Na Ahmed
Abdulla, Zanzibar
Mwanamke ni mlezi na mwanamke ni kiongozi.
Hii imedhihirika sio katika familia na
jamii tu bali hata ndani ya muhimili muhimu wa dola wa kutunga na kuzilinda
sheria za nchi – Baraza la Wawakilishi.
Uweledi huu wa viongozi ambao siku hizi,
tafauti na dhana potofu iliokuwepo zamani, umethibitishwa na Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduizi, Dk. Hussein Mwinyi.
Alisema’’Najivunia utendaji wa viongozi
wanawake katika serikali yangu, wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu,
manaibu makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wilaya, wakurugenzi wa taasisi na
mashirika ya umma’’.
Aliwapongeza wanawake aliowateua kushika
nyadhifa mbali mbali za uongozi kwa kazi nzuri wanayofanya ambayo alisema
anaridhika nayo.
Imani ya Dk. Mwinyi kwa wanawake kuonyesha
uongozi bora ndio iliopelekea wanawake kuongoza wizara sita kati ya 18.
Vile vile wapo manaibu mawazi wanawake
watatu kati ya saba.
Baraza hilo limefanyiwa mabadiliko mara
mbili tokea lilipoundwa mara ya kwanza na Rais Mwinyi na katika mabadiliko hayo
hakuna waziri mwanamke aliyewekwa pembeni.
Hapo awali Baraza lilikuwa na wizara 15 na
kati ya hizo wizara nne ziliongozwa na Wanawake. Nazo ni za Habari, Vijana na
Utamaduni ambayo iliongozwa na Tabia Mwita Maulid, Wizara ya Ardhi na
Maendeleo ya Makaazi iliyoongozwa na Riziki Pembe Juma, Wizara ya Utalii na
Mambo ya Kale inayoshikwa Lela Mohammed Mussa na Rahma Kassim Ali
aliteuliwa Waziri wa ujenzi.
Mabadiliko yaliyofanywa mara ya kwanza na
Dkt. Mwinyi ilikuwa ni faraja kwa wadau wanaopigania usawa wa kijinsia kwenye
demokrasia na uongozi kwani licha ya kwamba hakuna Waziri waziri mwanamke aliyewekwa
pembeni.
Baadaye pakaongezeka mawaziri wawili
wanawake ambao, Dk. Saada Mkuya Salum aliyeshika Wizaza ya Nchi, Offisi ya Rais
Fedha na Mipango na Harous Said Suleiman aliyeteuliwa Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.
Lakini jee wadau kupigania usawa wa
kijinsia kwenye nafasi za uongozi na demokrasia wanaupimaje utendaji wao kwenye
wizara walizopewa?
Maryam Ame amnbye ni Ofisa wa Mradi wa
Kuwawezesha wanawake kushika nafasi uongozi kutoka Chama cha waandishi wa
habari wanawake (TAMWA-Zanzibar) alisema kilichofanyika ni ishara ya matumaini
kwa wanawake wanaotaka kuingia kwenye uongozi.
“Wanawaona wenzao kuwa wanaweza na
wanazidi kuaminiwa” alisema.
Alieleza wakati umefika kwa wanawake
kujitokeza kushika nafasi za uongozi na kitu muhimu ni kuwa na sifa za uongozi
na sio maumbile ya mtu.
Aliihimiza jamii kuacha kumuangalia mtu
kwa jinsia yake bali elimu, uwezo na juhudi zake katika kazi.
“Inawezekana ikawa ana elimu ya
kawaida, lakini anaweza kuwa na uwezo mzuri wa kuongoza na kuzijua mbinu sahihi
za kutatua changamoto za watu wake, kufuatilia matatizo ya kijamii na kuyapatia
ufumbuzi”, aliongeza
Wanamichezo nao walizungumzia kufurahishwa
na mabadiliko yanayoonekana ya wanawake kupewa nafasi za uongozi.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Zanzibar (ZFF), Hussein Ahmada Vuai, alisema wanawame wamekuwa
wanatekeleza majukumu yao ya uongozi kikamilifu, iwe ni ya wizara,
taasisi ama Shirika.
Alisema hata wizara inayohusika na michezo
inaongozwa na wanawake kwenye nafasi za juu, akimaanisha Waziri na Katibu Mkuu
na kufurahishwa kwamba wanatekeleza vyema majukumu yao.
“Sisi kama ZFF tumekuwa tukitoa nafasi kwa
wanawake katika kamati mbalimbali na wengini ni watendaji wakuu kwenye kamati
hizo na wanafanya vizuri”, aliongeza.
Wanasiasa nao wamempongeza Dkt. Mwinyi kwa
kuwaamini mawaziri wanawake.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa
CCM (UWT) wa Wilaya ya Amani Kichama, Francisca Camilius Climent, alisema
wanawake wa CCM wamefarijika kuona Rais Mwinyi anavyowaamini wanawake.
“Hii kwetu ni faraja na inatutia nguvu
kuona wanawake sasa tunashiriki kwenye vyombo vya maamuzi ‘’,
alidokeza.
Alisema hatua hii itawaongezea hamasa
wanawake kuwania nafasi za uongozi na wanaopewa dhamana kufanya kazi kwa bidii.
Aliwataka wanawake waliopewa dhamana
zanyadhifa mbalimbali kufanya kazi kama walivyotarajiwa ili taifa lipate
maendeleo.
Mnamo tarehe 27 Januari, mwaka huu, Rais Mwinyi
alifanya mabadiliko ya baraza la mawaziri yaliyohusisha kuwateua
wanawake wawili kushika nafasi za Manaibu waziri.
Nao ni Salha Mohamed Mwinjuma kuwa
Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi na Zawadi
Amour Nassor kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Maji,Nishati na Madini.
Zanlight Blog ilipomtaka Salha Mohammed
Mwinjuma na kuzungumzia uteuzi wake alisema anaamini uteuzi wa wanawake zaidi
kushika nafasi za uongozi unatokana na kuthibitika kwamba wanao uwezo na uweledi
wa kuongoza.
Aliwataka wanawake wengine wajifunze
kutoka kwa viongozi waliowatangulia na mfano mzuri ni wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano, Mama Samia Suluhu Hassan na wanawake wengine waliowahi kuwa mawaziri
au kushika nyadhifa nyengine za juu za uongozi.
Bahati Chumu Haji ambaye ni Naibu Katibu
Mkuu wa Baraza la Wanawake la Chadema alisema imani ya Rais Mwinyi kwa wanawake
ni hatua muhimu ya maendeleo.
“Hii kwa upande wetu wanawake inatutia
moyo na kutufanya tujione ni watu muhimu na kuwa na ujasiri wa kufanya mambo
muhimu kwenye nchi yetu” alisema Bi Bahati
Aliwanasihi wale waliopewa dhamana ya
kuongoza taasisi mbalimbali kufanya kazi kwa bidii ili kuwabadilisha mtazamo
wale wanaodhani mwanamke hawezi kuongoza.
Kwa kweli sura ya uongozi Zanzibar
inabadilika na kutoa matumaini ya kupatikana taswira inayoonyesha nafasi za
uongozi ni sawa kwa wanaume na wanawake, ijapokuwa bado uwiano sio mzuri sana.
Hata hivyo hataua iliyopatikana katika
miaka mitatu ya utawala wa Rais Mwinyi inatoa ishara kwamba safari ya kuelekea
usawa wa uongozi unaopigiwa kelele inakwenda vizuri.
Lililo muhimu ni kwa wale waliokuwa na
mashaka juu ya uwezo wa mwanamke kuongoza kubadilika na kuukubali kweli kwamba
mwanamke mbali ya kuwa mlezi mzuri pia ni kiongozi mzuri.
0 Comments