Na Mwandishi Wetu, Zanzibar:
“Wakanivuta kwa nguvu na kunitia kwenye gari nyeusi”
Ni simulizi ya Salma Said, mwandishi wa habari wa idhaa ya Kiswahili ya DW, aliyepitia tukio la kutisha mnamo Machi 18, 2016 alipotekwa na watu wasiojulikana nje ya Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
“Nimetoka nje katika uwanja wa ndege mbele nikaona gari nyeusi imesimama, wakatoka watu wakaniingiza kwa nguvu,” alisema Salma akiwa mafichoni.
Kisa hicho kilizua hofu miongoni mwa wanahabari, hasa kutoka Zanzibar, ambako matukio yanayoashiria dhuluma dhidi ya waandishi wa habari yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara.
Mnamo Aprili 21, 2021, Jesse Mikofu, mwandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), alishambuliwa na askari wa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) alipokuwa akitekeleza majukumu yake ya kazi.
Mikofu alikumbwa na mkasa huo baada ya kuwapiga picha askari waliokuwa wakiwahamisha wafanyabiashara wadogowadogo katika eneo la Darajani, Mjini Unguja.
Kisa kingine kilitokea Juni 20, 2022, ambapo Yasir Mkubwa, mwandishi wa habari kutoka kituo cha televisheni cha RVS, alikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi Madema Mjini Zanzibar.
Alikamatwa mara baada ya kushiriki mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari yaliyoandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Hakuwa ametenda kosa lolote, bali alikuwa katika utekelezaji wa kazi yake ya uandishi.
Haya ni baadhi ya matukio yanayodhihirisha hali tete ya uhuru wa habari Zanzibar. Wadau mbalimbali wa sekta ya habari na watetezi wa haki za binadamu wamekuwa wakiyataja matukio hayo kama dalili ya mazingira kandamizi yanayowakabili wanahabari visiwani humo.
Katika dunia ya sasa inayoshuhudia muunganiko wa kidijitali na kasi ya maendeleo ya kiteknolojia, uhuru wa habari ni msingi muhimu wa demokrasia, uwajibikaji wa serikali na maendeleo ya kijamii. Habari hutoa mwanga unaowasaidia wananchi kuelewa hali halisi ya nchi yao, kushiriki katika maamuzi na kudai haki zao.
Hata hivyo, uhuru huo wa msingi unakabiliwa na changamoto kubwa visiwani Zanzibar, hasa kutokana na uwepo wa sheria zilizopitwa na wakati ambazo zinatajwa kubana na kudhibiti vyombo vya habari kwa njia zisizo rafiki.
Zanzibar bado inatumia Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu Na. 5 ya mwaka 1988 na Sheria ya Tume ya Utangazaji Na. 7 ya mwaka 1997. Sheria hizi hazijafanyiwa marekebisho makubwa licha ya mabadiliko makubwa ya kijamii, kiteknolojia na kisiasa.
Mojawapo ya malalamiko makubwa kutoka kwa wadau ni kwamba sheria hizo zinatoa mamlaka makubwa kwa Waziri wa Habari na kwa maofisa wa polisi wenye vyeo vya juu, ikiwa ni pamoja na uwezo wa kufungia, kusitisha au kufuta vyombo vya habari kwa kile kinachotajwa kuwa “usalama wa taifa” au “maslahi ya umma.”
Wadau mbalimbali wa habari, wakiwemo waandishi, wahariri, wataalamu wa sheria na wanaharakati wa haki za binadamu wamekuwa wakieleza bayana hofu yao juu ya sheria hizo, wakisisitiza kuwa mazingira yaliyopo hayaruhusu uhuru wa kweli wa uandishi.
Katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani mwaka 2022, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, alikiri kuwepo kwa mazingira yasiyo rafiki kwa wanahabari.
“Tunafahamu jinsi ambavyo baadhi ya viongozi wa serikali, taasisi za umma na jumuiya za kiraia wanavyoficha habari, hasa zile zinazotoa sura mbaya au kukosoa vitendo vyao. Wengine hudiriki kuwafukuza waandishi, kuwakaripia na hata kuwatisha wanapojaribu kutafuta undani wa suala lenye harufu ya uzembe, ubadhirifu, rushwa na ufisadi,” alisema.
Aliongeza kuwa mchakato wa kurekebisha sheria za habari umekuwa wa muda mrefu na kuahidi kwamba serikali itahimiza taasisi husika kuharakisha mapitio hayo ya kisheria.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Imane Duwe, alieleza kuwa vikao na mijadala juu ya mabadiliko ya sheria hizo vimekuwa vikifanyika kwa muda mrefu bila kuzaa matunda.
“Serikali haitakiwi kuwaona waandishi kama maadui, bali washirika wa maendeleo,” alisema. Alisisitiza kuwa kuna umuhimu wa kuwa na sheria rafiki zinazolingana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya sekta ya habari.
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ), Dkt. Mzuri Issa, naye alieleza kwamba mchakato wa mabadiliko umekuwa wa muda mrefu mno.
“Sisi wengine tangu tuko waandishi chipukizi tunazungumzia kupata hizi sheria mpya za habari. Tangu mwaka 2008 kwa kweli ni muda mrefu. Tunahitaji kusimamia jambo hili kwa umoja wetu na hatimaye tupate sheria mpya za habari Zanzibar,” alisema.
Mwanaharakati wa demokrasia, Almas Mohamed, alisema kuwa uhuru wa habari ni kigezo muhimu cha kuwepo kwa utawala bora.
“Huwezi kusema una demokrasia kama wananchi hawana uhuru wa kuhoji, kukosoa, na kuelewa kinachoendelea Serikalini. Vyombo vya habari vinapobanwa, basi hata wananchi wanabanwa,” alisema kwa msisitizo.
Hali hii imeendelea kuzua wasiwasi mkubwa miongoni mwa wanahabari na wadau wa maendeleo, ambao wanaamini kuwa bila kuwa na sheria rafiki, vyombo vya habari haviwezi kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi, na hivyo kuhatarisha maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Kwa msingi huo, wito wa pamoja umetolewa kwa serikali ya Zanzibar kuharakisha mchakato wa kurekebisha sheria za habari, kwa kushirikiana na wadau wote muhimu ili kujenga mazingira wezeshi kwa uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza.
0 Comments