Ticker

6/recent/ticker-posts

Wadau Waitaka Jamii Kuripoti Matukio Ya Utelekezaji Wa Familia



Imeandikwa Na: Nafda Hindi


Licha ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kukemea na kupinga vitendo vya udhalilishaji lakini bado vinaonekana kuchukuwa sura mpya huku ikionekana baadhi ya wanaume wakitelekeza familia zao.

Hayo yamejiri wakati  mama mmoja ambae hakupendelea kutajwa jina lake  akilalamika kuachiwa ulezi wa watoto peke yake bila ya huduma kutoka kwa baba mzazi wa watoto hao.

Zanlight Blog  imezungumza na mama huyo alitelekezwa na watoto ambapo alisema kutokana na ugumu wa maisha yeye hapati huduma stahiki kutoka kwa baba wa watoto hivyo hawezi kumudu gharama za kuwahudumia watoto hao.

“Mimi nimeanza nae maisha mume wangu na yalikuwa ya tabu, tumeanza nyumba ya udongo hana mbele wala nyuma, leo kapata uwezo ananitelekeza na watoto, hapiti wala haulizi kila kitu mwenyewe,” alisema Mama huyo.

Shadida Omar ni mwanasheria kutoka chama cha wanasheria wanawake ZAFELA alisema ni kosa kisheria kumtelekeza mtoto na pia ameiasa jamii kuripoti na kukimbila kwenye vyombo vya sheria endapo itatokezea hali hiyo.

 “Sheria no 6 (2004)imeelezea kipengele cha malezi,(108)kifungu (1) kimeeleza makosa ya jinai ambapo pia kumtelekeza mtoto nalo pia ni kosa kisheria, ambapo kifungu hicho kimetowa adhabu kwa mzazi/mlezi kumnyima mtoto huduma za lazima awajibishwe,” alisema Shadida.

Nae mwananchi kutoka Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja alisema kwa sasa Zanzibar inaonekana ni jambo la kawaida kwa baadhi ya wanaume kutelekeza familia zao ambapo wanakwenda kinyume na sheria.

“Kwa sasa baadhi ya wanaume kwa Zanzibar kutelekeza familia wanaona kama mchezo ,wanazaa na wanawake halafu wanamuacha mke bila kujali na kumtupia mzigo wa watoto bila huduma yoyote, hivyo naomba Serikali ifatilie suala hili kwa kina na sheria ichukuwe mkondo wake ili iwe funzo kwa wengine”, alisema mwananchi.


Mapema Mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto Mkoa wa Kusini Unguja Inspekta Sadiki Ali Sultan alisema kutelekeza familia ni kosa la jinai na endapo watabainika watapelekwa Mahakamani na sheria kuchukuwa mkondo wake na ametowa wito kwa jamii kuripoti kesi hizo kwenye vituo vya polisi ama Mahakama ya Kadhi.

 “Natowa wito kwa jamii iwe na muamko endapo itatokea mwanamke katelekezwa na watoto basi achukuwe hatua kuripoti kituo cha polisi ama wafike katika kituo cha dawati na jinsia ili mtuhumiwa kuchukuliwa hatua za kisheria”,alisema Inspekta wa polisi.

Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) Sheikh Ali Amour Abdalla yeye alisema katika sheria za dini ya Kiislam inasema baba anajukumu la kuwahudumia watoto wake akiwa ndani ya ndoa au hata kama ameshamuacha mke na asipofanya hivyo anabeba jukumu mpaka mbele ya Mungu na atalipwa kwa mujibu wa imani ya kiislam.

“Mwanamme ana wajibu kushughulikia familia na ukenda kinyume na maamrisho haya uanabebeba jukumu kwa Allah hadi siku ya malipo, wajibu huo ukiwa ndani ya ndoa au nje ya ndoa hatimae watoto hukosa mapenzi kwa kulelewa na mzazi mmoja na mwisho watoto watakutelekeza pindipo ukifikia uzeeni kwa mujibu wa hadithi ya bwana Mtume Muhammad (S.A. W)” Alisema Sheikh huyo.

 

                                                                 


Post a Comment

0 Comments