Na Ahmed Abdulla, Zanzibar:
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
imepongeza juhudi za Jukwaa la Walimu Wanawake wa Kiafrika (FAWE) Zanzibar
katika mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji na ukatili kwa watoto.
Katika hafla iliyoandaliwa na Jukwaa Walimu
Wanawake Wa Kiafrika Upande Wa Zanzibar katika Ukumbi wa Walimu Kiembe Samaki,
Afisa Hifadhi ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Nyezuma Simai Issa, alisema kuwa serikali inatambua na kuthamini
mchango wa FAWE Zanzibar katika kutekeleza miradi inayolenga ustawi wa watoto.
"FAWE Zanzibar imekuwa nguzo
muhimu katika mapambano haya. Miradi yao inahakikisha watoto wanapata malezi
bora na haki zao zinaheshimiwa," alisema Nyezuma Simai Issa, akiongeza
kuwa ushirikiano kati ya serikali na FAWE ni muhimu katika kuhakikisha jamii
inapata elimu kuhusu haki za watoto na namna ya kuepuka vitendo vya ukatili.
Hafla hii ilikuwa sehemu ya
maadhimisho ya siku 16 za kupinga udhalilishaji na ukatili kwa watoto, ambapo
wanajamii, walimu, na viongozi wa serikali walishiriki.
Sabrina Omar Abdalla, ni Mjumbe wa
Bodi ya FAWE Zanzibar, aliwahimiza wazazi na walezi kuwa na jukumu muhimu
katika malezi bora ya watoto.
"Tunawaasa wazazi kuhakikisha
watoto wao wanalelewa katika mazingira salama. Malezi bora ni silaha muhimu
katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji na ukatili," alisema Sabrina.
Kwa upande mwingine, Afisa Programu
kutoka FAWE Zanzibar, Habiba Stumai Said, aliwakumbusha wanajamii kuwa
mapambano dhidi ya ukatili na udhalilishaji ni jukumu la kila mmoja.
"FAWE Zanzibar inaendelea
kushirikiana na jamii na wadau wengine katika kuhakikisha watoto wetu wanapata
malezi bora, salama na yenye heshima," alisema Habiba.
Katika maadhimisho hayo, FAWE
Zanzibar ilionyesha juhudi zake katika kutoa elimu kuhusu haki za watoto na
umuhimu wa malezi bora kwa kuwashirikisha watoto hao katika maonyesho
mbalimbali ikiwemo Ngonjera, picha pamoja na uandishi wa insha ambapo juhudi
hizi zinahakikisha kuwa watoto wanakua katika familia salama na zinazowalinda
dhidi ya vitendo vya udhalilishaji.
Hii ni sehemu ya hatua zinazoendelea
kuchukuliwa na serikali na mashirika ya kiraia kama FAWE Zanzibar katika
kutokomeza vitendo vya ukatili na kuhakikisha ustawi bora wa watoto.
0 Comments