Na
Thuwaiba Habibu,Zanzibar:
Licha ya kuwa wanahabari ni wahabarishaji wakubwa wa
umma lakini wanakabiliwa na vikwazo
vingi katika utendaji kazi zao ambavyo vinahatarisha usalama wa maisha yao
ikiwamo kuuawa, udhalilishaji, utekwaji na uporwaji wa vifaa vyao; yote hayo
hutokea kwa sababu hawana sheria rafiki ambayo ingeliweza kutoa ulinzi dhidi yao.
Hii imebainika baada ya waandishi wa habari kuonesha
vikwazo vinavyotokea baada ya wao kukosa ulinzi
Mwandishi wa habari wa Mihra Tv 0nline Haji Bakari
anasema wakati vyombo vya habari
vinakosa ulinzi, kuna uwezekano mkubwa wa kupungua kwa ubora wa taarifa
zinazotolewa. na wanahabari wanaweza kujiwekea mipaka katika kuripoti habari
muhimu kutokana na hofu inayowakabili.
Pia anasema kupungua kwa uhuru wa vyombo vya habari na
ulinzi wa waandishi wa habari kunababisha waandishi wengi kufuata matakwa ya
watu na siyo maadili ya uandishi wa
habari. anaeleza Haji.
"Bila ya kuwa na sheria rafiki za habari utendaji
kazi wa waandishi wa habari unakuwa mgumu"
Mwandishi wa ZBC Tv Jamila Thabit Kombo anasema lipo
tatizo la kupotosha taarifa; waandishi wa habari wanaweza kutoa taarifa ambayo
si sahihi au kwa kutokutoa taarifa kabisa kwani kufanya hivyo ndiyo wanaamini
watakuwa wamenusuru maisha yao na usalama.
Anasema
wanahabari wanaweza kuwa wahanga wa unyanyasaji, kama vile kutekwa,
kupigwa, kuharibiwa vitendea kazi vyao, kuteremshwa kutoka kwenye chombo cha
usafiri na kuachwa mwituni; Kusema kweli bila ya kuwapo kwa sheria
zinazowalinda wanahabari kunawafanya wawe katika hatari kubwa zaidi ya
unyanyasaji.
"Kuna mifano mingi ya waandishi ambayo tayari
wameshafanyiwa unyanyasaji na bado hauwezi kukoma kwa sababu hakuna sheria
inayowalinda,” anasema Jamila.
Mwandishi wa habari na Mjumbe wa Kamati ya
Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar
(ZAMECO) Jabir Idirisa anasema yeye ni miongoni mwa waandishi
waliokumbana na mashtaka kwa kufunguliwa kesi ambayo aliishi nayo kwa muda wa
miaka 6 kuanzia Januari 2016 hadi Septemba 2021 akituhumiwa
kufanya uchochezi kwa kutimiza wajibu wake wa kutoa taarifa ambayo ni haki ya
wananchi.
"Ni muhimu kuwa na sheria rafiki ambayo inaondoa
hali ya kudhibiti sana vyombo vya habari
na itakuwa imewapa uhuru waandishi wa kufanya kazi zao."
Mwandishi Zulfa Juma Silima anasema vyombo vya habari
vina jukumu muhimu katika kudumisha demokrasia. Kukosekana kwa ulinzi kunaweza
kuathiri uwezo wao wa kuchunguza na kutoa taarifa kuhusu ufisadi, ukiukwaji wa
haki za binadamu na masuala mengine ya kijamii.
"kukosekana kwa ulinzi wa vyombo vya habari na
wanahabari kunaweza kuchangia changamoto nyingi ambazo zinaweza kuathiri si tu
wanahabari wenyewe bali pia jamii nzima inayotegemea taarifa sahihi na
huru."
Katibu wa Klabu
ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC) Mwinyimvua Abdi Nzukwi anasema
kukosekana kwa ulinzi wa waandishi ndani ya sheria ya Usajili wa Wakala wa Magazeti na Vitabu, Na 5
ya mwaka 1997 iliyofanyiwa marekebisho na Sheria Na. 8 mwaka 2010; ni kikwazo
cha kutamani sheria ambayo itakuwa ndio mtetezi wao kwasababu sheria hii
imeingiwa Mamlaka yake na sekta
nyengine.
"kukosekana kwa ulinzi kwa waandishi wa habari
kupelekea waandishi kutowezesha kutoa baadhi ya taarifa na kufanya hivyo ni
kuminya uhuru wa kujieleza na kutoa maoni
ambayo ni haki wa kila mtu"
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania
(TAMWA-ZNZ ) anasema ulinzi na heshima ya waandishi wa habari ipo ndogo kwa
Zanzibar, kwa wakati huu tuliona nao kama huheshimiki na huna ulinzi huwezi
kuwa na uhuru wa kuandika habari.
Dr. Mzuri anasema ipo haja ya kuwapo sheria mpya
ambayo pia itawahakikishia ulinzi na usalama wanahabari wanapofanya kazi zao.
0 Comments