Ticker

6/recent/ticker-posts

TAMWA-Zanzibar Yasisitiza Uwepo Sera Ya Jinsia Kwenye Vyombo Vya Habari

 


Na Nafda Hindi


Chama cha waandishi wa Habari wanawake Tanzania TAMWA Zanzibar kimesisitiza kuwepo sera ya jinsia katika vyombo vya habari  ili kusaidia kuweka mazingira salama na kuondosha unyanyasaji katika maeneo ya kazi.

Mkurugenzi wa chama hicho Dk Mzuri Issa amesema hayo katika mkutano wa maboresho ya sera  ya jinsia kwa vyombo vya Habari uliowakutanisha wadau mbalimbali uliofanyika huko Tunguu wilaya ya kati Unguja..

Dk Mzuri amesema Zanzibar ni miongoni mwa nchi zilizojikita kuleta usawa wa kijinsia katika Nyanja mbambali za kiuchumi, kijamii na kisiasa hivyo kuwepo kwa sera hiyo itakuwa chachu ya kufikia malengo ya kuwainua wanawake katika uongozi na kufikia asilimia 50 kwa 50.

Alisema licha ya kuridhia mikataba mabalimbali ya kikanda na mataifa ikiwemo, AU , nchi za kusini mwa afrika SADEC, SEDAU muongozo wa mwaka 1979 wa kuondosha aina zote za ubaguzi wa jinsia lakini bado kuna maeneo yanahitaji kuwekewa mkazo Zaidi ili kuona malengo hayo yanafanikiwa.

“ Vyombo vya Habari vina jukumu kuhakikisha kazi zao zinaleta usawa wa kijinsia na kuondosha aina zote za ubaguzi na kulinda haki zote za binaadamu”, Dk Mzuri amesema.

Akiwasilisha  mambo muhimu yaliyomo kwenye sera ya jinsia kwa vyombo vya Habari Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Idara ya Mawasiliano na taaluma ya Habari, Imane Duwe, amesema uwepo wa sera hiyo katika vyombo vya Habari itasaidia kutengeneza mazingira salama na yaliyobora ili kuondoa mwanya wa unyanyasaji.

Sambamba na hayo alisema sera hiyo itasaidia kutoa miongozo na kutanua wigo katika kupaza sauti za wanawake kupitia shughuli mbalimbali wanazozifanya ikiwemo uzalishaji mali na shughuli nyengine ili kuondosha mawazo mgando ya kumkandamiza mwanamke.

“ Hatua hiyo itasaidia kuwa na utaratibu thabiti wa kuripoti masuala yote ya jinsia na kuviwezesha vyombo vya Habari kuweka usawa wa kuripoti masuala mbalimbali yanayohusu jinsia zote,” amesema Imane.

Nae Shifaa Said kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa upande wa Zanzibar amesema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Baraza la Habari Tanzania (2019) uligundua kwamba katika vyombo vyote vya habari Tanzania hakuna hata chombo kimoja chenye sera ya jinsia.

Ali Mkubwa Zubeir kutoka radio Al-Noor alisema madawati hayo na sera ya jinsia ni umuhimu katika utendaji wa kazi zao na endapo wataanzasha watawasaidia wananchi katika mambo mbali mbali ikiwemo usawa wa kjinsia  na kupunguza vitendo vya udhalilishaji hivyo ameiomba TAMWA Zanzibar kushirikiana vyema na vyombo hivyo ili kufanikisha malengo hayo

“Kuwepo kwa madawati na sera ya jinsia katika vyombo vya habari ni vyema kutolewa elimu zaidi kwa viongozi  na wamiliki wa vyombo vya habari ili kuona umuhimu wa kuwepo usawa katika vyombo vyao,”amesema.

Kwa mujibu wa tamwa Zanzibar Jumla ya vyombo vya habari 11 ikiwemo magazeti, redio na televisheni vilipatiwa mafunzo ya namna ya  kuanzisha madawati na sera ya jinsia kati ya vyombo hivyo 5 vinmeshaanzisha madawati ya jinsia.

Post a Comment

0 Comments