Na Ahmed Abdulla, Zanzibar:
“Sheria ni msingi wa haki amani na maendeleo kwa kila
nchi “Hayo si maneno yangu bali yalikuwa ni
maneno ya Raisi wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
alipokuwa akizindua toleo jipya la juzuu za sheria mwezi Aprili ,2025 jijini Dar es salaam.
Anasema, bila ya sheria kuwa wazi uhakika wa ulinzi wa
haki za raia unatoweka au unakuwa hauna uhakika na kusababisha uvunyifu wa
amani.
Wandishi wa Habari Zanzibar wamekuwa wakidai sheria
nzuri na rafiki ya habari bila ya mafanikio yoyote.Kutokana na kutumia sheria
ya zamaani na iliyopitwa na wakati
iliyotungwa tokea miaka ya 1988 ambayo kwa sasa ni kikwazo kwa wandishi
wa habari.
Akizungumzia kuhusu sheria hiyo, mwandishi nguli wa
habari visiwani Zanzibar, Salma Lusangi anasema ni muhimu kwa sasa sheria hiyo
ibadilishwe ili iendane na wakati na kukidhi matakwa ya wakati husika.
“Kwa kipindi kirefu tumekuwa tukifanya uchechemuzi wa
sheria mbili kuu yaani sheria ya Wakala wa Habari Magazeti na Vitabu ya mwaka
(1988) na sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar (1997) ambazo waathirika
wakubwa ni wandishi wa habari na jamii kwa ujumla” anasema Salma na kuongeza
kuwa.
“Sheria za Habari zilipotungwa kulikuwa hakuna
mitandao ya kijamii ila sasa tuna mitandao ya kijamii hivyo ni lazima twende na
wakati, sheria iifanyiwe marekebisho ili iwe rafiki na ilete tija”.
Salim Said ni mhariri na Mjumbe wa Jukwaa la Wahiriri
Tanzania TEF anasema anaamini kwamba nia
ya kupatikana sheria mpya ya habari haipo kwa Serikali ya Zanzibar, kwani
haitaki kuifanyia kazi suala la marekebisho ya sheria za habari na badala yake
imekuwa ikifanya udanganyifu kwa kutoa ahadi za uongo.
“Tokea suala hili lizungumzwe na sisi wadau wa habari,
tumekuwa tukipewa ahadi tofauti, mfano tupo njiani, tupo mbioni hizo hazina
mwanzo wala mwisho, hata Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi alipoingia
madarakani tulikutana nae, alituahidi hivyo na mpaka sasa hakuna
kilichofanyika” anasema Salim.
Salim hakuishia hapo anaona kuwa Waziri wa Wizara
hiyo Tabia Maulid Mwita imekuwa tabia
yake , kila anapoulizwa kwa takribani mara tatu 3 ameahidi mswada huo utasomwa
katika Baraza la Wakilishi ahadi ambayo hadi sasa haijatimia.
“Katika miaka 20 hii tunayopigania uhuru wa habari,
tunashuhudia Baraza la Wawakilishi Zanzibar limepokea na kuzirekebisha au
kutunga sheria zaidi ya 10 lakini wanaifumbia macho sheria ya habari”.
Anawasihi viongozi kuiga mifano ya nchi jirani na
wanapaswa kujiuliza kwanini nchi kama Uganda, Rwanda na Tanzania bara wamefanya
marekebisho ya sheria na kuweka mazingira mazuri ya waandishi wa habari kupaza
sauti zao na kutoa maoni ya wananchi.
Kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba
2025, wandishi wa habari wanabanwa kufanya kazi zao kwa uwazi na wanapojaribu
kuhoji kuhusiana na kitu fulani wanaitwa wachochezi.
Mwanaharakati na mtetezi wa maswala ya habari Zanzibar
Juma Khamis Juma, anasema sheria ya habari ni muhimu katika kuimarisha uhuru wa
kujieleza na kutoa maoni katika nchi yoyote duniani.
“Zanzibar ni
sehemu ya nchi hizo, ingawa sheria iliyopo ni ya muda mrefu ambayo imetungwa
tokea mwaka 1988, miaka mitatu ijayo itatimiza miaka 40, hivyo bila shaka kuna
haja ya kuwa na sheria mpya ya habari”.
Juma anaogeza kuwa, sheria ya sasa ya habari ina
changamoto ambazo wadau wanaamini zinawakwaza katika utekelezaji wa majukumu
yao, ikiwemo mamlaka makubwa aliyopewa askari polisi kuingia katika chombo cha
habari bila ya idhini au kwa idhini ya mahkama.
“Sheria pekee haiwezi kusaidia kuboresha mazingira ya
kazi, lakini uwepo wa sheria na utashi wa kuitekeleza ndio utaleta mabadiliko
yenyewe”.
Suala la haki za kibinaadam linalenga pia uwepo wa
sheria zinazoangalia mustakbali wa uhuru wa kupata, kutafuta na kupokea taarifa
au habari, Mkurugenzi Mtendaji wa
Shirika la Msaada wa Kisheria Zanzibar (ZALHO) Harusi Miraji Mpatani
anasema suala la uhuru wa habari ni suala la haki ambayo imeelezwa katika kifungu cha 18 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ambayo inasema kila raia ana haki ya kutoa na kupokea taarifa.
“Tunahitaji sheria ambazo zitaamini kuwa suala la
habari ni suala la haki, ambayo inatakiwa kutolewa bila ya makando kando yoyote
ambayo unapewa kwa mkono wa kushoto na unanyang’anywa kwa mkono wa kulia”
anasema Harusi kwa msisitizo huku akiongeza kuwa kuna athari kubwa kwa jamii
kama hakuna sheria nzuri za habari kwani kutapelekea kuenea kwa habari zisizo
sahihi.
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania
TAMWA-Z wamekuwa katika harakati za mageuzi kwenye suala la uhuru wa habari na
kupatikana kwa sheria nzuri zitakazolinda maslahi na usalama wao.
Afisa mradi wa masuala ya utetezi na uchechemuzi
kutoka TAMWA-Z Zaina Abdallah Mzee anasema kuwa wanachukuwa jitihada mbalimbali
za kuzisemea sheria zote zinazohusu habari ambazo haziko huru na rafiki kwa
waandishi wa habari na vyombo vya habari
ambazo ni sheria ya Wakala wa Habari Vitabu na Magazeti ya mwaka 1988,
Sheria ya Tume ya Utangazaji, Sheria ya Uchaguzi na nyenginezo ambapo sheria
zote hizi zinawagusa waandishi wa habari na vyombo vya habari na badala yake
kupendekeza kuwekwa sheria moja tu ambayo ni rafiki kwa waandishi wa habari na
vyombo vya habari katika kazi zao.
“Tumekuwa tukipaza sauti zetu kwa muda mrefu sasa
kupatikana sheria mpya ya habari Zanzibar kuzisemea sheria ambazo zina
mapungufu kwa waandishi wa habari na badala yake kupendekeza sheria moja tu
ambayo ni rafiki kwa waandishi wa habari”.
Zaina anaelezea mashirikiano yao baina ya Kamati ya
Wataalam wa Masuala ya Habari Zanzibar ZAMECO na serikali ikiwa ni pamoja na
kukutana na kufanya mazungumzo na
viongozi wa nchi akiwemo Rais na Waziri
wa Habari ,Tume ya kurekebisha sheria ,Idara ya habari maelezo na wajumbe wa
baraza la wawakilishi ambapo wote hawa wamekiri kuwepo kwa mapungufu katika
sheria ya habari iliyopo.
“Mashirikiano ni mazuri baina yetu na serikali kwani
tumepata kufanya mazungumzo na viongozi mbali mbali wa nchi na wao wamekiri
kuwepo kwa mapungufu katika sheria ya habari iliyopo na kuwahidi kufanyia
marekebisho”.
Abdallah Mfaume ni mjumbe wa Kamati ya Wataalam wa
Masuala ya Habari Zanzibar ZAMECO anasema kuna umuhimu mkubwa wa kuharakishwa
kwa sheria mpya ya habari ili iwasaidie waandishi wa habari hasa katika
kutekeleza majukumu yao.
“Waandishi wa habari wanahitaji utulivu, usalama na
ulinzi ili jamii inufaike kupitia fani hiyo ambayo ndiyo yenye jukumu la
kuhabarisha jamii”.
Baraza la Habari Tanzania MCT lilikuwa mstari wa mbele
katika kuhakikisha kunawepo kwa mabadiliko ya Sheria za Habari Tanzania bara
wakifanya shughuli zao hapa Zanzibar wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kuwepo
kwa sheria mpya na rafiki kwa wana habari.
Ziada Kilobo ni Msimamizi wa Ofisi ya Baraza la Habari
Tanzania upande wa Zanzibar anasema kuwa suala la sheria nzuri za habari ni
suala la kupewa kipaombele hasa kwa nyakati hizi ambazo tunaelekea kwenye
uchaguzi.
“Kukiwa na sheria nzuri wanahabari wanaweza kuwasaidia
wakafanya kazi zao kwa weledi na kuna umuhimu wa kuwa na sheria mpya na zenye
kulinda maslahi ya waandishi na hata jamii”
Ziada ameongeza kuwa kwa upande wa serikali ni vyema
kuona suala hili kuwa linahusua maisha ya jamii zaidi.
“Serikali ione suala hili kuwa ni muhimu kwa nchi na
kwa jamii maana uhuru wa Habari ni suala linalotoa nafasi kwa waandishi
kuzisemea changamoto na mafanikio yaliyopo kwenye jamii yao”.
0 Comments