Na
Asia Mwalim, Zanzibar:
WANAWAKE na watoto wa kike wametakiwa kushiriki
michezo mbali mbali bila ya kukiuka mila na tamaduni za Kizanzibari ili
kufaidika na fursa za michezo ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake
Tanzania TAMWA-ZNZ, Dk. Mzuri Issa Ali alitoa wito huo wakati akifungua mafunzo
ya Jinsia na michezo kwa waandishi wa habari huko Tunguu wilaya ya Kati Unguja.
Alisema wakati umefika wanawake na watoto wa kike
kutumia fursa za michezo kuonesha uwezo wao na kufanikiwa kwenye maendeleo ya
kifedha kupitia michezo kulingana na utamaduni wao.
Aidha alisema bado mapungufu ni makubwa kwenye
michezo kutokana na wanawake kuachwa nyuma sambamba na kutozungumzwa sana
kwenye vyombo vya habari.
Dk. Mzuri alitaja miongoni mwa faida za michezo ni
pamoja na kuimarisha afya ya akili, mwili na kuongeza kipato jambo ambalo
wanawake wengi wanalikosa
Awali Afisa Programu wa mradi wa kuinua masuala ya
jinsia kwenye Michezo, Khairat Haji Ali, alisema wameamua kuandaa mafunzo ya
siku tano kwa waandishi wa habari ili kushajihisha michezo kwa wanawake na
watoto wa kike.
Aidha alisema, lengo la mradi huo ni kufikia dhana
ya usawa wa kijinsia kwenye michezo ikiwemo nafasi za kuongoza timu za mipira,
na michezo mengi ne kwa wanawake sambamba na kuoatikana ushiriki wao
kikamilifu.
Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, Mwaandishi
habari mkongwe Haura Shamte, alisema ni vyema jamii kubadilisha mifumo ya
malezi ili watoto wa kike wapate muda wa kushiriki vyema michezo kama ilivyo
watoto wa kiume.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walisema baadhi
ya changamoto zinazorudisha nyuma jitihada za wanawake na watoto wa kike
kushindwa kushiriki michezo ni kupewa majina mabaya, kuhusishwa na tabia chafu.
Mradi wa kukuza masuala ya jinsia kwenye michezo
unatekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA-ZNZ),
Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na Kituo cha Majadiliano
kwa Vijana (CYD) ambao umedhaminiwa na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa wa
Ujerumani (GIZ).
0 Comments