Na Nafda Hindi
Wakulima
wanaojishughulisha na kilimo cha mboga
mboga, matunda na viungo kupitia MRADI
wa VIUNGO (AGRI-CONNECT) wamekabidhiwa vifaa vitakavyowasaidia
kuongeza nguvu katika uzalishaji wa bidhaa bora zitakazokidhi masoko.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo
iliofanyika katika jengo la Kificho Mwanakwerekwe Meneja Mkuu wa mradi huo
Simon Makobe alisema vifaa hivyo
vitatumika kusaidia kuongeza uzalishaji na kufikia malengo ya utekelezaji wa
mradi huo.
Alisema MRADI wa VIUNGO ulilenga mambo mbalimbali ikiwemo
kufungua fursa na kuongeza mnyororo wa thamani ya mazao hapa Zanzibar pamoja na
kupatiwa vifaa kwa lengo la kuwawezesha wakulima kuwa na nyenzo muhimu ili
kulima kilimo bora kitakachowasaidia kujikwamua kiuchumi,”alisema.
“Ugawaji wa vifaa
hivyo ni moja ya mikakati ya utekelezaji wa mradi huo pamoja na kutumia ujuzi
mulioupata juu ya matumizi ya teknolojia muliyojifunza kipindi chote cha
utekelezaji wake,” alisema Makobe.
Alifahamisha kuwa lengo la mradi huo ni kuleta mabadiliko
makubwa ya kiuchumi kwa wakulima na taifa hivyo kupitia hatua hiyo itasaidia
kufikia malengo hayo.
Sambamba na hayo aliwataka wakulima walionufaika na vifaa
hivyo kufuata maelekezo ya matumizi ya vifaa hivyo ili viweze kuleta tija
kwenye shughuli zao za kilimo.
Kwa upande wake Meneja tathmini na ufatiliaji wa mradi huo
Ali Abdalla Mbarouk alisema kukabidhiwa kwa vifaa hivyo itasaidia kuimarisha
ustawi wa shughuli zao kwa kuondosha changamoto zilizokuwa zikijitokeza baina
ya viongozi wa mradi huo na wakulima.
“Tulitegemea vifaa hivi vitolewe kipindi cha utekelezaji wa mradi kwa bahati
mbaya sasa mradi umemaliza ila tulikabiliwa na changamoto ya fedha
kidogo,”Mbarouk alisema.
Mratibu wa mradi huo kutoka Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji,
Maliasili na Mifugo Zanzibar Mashavu Said Sukwa alisema mradi huo pamoja na
changamoto za hapa na pale zilizojitokeza katika utekelezaji wake lakini
umeweza kuleta tija kwa wakulima kwa kupata elimu ya kuongeza uzalishaji na
kuzalisha bidhaa bora.
Alisema endapo wakulima hao wakishindwa kuvitumia vifaa
hivyo ni vyema kuvirudisha serikali na sio kufanya wanavotaka wao kwani kufanya
hivyo ni kwenda kinyume na malengo ya matumizi ya vifaa hivyo na
kutawasababisha kuingia katika matatizo.
“ Wakulima tunawaomba kuvitunza vifaa hivyo na kuvitumia kwa mujibu
wa matumizi yaliopangwa na si vinginevyo, mukenda kinyume na hayo kwa mujibu wa
Sheria mutafanya kosa na kuingia hatiani,” Mashavu alisema.
Kwa upande wa Ofisa
elimu kutoka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA)
Saumu Ramadhan Haji alisema watafatilia kwa karibu matumizi ya vifaa bivyo ili
kuondosha ubabaifu unaofanywa na baadhi ya wakulima kwa kuvitumia kinyume na
malengo ya vifaa wanavokabidhiwa.
Sheria ya ZAECA No 5, (2023), kifungu No 53 kinaeleza juu ya
matumizi mabaya ya Umma, pindipo utatumia vibaya mali ya Umma utaingia hatiani
na adhabu yake ni shilingi milioni 10 za Kitanzania, au utafungwa jela kifungo
cha miaka 5 au vyote kwapamoja.
Kwa upande wa wakulima hao walishukuru kupatiwa vifaa hivyo
na kuahidi kuvitumia kama walivyoelekezwa ili kwenda sambamba na malengo husika
ya mradi.
Walisema vifaa hivyo
vitasaidia kuongeza kasi ya uzalishaji wa kilimo chao kutokana na kikwazo kikubwa
kilikuwa ni kukosa nyenzo za kisasa za kuendeleza kwa shughuli zao hivyo
kupitia hatua hiyo wataweza kufikia malengo yao.
Jumla ya wakulima 31 walikabidhiwa vifaa mbalimbali vya kilimo na watatu (3) fedha taslimu ikiwemo
matenki ya maji, mashine za kuvutia maji, mipira ya kusambazia maji na vifaa
vingine kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za kilimo.
Mradi wa VIUNGO ulioanza mwaka 2020-2024 ni mradi wa miaka
minne (4) uliomaliza mda wake, uliwafikia wakulima wapatao elfu hamsini na
saba, mia tisa na sabiini na nne hapa Zanzibar kwa Wilaya tisa (9), tano (5)
Unguja na nne (4) Pemba ambao ulitekelezwa
kwa pamoja na TAMWA, People Developmend
Forum (PDF) na Community Forest in Pemba (CFP) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya.
0 Comments