Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Innocent Bashungwa amesema Wizara hiyo ni
msingi wa kulinda historia, mila na desturi za nchi pamoja na kuhakikisha sekta
zake zinachangia katika kukuza pato la taifa, ambapo amesisitiza kuwa sekta ya
Michezo ina wajibu wa kuhakikisha inafanya vizuri ndani na nje ya nchi hivyo
amewataka wataalamu wa Sekta hizo kuongeza ubunifu katika kutekeleza majukumu
yao.
Mhe.Bashungwa
ameyasema hayo leo Desemba 10,2020 katika kikao na Menejimenti ambayo
ilijumuisha Wakuu wa Idara, Vitengo na Taasisi zilizo chini ya wizara
hiyo ambapo amesema ni jukumu la kila Idara na Taasisi kuwa na mtazamo chanya
na kubuni njia mbalimbali za kitaalamu zitakazosaidia kutatua changamoto
zilizopo katika sekta zao lengo likiwa ni kukidhi maatarajio ya kuundwa kwa
Wizara hiyo.
"Ni lazima
tuangalie namna ya kuchangia katika pato la taifa, pamoja na kuboresha
makusanyo ya Mirabaha, Sekta ya Michezo leteni suluhisho la changamoto ambazo
nyinyi wataalamu mnaona zitasaidia kuboresha sekta hii" alisema Bashungwa.
Mhe.Bashungwa
ameongeza kuwa mkakati wa Serikali ni kuhakikisha Shirika la Utangazaji
Tanzania (TBC) linasikika nchi nzima, hivyo fedha ambazo zimetengwa kwa ajili
ya kuimarisha usikivu zitumike ipasavyo, huku akisisitiza Chama cha Hakimiliki
Tanzania (COSOTA) kuendelea kutatua kero za wadau wake ili wanufaike na kazi
zao.
Naye Naibu Waziri wa
wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega amewaagiza wajumbe hao wa menejiment ya Wizara
na Wakuu wa Taasisi kuangalia Sera zote zilizopo kama zinaendana na wakati
uliopo na zinakidhi matakwa ya wadau wao na nchi katika kuendeleza sekta hizo.
Mhe.Ulega amesisitiza
viongozi hao kuwa katika kulinda na kuendeleza maadili ya Kitanzania, mila na
desturi za jamii ni vyema kuwatumia viongozi wa dini ambao wanahudumia
jamii kiimani, kimaadili na kielimu, Huku akihimiza Sekta ya michezo kuwa ina
wajibu wa kutumia michezo ya UMITASHUMTA na UMISETA kuibua vipaji
vitavyosaidia kuzalisha wanamichezo.
0 Comments