Na Ahmed Abdulla, Zanzibar:
Kwa miaka kadhaa sasa, tasnia ya habari visiwani
Zanzibar imeendelea kupambana na changamoto nyingi za kisheria zinazowanyima
waandishi wa habari uhuru wa kufanya kazi zao kwa ujasiri na bila woga.
Sheria zilizopo zinatajwa kuwa kandamizi na zimepitwa
na wakati, hali inayoifanya sekta ya habari kuwa katika mazingira magumu na
yasiyotabirika.
Wadau wa sekta ya habari wanasema kuwa sheria hizo
zimekuwa kikwazo kikubwa kwa utekelezaji wa haki ya msingi ya wananchi kupata
taarifa.
Miongoni mwa sheria hizo ni Sheria ya Usajili wa
Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu Na. 5 ya mwaka 1988, iliyorekebishwa na
Sheria Na. 8 ya mwaka 1997, pamoja na Sheria ya Tume ya Utangazaji Na. 7 ya
mwaka 1997, iliyofanyiwa marekebisho na Sheria Na. 1 ya mwaka 2010.
Sheria hizo zinalalamikiwa kwa kutoa mamlaka makubwa
kwa taasisi za serikali kuingilia utendaji wa vyombo vya habari na kudhibiti
usambazaji wa taarifa kwa umma.
Hali hiyo imefanya waandishi wengi kutekeleza majukumu
yao kwa tahadhari kubwa, huku wakikabiliwa na hofu ya kuvunja sheria hizo.
Afisa wa programu ya utetezi wa haki ya habari, Zaina
Abdallah Mzee, anasema kuwa sheria hizo zimewageuza waandishi kuwa walengwa wa
mashinikizo ya kisiasa badala ya kuwa walinzi wa haki ya habari.
“Sheria tulizonazo sasa zinawaweka waandishi katika
hatari, zinawanyima ulinzi wa kisheria na zinakandamiza haki ya wananchi kupata
taarifa,” anasema.
“Tunataka sheria ambayo inalinda, siyo kufifisha uhuru
wa habari.”
Mtaalamu wa sheria, Juma Khamis Juma, anasisitiza kuwa
ili kupata sheria mpya yenye tija, mchakato wa utungaji wake unapaswa kuwa jumuishi
na kushirikisha wadau wa sekta ya habari kuanzia hatua za awali.
“Katika mchakato wa kutunga sheria mpya ya habari,
lazima wadau washirikishwe kikamilifu, vinginevyo tutakuwa tunatibu jeraha kwa
kutumia moto,” anasema.
“Sheria ya habari lazima izingatie muktadha wa sasa wa
teknolojia, uwazi na demokrasia.” anaongeza
Kwa upande wake, Salma Lusangi, mwandishi wa
kujitegemea, anaeleza kuwa mazingira ya sasa yamewafanya waandishi wengi
kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kutokana na hofu ya kuvunja
sheria zisizo rafiki.
“Waandishi wa habari hawawezi kufanya kazi zao kwa
ufanisi kama wanafanyakazi kwa woga,” anaeleza.
“Sheria mpya na rafiki kwa tasnia hii italeta imani
kati ya jamii, vyombo vya habari na serikali.”
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kupitia kifungu cha 18,
inatamka bayana haki ya kila raia kupokea na kupata taarifa.
Hata hivyo, utekelezaji wa haki hiyo umekuwa mgumu
kutokana na kutozingatiwa kwa matakwa ya katiba katika sheria zilizopo.
Harusi Miraji Mpatani, ni Mkurugenzi Mtendaji wa
ZALHO, anasema kuwa bila sheria rafiki, katiba itabaki kuwa karatasi isiyo na
maana kwa wananchi wa kawaida.
“Katiba ya Zanzibar tayari inatambua haki ya kupata
taarifa, lakini bila sheria rafiki, hiyo haki inabaki kuwa maandishi tu,”
amesema.
“Ni wakati sasa serikali iandae na kupitisha sheria ya
habari inayozingatia haki za binadamu na utawala bora.”
Licha ya mijadala ya muda mrefu na ahadi kutoka kwa
mamlaka mbalimbali, hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa hadi sasa
kuhakikisha muswada wa sheria mpya ya habari unapelekwa Baraza la Wawakilishi.
Wanahabari wengi wanaeleza kuwa matumaini yao yanazidi
kufifia huku wakiwa na wasiwasi juu ya mustakabali wa taaluma yao.
Kuelekea uchaguzi mkuu, umuhimu wa kuwa na sheria bora
ya habari hauwezi kupuuzwa. Vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee katika
mchakato wa uchaguzi, na hivyo vinahitaji mazingira ya kisheria
yatakayowawezesha kutekeleza wajibu huo kwa uwazi na usalama.
0 Comments