Ticker

6/recent/ticker-posts

Wasaidizi Wa Sheria Waombwa Kutovunjika Moyo



Na Nafda Hindi, Zanzibar

Naibu Mwanasheria Mkuu Zanzibar Shaaban Ramadhan Abdalla amewataka wasaidizi wa sheria  kuendelea kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi kwa lengo la upatikanaji wa haki.

Akifunguwa Jukwaa la tatu la mwaka la msaada wa kisheria huko Chuo cha Utalii Maruhubi kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu Dr Mwinyi Talib amesema Serikali inatambuwa na kuthamini mchango wa wadau hao kuhakikisha jamii isiyo na uwezo inafikiwa na kupata haki zao.

Amesema  wasaidizi wa sheria wanafanya kazi kubwa ya kujitolea na kutoa huduma hiyo katika ngazi ya jamii  bila ya malipo  ili jamii ipate  haki zao bila ya ubaguzi wowote.

Aidha ametoa wito kwa wasaidizi wa sheria kutofanya kazi kimazowea na badala yake kubadilika katika utendaji wa majukumu yao hatimae kuleta tija katika jamii na kuendeleza juhudi za Serikali za kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa jamii ya Kizanzibari.

“Ili mubadilike ni lazima mujifunze na kuongeza ujuzi Zaidi na itapendeza kubadilishana uzoefu na nchi nyengine na ikiwezekana katika jukwaa lijalo mwakani tuone nchi za Afrika Mashariki wanahudhuria kwa lengo la kubadilishana uzoefu,”  Mwanasheria Mkuu Zanzibar, Dk Mwinyi Talib.

Mapema Mkurugenzi kutoka Idara ya Katiba na msaada wa Kisheria Zanzibar Hanifa Ramadhan Said amesema lengo la Jukwaa hilo ni kukuza ubunifu, kuimarisha ufanisi na uweledi kwa watendaji wanaotowa huduma hiyo.

“ Tunajipanga na Tunatarajia jukwaa lijalo mwakani kushirikisha nchi za Uganda, Kenya na Afrika Mashariki kwa ujumla ili kubadilishana uzoefu kwa watendaji wetu,”  Hanifa Ramadhan Mkurugenzi Idara ya Katiba na msaada wa kisheria.

Nae Mwakilishi wa Taasisi ya  Leagal Service Facility (LSF) Wakili Alphonce Gura amesema Zanzibar imekuwa kituo cha kujifunzia utowaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa Afika Mashariki.

“ Kwa ujasiri mkubwa tunaweza kusema kuwa Zanzibar imejidhihirisha kuwa nchi bora kwa huduma za utowaji wa msaada wa kisheria kwa Afrika ya Mashariki kwa kuona maendeleo yanayopatikana hasa katika upatikanaji wa haki,” Wakili Alphonce Gura kutoka  Legal Service Facility.  

Kongamano hilo la siku mbili limewashirikisha washirki kutoka Unguja, Pemba na Dar es Salaam likiwa na kauli mbiu Kuimarisha huduma za msaada wa kisheria zenye ubora na zinazozingatia matokeo.     


Post a Comment

0 Comments