Na Ahmed Abdulla, Zanzibar
Vijana ni kundi lenye nguvu, ubunifu na ndoto kubwa za kubadilisha dunia.
Hata hivyo, licha ya uwezo huo, bado wanakabiliwa na changamoto nyingi katika safari yao ya kufikia mafanikio, ikiwemo upungufu wa elimu sahihi kuhusu afya ya uzazi, lishe, afya ya akili, kinga dhidi ya magonjwa ya zinaa na ushauri nasaha wa maisha bora.
Utafiti uliofanywa na UNICEF kwa kushirikiana na Serikali ya Zanzibar mwaka 2023 ulionesha kuwa vijana wengi, hasa wa vijijini, hawapati taarifa muhimu za afya kwa wakati.
Hii inatokana na ukosefu wa mawasiliano ya wazi kati ya wazazi, walezi na vijana kuhusu masuala ya afya ya uzazi, mienendo salama ya maisha na mabadiliko ya kimwili na kihisia.
Fatma Yussuf Amour, muelimishaji rika na mtoa huduma katika kituo cha huduma rafiki kwa vijana (YFS Mwera), Wilaya ya Kati, alisema elimu ya afya ya uzazi bado ni changamoto katika maeneo mengi ya Zanzibar kutokana na mila, hofu, na upotoshaji wa taarifa.
“Tunapowaelimisha vijana kuhusu afya ya uzazi na stadi za maisha, tunawapa silaha ya kujiamini, kujitambua na kujilinda. Elimu hii haichochei tabia hatarishi bali inasaidia kuzuia,” alifafanua Fatma.
Aidha aliongeza kuwa kumpa kijana taarifa sahihi kuhusu afya yake humjengea uwezo wa kufanya maamuzi bora, jambo linalochangia ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa.
Ali Hamad Mohammed na Aziza Haji Khamis, wazazi wakazi wa Mji Mwema, Mwera, walisema wazazi wengi hukosa muda wa kuzungumza na vijana wao kutokana na majukumu ya kila siku, jambo linalowaacha vijana wakitafuta majibu mitandaoni au kwa marafiki.
“Elimu ya afya inapaswa kuanzia nyumbani. Tukinyamaza, vijana watajifunza kutoka vyanzo visivyo sahihi, na si kila taarifa mitandaoni ni ya kweli. Kuwafundisha mapema ni njia bora ya kuwalinda kabla ya madhara kutokea,” walieleza kwa pamoja.
Kwa upande wake, Zainab Rashid Abdalla (22), aliyemaliza kidato cha nne mwaka 2024, alisema elimu ya afya imemsaidia kuelewa mabadiliko ya mwili na hisia zake, kujitunza, na kufanya maamuzi sahihi.
“Elimu ya afya imenisaidia kujitambua, kuchagua marafiki wa kweli na kuelewa umuhimu wa afya ya akili. Bila elimu sahihi, ni rahisi kupotea kwenye mitandao au makundi ya mitaani,” alisema Zainab.
Zawadi Suleiman Mcha, mwalimu katika Skuli ya Sekondari Regeza Mwendo, alisema kuwapatia vijana elimu ya afya ya uzazi ni kuwajengea mwanga wa kuelewa miili yao, kuheshimu mipaka na kufanya maamuzi yenye busara.
“Elimu hii huwasaidia vijana kutambua hatari za mimba za utotoni, magonjwa ya zinaa, na unyanyasaji wa kingono, sambamba na kuwajengea ujasiri wa kujithamini na kupanga mustakabali wao,” alisema mwalimu Zawadi.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya na Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeendelea kutekeleza mikakati ya kuwaelimisha vijana kuhusu afya ya uzazi, pamoja na kuimarisha vituo vya Youth Friendly Services (YFS) ili kutoa ushauri nasaha, elimu na huduma rafiki kwa vijana kote nchini.
Aidha, wadau wa maendeleo na mashirika yasiyo ya kiserikali wameendelea kushirikiana na serikali katika kutoa elimu ya afya, semina na programu za mafunzo zinazolenga kujenga kizazi chenye maarifa, afya bora na maadili mema.
Elimu ni nguzo imara ya maendeleo. Vijana wanaopewa elimu sahihi hujengewa uwezo wa kufikiri kwa kina, kufanya maamuzi yenye tija na kujenga maisha bora kwao na kwa taifa. Elimu hufungua milango ya fursa, huimarisha maadili na kuwaandaa vijana kuwa viongozi wa kesho wenye dira, uadilifu na maono ya maendeleo endelevu.
0 Comments