NA BEREMA SULEIMAN.
Kwa muda mrefu sasa, waandishi wa habari na vyombo vya habari visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira yasiyo rafiki, yakihodhiwa na sheria kandamizi, vitisho, na hofu. Hali hii imeendelea kuathiri si tu taaluma ya habari, bali pia haki ya wananchi kupata taarifa sahihi, kwa wakati, na kwa uhuru.
Moja ya sheria inayotajwa kuwa kikwazo kikubwa ni Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu namba 5 ya mwaka 1988, ambayo ilifanyiwa marekebisho na Sheria namba 8 ya mwaka 1997. Kifungu kinacholalamikiwa zaidi katika sheria hiyo ni Kifungu cha 27(1) kinachompa afisa wa polisi mamlaka ya kukamata gazeti lolote popote lilipo ikiwa ana “shaka” kuwa limekiuka sheria.
Kifungu hiki si tu kwamba kinakiuka misingi ya haki na utawala bora, bali pia kinapingana moja kwa moja na Katiba ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambazo zinatambua uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa vyombo
Katika makala hii ilipata nafasi ya kuzungumza na wadau wa habari ambao walionesha wasiwasi mkubwa juu ya vifungu hivi vya sheria katika tasnia ya habari katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku katika kutoa tarifa kwa umma.
Suleiman Said ni mwandishi wa habari wa kujitegemea alisema iwapo sheria haitafanyiwa marekebisho katika vifungu ambavyo vinakwanza uhuru wa habari na vyombo vya habari katika kutekeleza wajiu wao wa kutoa tarifa kwa maslahi mapana ya tasnia ya habari na wandishi wa habari.
“Tunafanya kazi kwa uoga mkubwa. Sheria hizi zinatunyima nafasi ya kutoa habari kwa uhalisia na kuikosoa serikali pale inaposhindwa kutekeleza wajibu wake.”alisema Suleiman
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Masuala ya Sheria Habari Zanzibar (ZAMECO) Jabir Idrisa alisema tasnia ya habari inapaswa kuheshimiwa kama tasnia nyengine hivyo ni vyema mamlaka ya taaluma ya habari isingiliwe na mamlaka nyengine.
“Kumpa afisa wa polisi mamlaka ya ‘kushuku’ na kuchukua hatua dhidi ya gazeti ni sawa na kuweka vizuizi visivyo vya haki kwa tasnia ya habari. Hii inaua uhuru wa kujieleza.”alisema Jabir.
Kwa upande wake mkurugenzi wa shirika la mswaada wa kisheria na haki za binadamu Harusi Miraji Mpatani alisema kwa sasa inapaswa kuangalia zaid uhuru wa habari katika kutoa tarifa kwani ikiwa tumekubali kuridhia mikataba mbalimbali ya kitaifa kikandana kimataifa hakuna budi tukaendana na matakwa ya mikataba hiyo.
“Sheria hizi zinapingana na Katiba hivyo hatuwezi kuwa na taifa huru ikiwa sauti za watu zinanyamazishwa kwa sheria za zamani ambazo zimepitwa na wakati.”alieleza
Alieleza kuwa ni wazi kuwa kuna haja ya dharura ya kufanyia marekebisho sheria zote kandamizi zinazotumika kuzuia uhuru wa vyombo vya habari kwani wanahabari wanahitaji kulindwa, si kutishwa.
Aidha alisema pia wananchi wanastahili kupata taarifa bila kupitia vichujio vya mamlaka, na kwa uhakika wa ukweli.
Hata hivyo alisema ikiwa taifa linadhamiria kujenga jamii inayojali uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi, basi uhuru wa habari ni lazima ulindwe kisheria, kimazingira na kiutendaji.
Alisema Sheria yoyote inayokinzana na Katiba na haki za msingi, ni lazima iangaliwe upya.
Nae kwa upande wake mwanasheria na wakili wa kujitegemea Omar Sheha, alisema sheria kandamizi zinazonyima uhuru wa vyombo vya habari visiwani Zanzibar alisema kuwa ni wakati sasa wa kufanya marekebisho ya kina ili kulinda uhuru wa kujieleza na kupata habari.
Aliendelea kusema kuwa baadhi ya vipengele vya sheria kama Sheria ya Magazeti Na. 5 ya Mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho Na. 8 ya mwaka 1997, vinaipa serikali mamlaka makubwa ya kusimamisha au kufuta leseni za magazeti au vyombo vya habari bila sababu za msingi, jambo linalotishia uhuru wa vyombo vya habari na kusababisha hofu kwa waandishi.
"Sheria hizi zimepitwa na wakati, zinapingana na misingi ya kidemokrasia na haki za binadamu hivyo ziinatoa nafasi ya kuingilia kazi ya uandishi wa habari, jambo ambalo linadhoofisha uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi," alisema Sheha.
Kwa upande wao, baadhi ya wanajamii waliotoa maoni yao kuhusu suala hilo walisema kuwa vyombo vya habari ni sauti ya wananchi, na visipokuwa huru havitaweza kufikisha kilio chao kwa viongozi au jamii nzima.
Asha Suleiman, mkazi wa Regeza mwendo Mwera alisema, “Vyombo vya habari vinatakiwa kuwa huru ili viweze kufichua maovu na kuwezesha wananchi kupata taarifa sahih, ambazo zitasaidia kuhakikisha umma uanapata tarifa zinazoendelea katika sekta zote.
Naye Subira Abdalla mwanafunzi wa chuo cha uandishi wa habari Mwenge Community College MCC, alisema kuwa sheria hizo huzuia waandishi kufanya kazi zao kwa ujasiri, na hivyo kusababisha taarifa nyingi muhimu kukosa kuifikia jamii.
Juhudi za makundi ya watetezi wa haki za binadamu na uhuru wa habari zimeendelea kuongezeka, wakihimiza maboresho ya sheria hizi kwa kushirikisha wadau wote wa habari ili kujenga mazingira salama na huru kwa uandishi wa habari na vyombo vya habari.
0 Comments