwa wakitumia njia za uzazi wa mpango bila ushauri wa kitaalamu, jambo linalosababisha madhara ya kiafya na kupelekea kudhani kuwa njia hizo si salama.

“Tatizo haliko kwenye njia, bali ni ukosefu wa taarifa sahihi. Huduma hizi rafiki zitawawezesha vijana kupata taarifa kwa wakati na ushauri wa kitaalamu.” Alisisitiza Mazrui

Kwa mujibu wa Sera ya Afya ya Taifa ya 2007 na Mpango wa Kitaifa wa Uzazi wa Mpango (2019–2023), elimu na huduma bora za afya ya uzazi ni haki ya msingi kwa kila kijana, mwanamke na mwanaume.

Utekelezaji wa huduma rafiki unalenga kutimiza Lengo namba 3 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) linalohimiza upatikanaji wa afya bora kwa wote.

Kwa ujumla, huduma rafiki kwa vijana si tu zinasaidia kupunguza mimba za utotoni na magonjwa ya zinaa, bali pia zinajenga kizazi chenye uelewa, heshima, na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya zao.

Ni wazi kwamba, kuwekeza katika huduma hizi ni kuwekeza katika mustakabali wa taifa lenye vijana wenye afya bora, wenye ndoto, na wanaochangia kikamilifu katika maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.


Post a Comment

0 Comments