Ticker

6/recent/ticker-posts

Mimba Za Mapema Changamoto Kwa Maendeleo Ya Wasichana


Na Ahmed Abdulla,Zanzibar

Mimba za mapema zimeendelea kuwa changamoto kubwa katika jamii nyingi, hususan kwa wasichana wa umri mdogo. Tatizo hili linaathiri maisha yao ya kielimu, kijamii, kiafya na hata kisaikolojia.

Katika mahojiano maalum na Bingoli Ali Makame, mwalimu msaidizi wa ushauri nasaha katika Skuli ya Sekondari Regeza Mwendo, Wilaya ya Magharibi ‘A’, alisema mimba za mapema zinachangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa kiwango cha elimu miongoni mwa wasichana, kwani wengi hukatisha masomo yao ghafla.

“Hali hii inasababisha wasichana wengi kushindwa kutimiza ndoto zao za kielimu, na hatimaye jamii inakosa nguvu kazi ya kike iliyoelimika,” alisema Bingoli.

Aliongeza kuwa walimu hukabiliana na changamoto ya kuwahamasisha wasichana waliopata mimba kurejea shuleni, jambo ambalo mara nyingi hukwazwa na upinzani kutoka kwa wazazi au jamii.

Miza Rashid Mussa, mwanafunzi aliyepata ujauzito akiwa shuleni (jina la shule limehifadhiwa), alisema alipopata ujauzito alihisi huzuni kubwa na kukosa hamasa ya kurudi tena shuleni, jambo lililosababisha wazazi wake kumuozesha akiwa bado mdogo. Sasa ni mama wa nyumbani.

“Ni wazi kuwa kuna haja kubwa ya kupatiwa msaada wa kisaikolojia kwa wasichana wanaopata mimba za mapema ili waweze kurejea kwenye maisha yao ya kawaida kabla ya ujauzito,” alisema Miza.

Kwa upande wake, Thaniya Ibrahim Maabad, muuguzi na mkunga katika Hospitali ya Wilaya ya Kitogani, Wilaya ya Kusini Unguja, alisema kiafya wasichana wanaopata mimba wakiwa wadogo hukumbana na matatizo wakati wa kujifungua kama vile Fistula, kutokana na miili yao kutokuwa imekomaa.

“Ni muhimu elimu ya afya ya uzazi kutolewa mashuleni ili wasichana waweze kujikinga na mimba zisizotarajiwa, jambo litakalowasaidia kutimiza ndoto zao na kuepuka madhara ya kiafya,” alifafanua Thaniya.

Salama Tahir, Mratibu wa Wanawake na Watoto Shehia ya Muembe Mchomeke, alisema jamii inapaswa kushirikiana kujenga mazingira rafiki kwa wasichana waliopata mimba, ili waweze kurejea shuleni na kuendelea na masomo yao.

“Iwapo tutashirikiana katika kuwalinda wasichana na kuelimisha wazazi juu ya athari za mimba za utotoni, sambamba na kutoa elimu ya afya ya uzazi mashuleni, tutaweza kupunguza mimba zisizotarajiwa,” alisema Salama.

Mwanajamii Maulid Kombo Ismail, mkazi wa Muembe Mchomeke, aliongeza kuwa jamii inapaswa kuwa sehemu ya suluhisho kwa kuwapa wasichana maarifa, msaada na mazingira salama ya kufikia ndoto zao.

“Elimu ya afya ya uzazi kwa wasichana itawasaidia vijana kuelewa umuhimu wa elimu kama nyenzo ya kujenga maisha bora ya baadaye,” alisema Maulid.

Kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na Wizara ya Afya, imekuwa ikitekeleza mikakati ya kuhakikisha wasichana wanaopata ujauzito wanarejea shuleni baada ya kujifungua, sambamba na kuimarisha elimu ya afya ya uzazi kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Aidha, wadau wa maendeleo wametakiwa kuendelea kushirikiana na serikali na jamii katika kutoa elimu, huduma za ushauri nasaha na msaada wa kisaikolojia kwa wasichana waliokumbwa na changamoto hii.

Mimba za mapema ni changamoto inayogusa nyanja mbalimbali za maisha ya wasichana. Ili kukabiliana nayo, kunahitajika ushirikiano wa pamoja kati ya wazazi, walimu, viongozi wa dini, serikali na mashirika ya kijamii, ili kuhakikisha wasichana wanapata fursa ya kuendelea na masomo yao na hatimaye kuchangia maendeleo ya taifa.

Post a Comment

0 Comments