Ticker

6/recent/ticker-posts

Dkt. Mwinyi awaapisha wakuu wa mikoa wapya asisitiza uwajibikazi aahidi kutumbua kwa asiyewajibika ipaswavyo.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka Wakuu wa Mikoa wapya wa Zanzibar kuwa na utaratibu maalum unaotambulika wa kusikiliza kero za wananchi pamoja na kuzitafutia ufumbuzi.

Dk. Mwinyi ametoa ushauri huo leo Ikulu jijini Zanzibar katika hafla ya kuwaapisha Wakuu wa Mikoa wapya, watakaohudumu katika Mikoa mitano ya Zanzibar.
Walioapishwa ni Ayoub Mohamed Mahamoud Mkoa Kaskazini Unguja, Rashid Hadid Rashid (Kusini Unguja), Idrissa Kitwana Mustafa (Mjini Magharibi), Salama Mbarouk Khatib (Kaskazini Pemba) pamoja na Mattar Zahor Masoud , mkoa wa Kusini Pemba.
Amesema viongozi hao wana jukumu la kuandaa utaratibu maalum utaowawezesha wananchi kuwasilisha kero mbali mbali zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi wa haraka, huku akiwataka kutokuwa sehemu ya kero hizo kwa kigezo kuwa wapo baadhi ya viongozi wanaojihusisha katika migogoro mbali mbali ikiwemo ya ardhi.
Aidha, aliwataka viongozi hao kuondokana na utamaduni wa kuoneana aibu au muhali, pamoja na kuwataka kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo iliomo Mikoani mwao hata kama miradi hiyo inatekelezwa na Wizara za Serikali.
Dk. Mwinyi aliwataka Wakuu hao wa Mikoa kujiridhisha iwapo miradi inayotekelezwa katika Mikoa yao inaendana na thamani halisi ya fedha zilizotumika.
Sambamba na hayo, aliwataka viongozi hao kuzifuatilia kwa karibu Manispaa na Halmashauri zilizomo Mikoani mwao kutokana na utendaji wa kazi usioridhisha, kiasi cha kushindwa hata kukusanya taka pamoja na kusimamia makusanyo ya fedha.

Post a Comment

0 Comments