Kamati ya
wataalamu wa masuala ya habari Zanzibar (ZAMECO) imekuwa mstari wa mbele katika
jitihada za kufuatilia mchakato wa marekebisho ya sheria za habari ikiwemo
sheria ya Utangazaji No. 7 ya 1997, ambayo ilifanyiwa marekebisho na sheria No.
1 ya 2010.
Katika vikao
mbalimbali ZAMECO ilitoa mapendekezo kuhusu marekebisho ya sheria hio kwa lengo
la kupatikana sharia mpya na rafiki kwa waandishi wa habari na vyombo vya
habari nchini.
Aidha mnamo
tarehe 9/4/2024 ZAMECO wamefika katika afisi za Tume ya kurekebisha Sheria
Zanzibar iliyopo Vuga kwa ajili ya kufuatilia hatua iliyofikiwa baada ya
kupokea mapendekezo hayo mwezi wa Octoba mwaka 2023.
Mratibu wa Baraza
la Habari Tanzania (MCT) kwa upande wa Zanzibar Shifaa Said ameeleza kuwa hatua
hii ya ufuatiliaji imechukuliwa ili kuhakikisha kwamba mchakato wa kupata
rasimu ya sharia ya Utangazaji unakwenda vizuri na hatimae sheria mpya
itayokidhi vigezo vya kihabari ipatikane.
Kwa upande wake,
Salim Said, mwandishi wa habari mkongwe amesisitiza kwamba vyombo vya habari
havina nia mbaya na serikali, bali ni washirika muhimu katika kuleta maendeleo
kwa jamii hivyo jitihada za ZAMECO na wengine katika kuendeleza maboresho ya
sheria ya Utangazaji zinachukuliwa kama sehemu ya ushirikiano mzuri kati ya
vyombo vya habari na serikali.
“Vyombo vya
habari havina uadui na Serikali, sisi ni washirika wazuri na wenye lengo jema
kwa jamii na nchi kwa ujumla, kwa kuzingatia vyombo vya habari ni nguzo ya
maendeleo ya uchumi” Alisema Salim Said.
Katibu Tume ya
Kurekebisha Sheria ndugu Mussa Kombo Bakari aliwapongeza ZAMECO kwa jitihada
wanazozichukuwa kutafuta maendeleo ya tasnia ya habari na kubainisha kuwa
mapendekezo waliyowasilisha yamepokelewa na kufanyiwa kazi.
“Tume imekwisha
yapeleka mapendekezo hayo katika mamlaka husika na tunatumaini kwamba
mapendekezo hayo yatachukuliwa kwa uzito unaostahili ili hatimaye rasimu ya
mswaada wa sheria hio ipatikane , alieleza Katibu Mussa.
Nae mkurugenzi wa
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Dkt.
Mzuri Issa ametoa shukrani kwa katibu na wafanyakazi wote wa Tume kwa
ushirikiano wao katika mchakato huu wa kupata sheria mpya huku akisisitiza
umuhimu wa ushirikiano huu katika kuhakikisha upatikanaji wa sheria mpya kwa
maslahi ya Zanzibar na wazanzibari wote.
Ni takribani
miaka 20 sasa wadau wa maswala ya habari Zanzibar wamekua wakipambania
marekebisho ya sheria mbalimbali za habari ikiwemo Sheria ya usajili wa wakala
wa habari, magazeti na vitabu No. 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na
sheria No. 8 ya mwaka 1997 na Sheria ya Utangazaji No. 7 ya 1997 ambayo
ilifanyiwa marekebisho na Sheria No. 1 ya 2010 , ambapo Oktoba mwaka jana Tume
ya kurekebisha sheria Zanzibar ilipokea mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya
uatangazaji lengo ni kupata sheria huru iliyokua rafiki kwa tasnia ya habari na
jamii kwa ujumla.
0 Comments