Na Ahmed Abdulla Othman
MKURUGENZI wa Chama cha Waandishi wa habari Tanzania
(TAMWA) Zanzibar Dk Mzuri Issa amesema kuwa licha ya adhabu kubwa inayotolewa
kwa washtakiwa wa kesi za udhalilishaji lakini anashangaa kuwa matukio ya
udhalilishaji yanaongezeka Zanzibar.
Aliyasema hayo wakati akifungua mkutano wa wadau wa
masuala ya udhalilishaji uliolenga kujadili changamoto, mafanikio na nini
kifanyike kutokomeza vitendo vya udhalilishaji.
Alisema kuwa hukumu za kesi za udhalilishaji
zinazotolewa na Mahakama zinaridhisha
ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Alieleza anashangaa kuona matukio ya udhalilishaji
yanaongezeka licha ya kwamba adhabu kubwa zinatolewa kwa washtakiwa wa makosa
hayo.
"Hukumu zinazotolewa kwa washtakiwa wa kesi za
udhalilishaji zinaridhisha tunashuhudia hukumu zinatolewa miaka 30 hadi 80
lakini sijui kwa nini matukio yanaongezeka"alisema Dk Mzuri.
Alieleza kuwa matukio ya udhalilishaji ikiwemo ubakaji
yamekuwa yakifanywa na watu wa karibu katika familia ikiwemo Baba kubaka watoto
wake.
Dk Mzuri alisema lazima kuwe na mikakati mipya ya ulinzi
mkubwa kwa wanawake na watoto ili kutofanyiwa vitendo vya udhalilishaji.
Akieleza changamoto katika kushughulikia kesi za
udhalilishaji wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka Hamad
Kombo, alisema mashahidi bado ni kikwazo katika kutoa ushahidi mahakamani hasa
kwa wahanga wenyewe wa kike wenye umri kati ya miaka 14 hadi 17 ambao
wamefanyiwa kitendo cha ubakaji.
Alisema wahanga hao wa udhalilishaji huwa wanawalinda
wadhalilishaji kwa kutoa ushahidi wa uongo mahakamani au kukataa kutoa ushahidi
kwa sababu huwa ni wapenzi.
Naye Ispekta wa Polisi kitoka dawati la jinsia Mkoa wa
Kaskazini Pemba Fakihi Yussuf alisema wanafanya kazi katika mazingira magumu
sana kufanya upelelezi wa kesi za udhalilishaji.
"Mimi binafsi natoa fedha zangu mfukoni kuwafuata
mashahidi wa kesi za udhalilishaji wakati ninapofanya upelelezi wa kesi
hizi......Polisi tunafanya kazi katika mazingira magumu sana katika mapambano
ya kesi za udhalilishaji"alisema.
Akieleza mafanikio katika mapambano ya kesi hizo alisema
kesi zinafikishwa mahakamani kwa haraka na kesi 15 zimetolewa hukumu kwa mwaka
jana kwa Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Kesi 168 za udhalilishaji zimeripotiwa Polisi katika
Mkoa wa Kaskazini Pemba na kesi 144 zimeripotiwa Mkoa wa Kusini Unguja ambapo
asilimia 20 ya watuhumiwa wa kesi hizo wamekimbia na bado hawajapatikana.
0 Comments