Na Berema Nassor, Zanzibar
Uzazi wa mpango si tu suala la afya, bali ni chombo muhimu cha kumkomboa mwanamke kutoka katika mateso ya uzazi usiopangilika.
Katika jamii nyingi, wanawake wamekuwa wakikabiliwa na mzigo mkubwa wa kuzaa mara kwa mara, hali inayowaathiri kiafya, kiakili na kiuchumi.
Kupitia matumizi ya njia salama za uzazi wa mpango, mwanamke hupata nafasi ya kupumzika, kupanga maisha yake na kutimiza malengo binafsi na ya familia kwa wakati unaofaa.
Salama Masingwa, mkazi wa Kinuni na mama wa watoto watano, alisema baada ya kuanza kutumia njia ya uzazi wa mpango maisha yake yalibadilika, na kumpa nafasi ya kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo uongozi.
“Nilipokuwa nikiingia ujauzito kila mara nilikosa muda wa kufuatilia harakati zangu. Lakini tangu nijiunge na uzazi wa mpango, nimeweza kupanga maisha yangu vizuri na kufikia malengo yangu,” alisema Salama.
Aidha, alihamasisha wanawake wenzake kujiunga na huduma za uzazi wa mpango ili kujiepusha na athari za uzazi wa mara kwa mara na kujipatia uhuru wa kupanga maisha yao.
Khairat Salum Abdalla, muuguzi na mkunga katika Hospitali ya Wilaya ya Kitogani, Wilaya ya Kusini Unguja, alisema njia za uzazi wa mpango ni salama na hazisababishi madhara yoyote ya kiafya endapo zitatumika ipasavyo.
Alisema tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa uzazi wa mpango unaweza kuzuia zaidi ya asilimia 80 ya vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi usio salama.
“Kwa sasa kumekuwepo na mwamko mkubwa wa wanawake kujiunga na uzazi wa mpango kutokana na elimu ya uhamasishaji inayoendelea kutolewa katika jamii,” alieleza Khairat.
Aliongeza kuwa kila mwanamke huchagua njia ya uzazi wa mpango kulingana na hali yake ya kiafya na ushauri wa wataalamu.
Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu ya mwaka 2006 inatambua umuhimu wa kuwaelimisha wanawake kuhusu faida za uzazi wa mpango kama sehemu ya mkakati wa kuimarisha afya ya uzazi.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Hali ya Idadi ya Watu Duniani ya mwaka 2022 iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), karibu mimba milioni 121 duniani kila mwaka ni mimba zisizotarajiwa.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa idadi kubwa ya mimba zisizotarajiwa ni ishara ya kushindwa kwa dunia kulinda haki za msingi za wanawake na wasichana.
“Hali hii inasababisha baadhi ya familia kuwa na watoto wengi au wachache zaidi ya walivyotarajia, jambo linaloathiri maisha ya familia na jamii kwa ujumla,” alisema Dkt. Natalia Kanem, Mkurugenzi Mkuu wa UNFPA.
Fadhili Hamis Hamad, mkazi wa Hawai, alisema wanawake wa sasa wanapaswa kutumia huduma za uzazi wa mpango kwa manufaa ya familia na taifa.
“Wanawake wengi siku hizi ni wafanyabiashara na wajasiriamali. Ili kufikia malengo yao ya kiuchumi, wanahitaji muda wa kupanga na kupumzika kati ya uzao na uzao. Bila hivyo, ni vigumu kufikia mafanikio,” alisema Fadhili.
Aliongeza kuwa njia bora na sahihi ya kumkomboa mwanamke ni kujiunga na huduma za uzazi wa mpango ili aweze kufanya kazi zake kwa ufanisi na kuwa na maisha bora.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto, ikiwemo kuhamasisha matumizi sahihi ya uzazi wa mpango.
Kwa ujumla, uzazi wa mpango ni nguzo muhimu ya kumkomboa mwanamke, kwani humpa nafasi ya kupanga maisha yake, kutunza afya, na kuchagua idadi ya watoto anaotaka kuzaa bila kuhatarisha afya yake.
Jamii inapaswa kuendelea kuhamasishana kuhusu umuhimu wa kujiunga na huduma hizi, kwa kuwa ni njia sahihi ya kujenga familia zenye afya, utulivu na maendeleo endelevu.
0 Comments