Na Ahmed Abdulla:
Kila ifikapo tarehe 3 Mei, dunia
huadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo
vya Habari Duniani, siku muhimu ya kutafakari nafasi ya vyombo vya
habari katika kuendeleza demokrasia, uwazi, na maendeleo ya jamii.
Kwa mwaka huu, maadhimisho haya
yamebeba uzito wa kipekee visiwani Zanzibar, ambapo kaulimbiu imeelekezwa
kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025 huku kauli mbiu hiyo
ikisema "Sheria nzuri ya Habari ni chachu ya uchaguzi ulio huru na wa
haki."
Katika kuadhimisha siku hiyo, Kamati
ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) ikihusisha Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar
(ZPC), Cahama Cha Waandishi wa Habari Tanzania upande wa Zanzibar TAMWA-Zanzibar,
Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo
Zanzibar (WAHAMAZA) pamoja na Jukwaa la Watetezi wa Haki za Binadamu wameungana
na jamii ya kimataifa kuhimiza upatikanaji wa sheria mpya
ya habari itakayolinda uhuru wa vyombo vya habari na waandishi wake.
Mambo
Matatu Muhimu Yanayoainishwa na ZAMECO:
ZAMECO inasisitiza kuwa ipo haja ya haraka kupatikana kwa sheria mpya ya habari
itakayozingatia Katiba, mikataba ya kikanda na kimataifa juu ya uhuru wa
kujieleza, pamoja na maoni ya wadau.
“Sheria hiyo itasaidia
kujenga msingi wa uchaguzi ulio huru, wenye haki na uwazi” inaeleza taarifa
hiyo
Aidha kamati hiyo inasema Katika
kipindi cha uchaguzi, waandishi wa habari huwa mstari wa mbele kufikisha
taarifa kwa umma. Hata hivyo, bado wapo katika hatari ya vitisho, mashambulizi
na unyanyasaji.
Hivyo ZAMECO inatoa wito kwa vyombo
vya dola, vyama vya siasa na wadau wengine kuhakikisha waandishi wanalindwa
kikamilifu wanapotekeleza majukumu yao.
sambamba na hayo ZAMECO inakemea vikali ubaguzi wowote dhidi ya vyombo vya
habari iwe kwa misingi ya kiitikadi, aina ya chombo au mtazamo wa mhariri.
Pia wanatilia mkazo kuwa utaratibu
wa utoaji wa kadi za kuripoti kutoka Tume ya Uchaguzi uwe wazi, shirikishi, na
usiomwondoa mwandishi yeyote mwenye sifa.
Wito
kwa Serikali na Wadau
Katika hitimisho la taarifa yao,
ZAMECO inatoa wito kwa serikali ya Zanzibar na Tume ya Uchaguzi kuonyesha
dhamira ya kweli kwa kuhakikisha waandishi wanapewa nafasi, heshima na ulinzi
wanaostahili katika utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha, waandishi wa habari na
mashirika yao wanahimizwa kuendelea kudai haki zao kwa njia za amani, na kuwa
mstari wa mbele kulinda misingi ya uwazi na uwajibikaji katika jamii.
"Kuwapo kwa Uhuru wa Habari ni
chachu ya maendeleo katika nchi."
Inamalizia taarifa ya ZAMECO
0 Comments