Ticker

6/recent/ticker-posts

Salama -“Ndoto Zangu Ni Kuwa Mchezaji Wa Yanga Na Barcelona”.Na Najjat Omar,Zanzibar:

Ni Jumapili asubuhi kwake ni siku kama zilivyo siku nyengine nzuri ambazo zinaendelea kumpa matumaini ya kufikia ndoto zake na sasa ni 12:45 za asubuhi anatembea kuelekea barabarani kwenda kupanda daladala ya kuelekea Ziwani – Bomani kwenye uwanja  wa mazoezi.

Salama Mcha Khamis 24,mchezaji namba mbili au beki katika timu ya mpira wa miguu ya New Generation na pia ni mchezaji wa timu ya Worries ya mpira wa kikapu msichana mwenye ndoto kubwa ambazo anaendelea kuziwekea juhudi,uthubutu na maarifa ili kuzitimiza.

Taasis ya Wanawake kwenye michezo nchini  Marekani (Women’s Sport Foundation) inaonesha kwamba wasichana ambao wana umri wa miaka 14 huacha kuendelea kwa michezo ikiwa tofauti na wavulana kwenye umri huo huo kuendelea kwenye michezo.

Utafiti huu unaoenesha kuwa wasichana hao huacha kwa sababu ya kutokuwa na uthubutu,jamii kuwakatisha tamaa,kuwekeza zaidi katika masomo na hata familia kuona michezo ni kitu cha wavulana zaidi.

Kwa Salama ni tofauti maana baba yake Mcha Khamis alikuwa ni shabiki namba moja wa mtoto wake alipoanza kucheza mchezo wa mpira wa kikapu akiwa skuli ya msingi na hapo alimpa moyo ili aweze kuwa mchezaji kubwa.

“Baba yangu alipenda sana niwe mchezaji japo kwa sasa alishatangulia mbele za haki na sasa naendelea na ndoto zangu za kucheza na kuwa na thubutu kwenye kufikia malengo yangu “. Amesema Salama huku akiendelea kusimulia kwamba baada ya kumaliza kidato cha nne aliendelea na kucheza mpira wa kikapi hadi alipoanza kuona wachezaji wanawake wakifanya mazoezi ya mpira wa miguu nae kuhamia huko na kuendelea kuwa mchezaji rasmi wa timu yake ya New Generation.

Akiwa kwenye daladala amevalia baibui jeusi na mtandio wa bluu iliyokoza huwezi kabisa kudhani kuwa huyu ni mwanamichezo wa mpira wa miguu kwani kucheza kwake hakujabadilisha muonekano wa kuwa mwanaume “Mimi sio mwanaume ni mwanamke hivyo navaa nguo za kike na ni mwanamke na nikirudi nyumbani napika na kufanya kazi zote huku kwa sasa nafanya biashara ya kuuza juisi pale nyumbani kupata kipato “.Licha ya kuwa beki katika timu hio ila bado hajaanza kulipwa anacheza mpira kama kitu akipendacho.

Ali Juma Shaame ni Mkaazi Mkele ,Wilaya ya Mjini Magharib ni jirani wa karibu na Salama anasema kwa upande wake anamuona salama kama msichana mstaarab na kucheza mpira hakujawahi kumfanya jamii imuone muhuni au amepotea “Mimi sijawahi kumuona muhuni na huwa tunamuunga mkono timu yake ikicheza na tunaona fahari siku akiwa mchezaji kubwa kisha akatokea mtaani kwetu” Amemaliza kusema Ali.

Salama akiwa mtoto wa pekee kwa Mcha Khamis na Nyafu Mussa anaona anawajibu wa kupambani ndoto zake kwa nguvu na juhudi kubwa ,Mama yake Nyafu anasema hakuna kipingamizi wala maneno yatakayoweza kumkatisha tamaa binti yake kwenye jambo analolipenda “Sijawahi kumuambia kitu kibaya wala kumkatisha tamaa najua siku moja ndoto zake zitatimia na huwa mkumbusha kwenda mazoezi” Amesema Nyafu huku akiwa anatabasamu.

Licha ya kuwa bado mpira wa miguu na wa kikapu haujaanza kumlipa na kupata faida ila Salama naamini ndoto za kuichezea klabu kubwa ya Yanga Princess ipo pale na pia kuichezea timu ya Barcelona ya nchini Spain iitwayo Barca Femeni haiwezi kufa kirahisi “Ndoto zangu ni kuwa mchezaji wa Yanga Princess na kuichezea Barcelona kwa upande wa wanawake najua itatimia na bado naipambania”Amemaliza kwa kusema kuwa wito wake kwa serikali warudishe michezo skuli na wawatangaze wachezaji wa Zanzibar kwenye soko la dunia maana michezo na ajira na ni sehemu ya maisha ya wanawake na wasichana.

Riziki Aboubakar Islah ni mwalimu na kocha wa timu ya mpira wa miguu ya New Generation amesema wasichana wanaoshiriki mchezo wa mpira wa miguu wanakatishwa tamaa sana kwenye jamii huku wengi wakiona kuwa mchezo huo ni uhuni na wasichana wengine wameacha ila Salama anaendelea kupambania ndoto zake. “Salama ana ndoto kubwa ambazo zimetoka kwake na familia yake ndo maana nae ana nguvu ila bado jamii haimini kwenye michezo kwa wasichana” Amesema Riziki.

Chama cha Waandishi wa Habari wanawake Zanzibar – TAMWA -Z  kupitia Shiriki la Maendeleo ya Ujerumani wanatekeleza mradi wa masuala ya jinsia na michezo  huku lengo kubwa ikiwa ni kuipatia jamii elimu ya kuwaunga mkono na kuona wasichana na wanawake wana haki sawa ya kushiriki michezo kwa maendeleo.

Post a Comment

0 Comments