Ticker

6/recent/ticker-posts

Zanzibar Na Safari Ya Kupigania Uhuru Wa Habari Wa Kweli

 


Na Ahmed Abdulla

Katika zama za utandawazi na maendeleo ya teknolojia ya habari, uhuru wa kujieleza ni nguzo muhimu ya kukuza demokrasia, uwajibikaji wa viongozi na maendeleo ya kijamii.

Kwa mujibu wa wataalamu wa haki za binadamu, hakuna jamii inayoweza kupiga hatua bila watu wake kuwa huru kutoa mawazo na maoni bila woga.

Licha ya Zanzibar kuwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwa na Katiba ya mwaka 1977 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 zinazotambua haki ya uhuru wa kujieleza, bado utekelezaji wake unakumbwa na changamoto nyingi.

Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu ya mwaka 1988 imeendelea kuonekana kama kikwazo kikuu katika kulinda haki hiyo ya msingi.

Kifungu cha 27(2) cha Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu ya mwaka 1988 kinampa hakimu mamlaka ya kutoa hati kwa polisi wa cheo cha Inspekta kufanya upekuzi na ukamataji katika maeneo yanayoshukiwa kuchapisha magazeti kinyume cha sheria hata bila ushahidi wa moja kwa moja.

Wadau wa habari wanasema kifungu hiki kinatishia uhuru wa habari na faragha ya watu, kwani kinatoa nguvu kubwa kwa vyombo vya dola bila uwajibikaji wa kutosha.

Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya Tanzania, imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa inayotambua na kulinda haki ya uhuru wa kujieleza.

Miongoni mwa mikataba hiyo ni pamoja na Tamko la Ulimwengu la Haki za Binadamu (UDHR), 1948 – Ibara ya 19 inaeleza kuwa "Kila mtu ana haki ya kuwa na maoni na kutoa maoni yake bila kuingiliwa. Ana haki ya kutafuta, kupokea na kusambaza taarifa na mawazo kwa njia yoyote ile, bila kujali mipaka."

Mkataba mwengine ni Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR), 1966 Ibara ya 19 inaeleza kuwa "Kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake bila kuingiliwa. Kila mtu ana haki ya kutafuta, kupokea, na kusambaza habari na mawazo za aina yoyote, kwa njia yoyote ile."

Kwa Afrika upo mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (ACHPR), 1981ambao nao katika ibara ya Ibara ya 9 umefafanua kuwa "Kila mtu ana haki ya kupata taarifa. Kila mtu ana haki ya kueleza na kusambaza maoni yake kwa mujibu wa sheria."

Hata hivyo, tafsiri ya ndani ya sheria kama ya mwaka 1988 imeendelea kutengeneza pengo kati ya yale yanayotamkwa kimataifa na hali halisi ya uhuru wa habari Zanzibar.

Aidha, kuna misingi ya kikatiba inayotambua uhuru wa habari.

Kwa upande wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 ibara ya 18 inasema “Kila mtu ana haki ya kupata habari, haki ya kuwasilisha maoni, na haki ya kujulishwa kuhusu matukio muhimu kwa maisha na shughuli za jamii”.

Katiba ya Zanzibar, 1984 nayo inatambua uhuru wa kujieleza na uhuru wa kupata habari kama Ibara ya 19 inavyoeleza.

“Kila mtu ana haki ya uhuru wa mawazo na kutoa maoni bila kuathiri sheria au haki za watu wengine” inaeleza katiba

Wakat wadau wa habari Zanzibar wakiwa wanadai sheria bora ya habari visiwani humo lakini zipo baadhi ya nchi za Afrika zimefanikiwa kuweka mifumo bora ya kisheria inayolinda uhuru wa habari.

Afrika Kusini ni moja ya nchi iliyopiga hatua kwrnye sheria za habari Ina Katiba yenye misingi imara ya uhuru wa habari.

Mahakama Kuu huchukua msimamo wa kulinda vyombo vya habari dhidi ya vitisho.

Kenya nayo Kupitia Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa ya mwaka 2016, wananchi wanaweza kupata taarifa rasmi kutoka kwa taasisi za umma, jambo linaloimarisha uwajibikaji.

Namibia ni nchi nyingine iliyoendele kuorodheshwa kuwa miongoni mwa nchi bora Afrika kwa mazingira ya kazi ya waandishi wa habari, kulingana na waandishi wasio na mipaka.

Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ, Dkt. Mzuri Issa, anasisitiza kuwa sheria ya sasa haiendani na mazingira ya kidemokrasia. Anasema kwa maendeleo ya kweli, Zanzibar inahitaji sheria bora inayolinda uhuru wa habari kwa wote.

Wadau wengine wa habari, kama Juma Khamis, wanaamini kuwa mazingira bora ya kisheria yataifanya Zanzibar kupiga hatua kubwa na kuwa mfano bora barani Afrika.

“Ninaamini kwamba iwapo mazingira bora ya kisheria yatawekwa, Zanzibar itapiga hatua kubwa zaidi za kimaendeleo na kuwa mfano kwa mataifa mengine duniani kote.” Anasema

Issa Yussuf naye anatoa wito kwa waandishi kutambua sheria wanazozifanyia kazi ili kujilinda na kuimarisha weledi wao.

“Licha ya changamoto zilizopo, bado kuna umuhimu mkubwa kwa wanahabari kufahamu na kuelewa sheria wanazofanyia kazi kila siku ili waweze kujilinda na kufanya kazi zao kwa ufanisi na usalama zaidi.” Anasema

Zanzibar inayo nafasi ya kipekee kujifunza kutoka kwa mataifa mengine, kurudi mezani na kuandaa sheria mpya ya habari itakayozingatia haki za binadamu, uwazi, na uwajibikaji.

Ni wakati wa kutambua kuwa bila uhuru wa habari, maendeleo hayawezi kufikiwa. Sheria mpya isiwe kikwazo, bali iwe dira ya uhuru, haki na ustawi wa wananchi wa Zanzibar.


Post a Comment

0 Comments