Ticker

6/recent/ticker-posts

KARAKANA UNITED BINGWA MPYA MIMI NA WEWE MAPINDUZI NAGE CUP, KARAKANA RENGERS WALIA KUFANYIWA HUJUMA YA KUZUILIWA WACHEZAJI WAO.

 

Mashindano ya mimi na wewe mapinduzi nage cup yamefikia tamati kwa mchezo wa fainali uliowakutanisha mahasimu wawili wa mji wa karakara kwa maana ya timu ya Karakana United  wakipambana na Karakana Rengers.

Katika mchezo huo wa vuta nikuvute ulishuhudiwa kwa timu ya Karakana United kuongoza kwa mabao 20 huku timu ya Karakana Rengers ikipata mabao 9 hivyo kuifanya timu ya karakana united kuwa bingwa wa michuano hiyo kwa mwaka huu wa 2021.

Awali Waziri Wa Habari Vijana Utamaduni Na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita alipata nafasi ya kuzungumza na wanamichezo pamoja na wadau wa mchezo huo ambapo aliwataka kuwa na mashirikiano na kutokuwa na uhasama wa kimichezo kwani kufanya hivyo kutapelekea maendeleo ya mchezo huo pamoja na chama cha mchezo huo kwa ujumla.

“Michezo ituunganishe na kutuongezea mshikamano na upendo hususan michezo hii tunayoicheza kwa ajili ya kudumisha kumbukumbu ya mapinduzi” alisema waziri huyo

 

Aidha  aliahidi kuwa atahakikisha chama cha mchezo wa nage za Zanzibar kinapatiwa usajili kwa gharama inayoendana na udogo wake ili kuona chama hicho kinakuwepo kwa mujibu wa taratibu na sharia zilizowekwa.

“Naahidi usajili utapatikana kwa wakati kabisa na nitamuelekeza mwanasheria wangu atalichukuwa na kulifanyia kazi” alisema Mhe Tabia

Sambamba na hayo ameahidi kusaidia chakula cha siku zote watakazokaa katika kambi huko Kinondoni Jijini Dar es salam ikiwa ni hatua za kubadilishana mawazo kwa wanamichezo wa mchezo huo wa visiwani Zanzibar na wenzao wa Dar er salam.

“Mhe. Mbunge ameahidi kugharamia gharama za usafiri kwa wale watakaobahatika kwenda Dar es salam na mimi waziri wenu nitadhamini chakula cha siku zote mtakazokuwa kule Kinondoni” aliongezea waziri huyo

Katika hatua hiyo alimuagiza Raisi wa chama cha mchezo wa nage Zanzibar kuhakikisha usalama wa wanamichezo hao wakiwa katika safari na kambi yao huko Jijini Dar es salam ambapo aliahidi kufuatilia kwa karibu safari hio ili kuona wanamichezo hao wanakuwa salama katika safari yao hiyo.

“Raisi wa chama cha nage una jukumu kubwa kuhakikisha usalama wa mabinti wetu unakuwa wa kutosha nitafuatilia kwa karibu mwenendo wa safari hiyo” alisisitiza mhe. Tabia

Kwa upande wake Raisi wa chama cha mchezo wa nage Zanzibar Haji Kaka alisema watahsakikisha chama kinasimamia mchezo huo ili kuona unakuwa ni sehemu ya ajira kwa wanamichezo wa mchezo huo.

“Tutahakikisha tunausimamia mchezo huu ili iwe ni sehemu ya ajira kwa wanamichezo wetu” alisema Haji Kaka

Ashura kudura mohammed ni nahodha wa timu ya  Karakana United alisema siri kuu ya ushindi wao ni kujituma katika kufanya mazoezi pamoja na kutekeleza maagizo ya kocha wao ambapo amewataka wanajamii kuachana na dhana ya kuwa mcheozo wa nage ni mchezo wa kihuni.

“Tumefanya mazoezi kwa bidii pia tumezifuata mbinu zote za mwalimu na ndio mana tumepata matokeo haya” alisema Nahodha huyo

Kwa upande wa mchezaji wa timu ya Karakana Rengers Salma Othman Omar alisema kupoteza kwa mchezo wao huo wa fainali kumesababishwa na kuzuiliwa kwa baadhi ya wachezaji wao tegemezi hivyo imewapelekea kutoka katika ubora wao na kupoteza mchezo huo kwa mabao mengi.

“wachezaji temecheza nao katika michezo iliyopita ila katika fainali wanazuiliwa kwa hili hatujatendewa haki” alisema Salma Othman

Mashindano hayo hufanyika kila mwaka ikiwa ni katika harakati za kudumisha historia ya Mapinduzi matukufu ya 1964.

 

 

 

wachezaji wa timu ya Karakana United

Post a Comment

0 Comments