Na Ahmed Abdulla:
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Taifa, Mohamed Ali Kawaida, ametoa kauli ya kumjibu aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Humphrey Polepole, kufuatia uamuzi wake wa kujiuzulu nafasi hiyo.
Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Kawaida amesema kuwa uamuzi wa Polepole kujiuzulu kwa kile alichokiita “kukosa amani ya moyo” haupaswi kuwa mizani ya kuamua uhalali wa uongozi wa Taifa.
"Hisia za mtu binafsi haziwezi kuwa mizani ya uhalali wa uongozi wa Taifa, kukosa amani ya moyo ni hali ya nafsi binafsi, si hoja ya kimfumo," alisema Kawaida.
Ameongeza kuwa, iwapo kila kiongozi angejiuzulu kwa sababu za maumivu ya nafsi, basi nchi haitakuwa na uongozi wa taasisi bali wa hisia, jambo ambalo si sahihi kwa mustakabali wa kitaifa.
Kauli hiyo imekuja saa chache baada ya Mhe. Polepole kutangaza hadharani kujiuzulu nafasi yake ya kidiplomasia nchini Cuba, akieleza sababu za kimaadili na dhamira ya ndani kama msingi wa uamuzi huo.
UVCCM kupitia alama zake za #SautiYaVijana na #MtotoWaMkweziNaMkulima imeashiria kuwa itaendelea kusimamia misingi ya taasisi na si hulka za watu binafsi.
0 Comments