Ticker

6/recent/ticker-posts

CYD Yaanza Mpango Wa Kuwajenga Wanamichezo 6,500



Na Ahmed Abdulla, Zanzibar:

Serikali ya mapinduzi Zanzibar imesema itaendelea kushirikiana jumuiya na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kuinua sekta ya michezo nchini.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Vijana Zanzibar ndugu Shaib Ibrahim Muhamed wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya kuwajengea uwezo walimu wa michezo,wanafunzi pamoja na wananchi ya namna ya kufundisha michezo ya mpira wa wavu,mpira wa kikapu pamoja na mpira wa pete yanayoendelea katika uwanja wa Mao ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa kuwawezesha Vijana na Kukuza Usawa wa Jinsia Katika Michezo.

Alisema  mpango wa  kituo cha majadiliano kwa vijana (CYD) kutoa mafunzo hayo kutatoa fursa kwa washiriki hao kuongeza ujuzi katika michezo hali itakayowafanya kuwa bora katika kwenda kutoa elimu kwa wengine.

“unaweza kusoma taaluma nyingine na usipate kazi lakini ukijihusisha na michezo huwezi kukosa kazi” alisema

Aidha alisema Serikali inaendelea kuimarisha sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kukarabati na kujenga miundombinu ikiwemo viwanja vya michezo ili kuona wanamichezo wanacheza katika mazingira bora.

 “Pamoja kwamba tunashirikiana na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Ujerumani (GIZ) Katika viwanja hivyo lakini kuanzia bajeti ya mwaka mpya wa fedha unaoingia mtaona namna Serikali ilivyojipanga Uwanja wa Amaan ni Rasharasha tu” Alisisitiza

Mratibu kutoka kituo cha majadiliano kwa vijana (CYD) Ali Shaaban alisema michezo hiyo mitatu inakwenda kusaidia kuwaweka vijana pamoja katika michezo hiyo pamoja na kutumia michezo hiyo kuhamasisha jamii kuhusu amani, umoja na kupinga vitendo vya ukatili na unyanyasaji kwa wanawake na watoto.

“Sisi sote tunatoka katika jamii na sote ukiacha tukiwa maskulini tukiwa maeneo yoyote bado tunafanya michezo katika jamii zetu lakini michezo hii inahitajika iwe ya Amani pia kusitokee kwa namna yoyote ukatili na udhalilishaji” alisisitiza

Alisema “michezo ni miongoni mwa nyenzo za maendeleo tunapofanya michezo tunapata furaha na tunapata fursa za kujiingizia kipato”

Kwa upande wake afisa kutoka idara ya michezo na utamaduni , Wizara Ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Kassim Mohammed Juma alisema idara ya michezo na Utamaduni ya WEMA ndio yenye chimbuko la michezo yote hivyo uimarishwaji wa michezo hiyo kutaibua hamasa ya ushiriki kwa wanafunzi wengi.

“Michezo hii ndani ya maskuli yetu ilikuwa inaonekana kama iko chini kuliko mchezo wa mpira wa miguu lakini naamini baada ya mafunzo haya sasa michezo hii itakwenda kuchezwa ndani ya maskuli yetu” alisema

Khairat Haji ni Afisa Programu kutoka Chama Cha Waandishi Wa Habar Wanawake Tanzania upande wa Zanzibar TAMWA-ZNZ alisema “Nafasi yetu katika mradi huu ni kutumia vyombo vya habari ili kukuza usawa wa kijinsia na ujumuishi katika michezo”

Rufea Khamis Juma yeye ni meneja Mradi kutoka Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) alisema kwa upande wa wanaanda muongozo ambao ni ulinzi wa kisera,kikanuni na kisheria ambao utatumika katika michezo.

“kama tunavyofahamu katika michezo pia kuna udhalilishaji lakini kupitia huu muongojo tutajuwa aina ya udhalilishaji na ni vipi tutaweza kuripoti huu udhalilishaji” alisema

Mradi huo unafadhiliwa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Ujerumani (GIZ) chini ya program ya Michezo kwa maendeleo(S4D) ambapo Afisa ushauri wa masuala ya jinsia kwenye michezo kutoka kwenye Jumuiya Hiyo Hija Mohammed Ramadhan alisema mradi umelenga maeneo makuu matatu ambapo amelitaja eneo moja kuwa ni ujenzi wa viwanja ambapo jumla ya viwanja saba vitajengwa Unguja na Pemba.

Chini ya mradi huo, vijana na watoto wasiopungua 6,500 wa Zanzibar watashiriki katika shughuli za michezo na michezo kwa maendeleo (S4D) katika maskuli na mazingira ya jamii ili kukuza usawa wa kijinsia, uongozi, mshikamano wa kijamii.

 

Post a Comment

0 Comments