Ticker

6/recent/ticker-posts

Umuhimu Wa Kipimo Cha Ultrasound Kwa Mama Mjamzito


Berema Nassor,Zanzibar

Katika safari ya ujauzito, hakuna jambo muhimu kama kupata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu afya ya mama na mtoto aliyeko tumboni. Moja ya vipimo muhimu vinavyotumika kuhakikisha ujauzito salama ni kipimo cha ultrasound.

Kupitia teknolojia hiyo, madaktari wanaweza kumuona mtoto akiwa bado tumboni na kufuatilia ukuaji wake hatua kwa hatua jambo ambalo hapo awali lilitegemea kubahatisha au dalili zisizo sahihi.

Daktari Lwahyumba Joram Lwegasila, Daktari Dhamana wa Hospitali ya Wilaya ya Ijtimai, alisema kipimo cha ultrasound si kwa ajili ya kujua jinsia ya mtoto pekee kama wengi wanavyodhani, bali ni njia muhimu ya kugundua matatizo ya kiafya mapema.

“Ultrasound husaidia kubaini matatizo kama mimba ya nje ya mfuko wa uzazi, matatizo ya placenta, au upungufu wa maji tumboni. Hivyo husaidia kufanya maamuzi ya haraka yanayoweza kuokoa maisha ya mama na mtoto,” alisema Dkt. Lwegasila.

Alisema mama mjamzito anashauriwa kufanya kipimo hicho ndani ya miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito ili kufuatilia ukuaji wa mtoto. Aliongeza kuwa katika hospitali hiyo, wastani wa mama wajawazito 550 hadi 600 huhudhuria kliniki kila mwezi, na wengi wao hufanyiwa kipimo hicho kama sehemu ya ufuatiliaji wa afya ya ujauzito.

Tauhida Ali Said, mkazi wa Muembe Mchomeke, alisema kipimo cha ultrasound ni muhimu sana kwani kinaweza kugundua matatizo ambayo hayana dalili za wazi.

“Nilifanya kipimo cha ultrasound nikiwa na mimba ya miezi minane, ndipo ikagundulika mtoto alikuwa amefariki tumboni, wakati nilihisi niko salama kabisa. Madaktari walichukua hatua za haraka kunizalisha na kuniokoa maisha,” alisema Tauhida.

Aliwahimiza wanawake wenzake kufanya kipimo cha ultrasound katika miezi ya mwanzo na kipindi cha mwisho cha ujauzito, kwani hutoa amani ya moyo na taarifa sahihi kuhusu hali ya mtoto tumboni.

Kwa upande wake, Haji Khamis, mume wa Tauhida, alisema ni wajibu wa wanaume kuelewa umuhimu wa kipimo hicho na kushirikiana na wake zao katika hatua za ujauzito.

“Wakati mke wangu alipofanya kipimo cha mwisho ndipo iligundulika mtoto amefariki. Tukio hilo lilinifundisha umuhimu wa kipimo hiki, kwani kinaweza kuokoa maisha ya mama na mtoto,” alisema Haji.

Aliongeza kuwa kipimo cha ultrasound humsaidia mzazi kuwa na matumaini na utulivu wa moyo kwa kufahamu maendeleo ya mtoto na ujauzito kwa ujumla.

Kwa ujumla, kipimo cha ultrasound ni nguzo muhimu ya uzazi salama. Kupitia kipimo hiki, matatizo ya kiafya hugundulika mapema kabla hayajawa hatari, na hivyo kusaidia kulinda maisha ya mama na mtoto.

Ni wakati sasa jamii ielewe umuhimu wa kutumia kipimo cha ultrasound kama sehemu ya lazima ya safari ya ujauzito, ili kuhakikisha usalama na afya bora kwa mama na mtoto.

Post a Comment

0 Comments