Na Nafda Hindi:
Mkurugenzi
wa Chama cha Waandishi wahabari Wanawake Tanzania Zanzibar Dk Mzuri
Issa Ali amewaomba vijana na wanawake kuzidisha bidii katika kilimo kwa
lengo la kujikwamua na umaskini na kuleta maendeleo katika Taifa.
Akitembelea
mabanda ya maonyesho yanayomilikiwa na mradi wa VIUNGO katika siku ya wakulima
Zanzibar (nane nane) huko Dole amesema kilimo ni sekta moja wapo iliodharauliwa
kwa miaka mingi na sasa inaonekana umuhimu wake kwa kuongeza ajira kwa vijana
pamoja na wanawake.
Aidha amesema
wanawake awali wakitumia fursa ya kilimo kwa ajili ya chakula cha nyumbani
pekee kwa sasa hali imebadilika na kutumia fursa hiyo kama njia moja ya
kujiongezea kipato kwa ajili ya biashara.
Nae mwenye
dhamana ya masoko katika mradi wa VIUNGO Zulfa M’bwana amesema lengo kuu la
mradi huo ni kuongeza thamani ya vidhaa za mboga mboga, matunda na viungo
pamoja na kuwaunganisha wanunuzi,wasafirishaji,wahifadhi na wakulima kwa
urahisi jambo ambalo limesaidia kupata soko la uhakika ndani na nje ya nchi
kama vile falme za Kiarabu katika nchi ya Oman na bara Ulaya nchini Ujerumani.
Mfanyakazi kutoka
mradi wa VIUNGO Ali Said Juma amesema wameshiriki katika maonyesho hayo
kwa lengo la kutoa Elimu kwa wakulima kwa kulima kilimo bora kinachohimili
mabadiliko ya Tabia ya nchi kulingana na mazingira ya nchi husika.
Mkulima ambae ni
mnufaika wa mradi wa VIUNGO Aviwa Ali Songoro ameanza na kilimo cha vanilla na
hatimae kuchanganya na kilimo cha migomba kwa muda wa miaka mitatu ambapo kwa
sasa ana miche ya zao la vanilla isiopungua elfu moja (1000) na miche ya
migomba isiopunguwa elfu tatu katika shamba lenye ukubwa wa ekari tatu.
Mkulima Aviwa
ananufaika na mradi huo kwa kujikimu kimaisha pamoja na familia yake kwa
kusomesha watoto na anawasihi wanawake na vijana watumie fursa ya kilimo
kibiashara kwa lengo la kupiga hatua kimaendeleo na kubadilisha maisha yao.
Mradi wa VIUNGO
unatekelezwa na Taasisi Tatu ambazo ni TAMWA Zanzibar. PEOPLE DEVELOPMENT
FORUM,(PDF) COMMUNITY FOREST PEMBA (CFP) Unaosimamiwa na Wizara ya
Kilimo,Umwagiliaji na Mifugo chini ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na
kufadhiliwa na Umoja wa Ulaya(Uropean Union).
0 Comments