MKUU wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe Idrissa Kitwana Mustafa
amewataka wananchi na wafanya biashara pembezoni mwa barabara itokayo wa uwanja
wa Ndege hadi Kilimani kutoa mashirikiano kwa wajenzi wakati wa matengenezo ya
barabara hiyo yatakapoanza.
Wito huo ameutoa wakati alipofanya ziara yake pamoja na
watendaji wa taasisi mbali mbali huko maeneo ya Kiembesamaki ili kupanga namana
ya kuanza kufanya kazi hiyo.
Amesema matengenezo ya misingi ya maji mvua na sehemu za
watembea kwa miguu pembezoni mwa barabara hiyo yataanza mapema wiki hii ikiwa
ni utekelezaji wa agizo alilolitoa Rais wa Zanzibar Dkt Hussen Ali Mwinyi
wakati alipofanya ziara yake ya kukagua miradi ya ZUSP wiki iliyopita na
kuagiza ndani ya miezi mitatu kuona mabadiliko barabara itokayo uwanaja wa
ndege hadi mnazi mmoja.
“Mhe Rais alipofanya ziara katika eneo hili alitoa
maagizo na maelekezo ya kuona mabadiliko ya haraka katika barabara hii na
madelekezo yaliyotolewa kwetu sisi ni kazi,hivyo nikiwa kiongozi wa Mkoa huu
nitahakikisha kazi hii inafanyika kwa haraka na wakati’alisema Mkuu wa Mkoa.
Aidha mkuu wa Mkoa ameziagiza taasisi zote ikiwemo
ZUSP,ZAWA,Mawasiliano,Mamlaka ya Viwanja vya ndege na Manispaa kuanza kazi hiyo
mara moja na kuikamilisha ndani ya miezi miwili kwa kiwango kinachotakiwa ili
kuweka manzari ya maeneo hayo vizuri.
Hata hivyo ameeleza kufarajika na namna wafanyabiashara
na wananchi wa maeneo hayo walivyo kuwa tayari kuunga mkono juhudi na hatua za
serikali za kufanya matengenezo katika barabara ya uwanaja wa ndege.
Katika hatua nyengine mkuu wa Mkoa amewataka wafanya
biashara kuhakikisha maeneo ya nje ya maduka yao yanakuwa safi na wasiweke
bidhaa ili kuacha nafasi hizo kutumika na wananchi wanaotembea kwa miguu.
Nae mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Magharibi B Ali
Abdalla Natepe amesema iwapo taasisi hizo zitaendelea kushirikiana kwa pamoja
upo uwezekano mkubwa wa kufanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa huku
akiwasisistiza wananchi kuacha kuweka taka chini na badala yake kutumia vifaa
maalumu vya kutilia taka.
Amesema manispaa yake imejipanga kugawa vifaa
maalumu vya kutilia taka katika maduka yote yaliopo mbele ya barabara kuu ndani
ya manispaa hiyo.
Mapema mwakilishi wa mamlaka ya viwanja vya ndege na
wizara ya mawasiliano wamesema wataanza kazi hiyo kwa panmoja ili kuona maeneo
yote wananyoyatengeneza yanakuwa na muonekano mmoja na wenye kuvutia.
0 Comments