Ticker

6/recent/ticker-posts

Afya Ya Uzazi Vijijini Yaanza Kuona Mwanga


Na Ahmed Abdulla, Zanzibar

Kwa kipindi cha nyuma, upatikanaji wa huduma za afya vijijini ulikuwa changamoto kubwa kwa wanawake na jamii kwa ujumla.

Huduma muhimu kama uzazi wa mpango, uchunguzi wa ujauzito, huduma za kujifungua, pamoja na elimu ya afya ya uzazi, zilikuwa haba au hazipatikani kabisa katika maeneo mengi ya vijijini.

Sababu kuu za hali hii zilihusishwa na ukosefu wa vituo vya afya vya karibu, mila na desturi zilizowazuia wanawake kutafuta huduma, pamoja na ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu afya ya uzazi.

Hali hiyo ilionyesha wazi pengo kubwa kati ya huduma za afya za mijini na vijijini, jambo lililoibua haja ya kuimarisha mifumo ya afya ili kuhakikisha kila mwanamke, popote alipo, anapata huduma stahiki kwa wakati.

Wasila Ame Zubeir, muuguzi na mkunga katika kitengo cha huduma za uzazi, wajawazito na watoto katika kituo cha afya cha Mkokotoni, alisema kuwa kwa sasa muamko wa jamii vijijini umeongezeka katika kuhudhuria vituo vya afya, ingawa bado zipo changamoto kadhaa.

“Changamoto kubwa ni kwa wanaume kutoshiriki kliniki pamoja na wake zao. Hili bado ni tatizo, hivyo nawashauri mama wajawazito kuhudhuria kliniki wakiwa na waume zao ili kwa pamoja waweze kuelewa changamoto zinazojitokeza wakati wa ujauzito,” alieleza Wasila.

Kwa upande wake, Hadia Ali Makame, mkazi wa Mkokotoni, alisema kuwa huduma za afya kwa sasa zimeboreshwa sana kutokana na ujenzi wa hospitali katika kila wilaya, jambo lililowezesha wananchi wengi kuzifikia huduma hizo kwa urahisi.

“Kilichosalia sasa ni kwa mtu binafsi kuchukua hatua ya kuhudhuria vituo vya afya. Tulikotoka ni mbali sana ukilinganisha na tulipofikia sasa, tukiwa na hospitali za kisasa na wataalamu wa kila aina,” alisema Hadia.

Vilevile, Asya Fadhil Makame, mhudumu wa afya ngazi ya jamii katika shehia ya Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini ‘A’, alieleza kuwa kwa sasa wananchi wengi wanahudhuria vituo vya afya, lakini bado uuelewa wa wanawake kuhusu uzazi wa mpango ni mdogo.

“Licha ya juhudi za kuhamasisha uzazi wa mpango, bado wanawake wengi wanashindwa kujiunga kutokana na mila potofu. Ninawahimiza wanawake wa shehia ya Mkokotoni kujiunga na uzazi wa mpango ili kuimarisha afya zao na afya za watoto wao,” alisema Asya.

Kwa upande mwingine, Seif Moh’d Kombo (si jina lake halisi), mkazi wa eneo hilo, alisema kuwa ingawa huduma zimeboreshwa kwa kiwango kikubwa, bado wanaume hawajaonyesha mwitikio wa kutosha kushiriki katika huduma za afya pamoja na wake zao.

“Ili kuelewa vizuri huduma za afya kwa mama wajawazito, ni muhimu kuhudhuria kliniki kwa pamoja. Hivyo ndivyo tunavyoweza kutatua changamoto na kuepuka matatizo yanayoweza kuzuilika,” alieleza.

Pamoja na mafanikio haya, bado kuna haja ya kuendelea kuelimisha jamii kuhusu ushiriki wa wanaume katika masuala ya afya ya uzazi, sambamba na kuongeza uboreshaji wa miundombinu ya afya vijijini.

Kwa ujumla, kuboresha huduma za afya ya uzazi vijijini ni hatua muhimu na ya lazima katika kuinua maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla kwani afya bora ya mama na mtoto ndiyo msingi wa kizazi imara na chenye matumaini.


Post a Comment

0 Comments