Ticker

6/recent/ticker-posts

Upungufu Wa Damu Kwa Mama Mjamzito Unahatarisha Maisha




Na Berema Nassor, Zanzibar

Upungufu wa damu kwa mama mjamzito ni tatizo linalohatarisha afya ya mama na mtoto aliyeko tumboni. Tatizo hili limekuwa likiwakumba wanawake wengi hasa katika jamii zenye kipato cha chini na huduma duni za afya.

Mara nyingi dalili zake huanza kama uchovu wa kawaida, lakini ndani ya mwili kunakuwa na hali hatarishi inayoweza kusababisha kuharibika kwa mimba, kujifungua mapema au hata kifo wakati wa kujifungua ikiwa hakutakuwa na matibabu sahihi.

Ruqaiya Haji, mkazi wa Regeza Mwendo Mwera, alisema alianza kujihisi kuchoka kupita kiasi, kupumua kwa shida na kuumwa kichwa, hali aliyodhani ni ya kawaida ya ujauzito.

“Nilihisi kama mwili wangu unaniacha, nikawa sina nguvu kabisa. Nilipoenda hospitali nikagundulika nina upungufu mkubwa wa damu,” alisema Ruqaiya.

Alisema baada ya kugundulika tatizo hilo alianza kutumia dawa za Folic Acid na kuzingatia ulaji wa vyakula vyenye lishe bora kama alivyoshauriwa na mtaalamu wa afya, na hali yake ilianza kuimarika.

Daktari Nicolus Kikoti wa Hospitali ya Wilaya ya Ijtimai alisema mama mjamzito mwenye upungufu wa damu anatakiwa kupata matibabu ya haraka ili kurejesha kiwango cha damu kabla ya kujifungua.

“Upungufu wa damu unaweza kumsababishia mtoto kukosa ukuaji wa kawaida tumboni, hivyo ni muhimu mama ahudhurie kliniki mapema na kupata lishe bora,” alisema.

Alisema tatizo hilo linaweza kuzuilika endapo jamii itaelimishwa kuhusu ulaji wa mlo kamili, chanjo, na umuhimu wa kuhudhuria kliniki mapema.

“Suluhisho la upungufu wa damu linaanzia nyumbani kupitia ulaji bora na upangaji wa familia. Hii itasaidia kuzuia matatizo kwa mama na mtoto,” aliongeza.

Kwa upande wake, mume wa Ruqaiya alisema awali alidhani ujauzito ni hali ya kawaida bila kujua upungufu wa damu unaweza kuhatarisha maisha.

“Sikujua kama tatizo hili linaweza kusababisha kifo cha mama au mtoto. Baada ya kupewa elimu, nilihakikisha mke wangu anapata matibabu,” alisema.

Alisema ni wajibu wa wanaume kushiriki kikamilifu katika afya za wake zao ili kuwasaidia kuepuka matatizo ya uzazi.

Upungufu wa damu kwa mama mjamzito si jambo dogo, ni tatizo linalohitaji uelewa na hatua za haraka. Ukosefu wa elimu, lishe duni na huduma hafifu za afya umeendelea kuchangia kuongezeka kwa tatizo hilo vijijini.

Jamii inahimizwa kuhakikisha mama mjamzito anapata lishe bora, elimu sahihi na huduma za afya kwa wakati ili kulinda uhai wake na mtoto aliyeko tumboni.


Post a Comment

0 Comments